Dar
es Salaam, Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete kesho anatarajia kuwa mgeni
rasmi kwenye sherehe za mahafali ya kwanza ya kidato cha nne katika
Shule ya Sekondari ya WAMA-Nakayama iliyopo kijiji cha Nyamisati
wilayani Rufiji mkoa wa Pwani.
Kwa
mujibu wa Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo jijini Dar es
Salaam na kusainiwa na Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Wanawake na
Maendeleo (WAMA) ambayo ndiyo inamiliki shule hiyo Daudi Nasib inasema
jumla ya wanafunzi wa kike 67 wanatarajia kuhitimu elimu yao ya kidato cha nne Novemba mwaka huu.
Taarifa hiyo inasema shule ya Sekondari ya WAMA-Nakayama ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya Taasisi ya WAMA na wadau mbalimbali wa maendeleo kutoka
ndani na nje ya nchi wenye mapenzi ya kusaidia jamii. Bodi ya
Wakurugenzi ya WAMA iliamua Shule hiyo iitwe jina hilo kwa heshima ya
Bwana Hayao Nakayama kutoka Japani aliyetoa msaada uliosaidia ujenzi wa awamu ya kwanza ya shule.
“Moja ya malengo ya Taasisi ya WAMA ni kusaidia
upatikanaji wa Elimu bora ya Sekondari kwa watoto wa kike na watoto
wengine waishio katika mazingira hatarishi na yatima. Na ni kwa mantiki
hii ndiyo maana shule ya WAMA- Nakayama imejengwa ili kutimiza lengo hili.
Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA,Mama Salma Kikwete na Bodi ya Wakurugenzi ya
WAMA inapenda kutoa shukrani za dhati kwa wadau wote wanaosaidia Shule
ya WAMA- Nakayama na kuunga mkono juhudi za Taasisi yetu”, ilisema
taarifa ya Nasib.
Shule ya Sekondari ya WAMA- Nakayama ilianza mwaka 2010 ina wanafunzi
wa kike 325 kutoka Mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani ambao ni
yatima na wengine wanatoka familia maskini, watoto hawa wasingeweza kupata elimu ya sekondari bila ya msaada wa Taasisi ya WAMA ambayo
huwapatia mahitaji yao yote bure ikiwemo; malazi, chakula, sare za
shule, shajara, vitabu na nauli za kwenda makwao kipindi cha likizo.
Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) ni Taasisi isiyo ya kiserikali na isiyo ya kibiashara iliyoanzishwa na Mama Salma Kikwete, Mke wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, mwaka 2006 ina malengo ya kuboresha maisha ya wanawake na wasichana katika masuala ya afya, elimu na uchumi pamoja na kutengeneza fursa za maendeleo ya wakina mama na watoto.



Post a Comment