THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
JK: Ni aibu Serikali kudaiwa na wakulima
· Ahidi wakulima wa mahindi kulipwa haraka
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa ni aibu kwa Serikali kudaiwa na
wakulima na amewahakikishia wakulima wa Wilaya ya Ludewa, Mkoa wa Njombe, kuwa
watalipwa haraka iwezekanavyo fedha zao wanazodai kwa kuiuzia Serikali mahindi
yao.
Aidha, Rais Kikwete amethibitisha kuwa meli
ambazo Serikali yake iliahidi kununua kwa ajili ya usafiri katika maziwa makuu
ya Tanzania zinajengwa na zitazinduliwa kabla ya mwaka 2015, zinaweza kuwa meli
mbili badala ya moja kwa kila moja ya maziwa ya Nyasa, Tanganyika na Victoria.
Rais Kikwete ameyasema hayo leo, Jumatatu,
Oktoba 21, 2013, wakati alipozungumza kwa nyakati tofauti katika ziara yake ya
Wilaya ya Ludewa, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kikazi kukagua na
kuzindua miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Njombe.
Rais Kikwete amewaambia wakazi wa Ludewa kwenye
mkutano wa hadhara kuwa ni kweli kuwa Serikali yake inadaiwa kiasi cha Sh.bilioni 17 ikiwa ni
deni la wakulima wa mikoa mbali mbali nchini ambao waliuza mahindi yao ya msimu uliopita kwa kwa Wakala
wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA).
Suala hilo lilijirudia tena wakati Rais Kikwete alipokuwa anapokea Ripoti ya Maendeleo ya Wilaya ya Ludewa ambako ameambiwa kuwa wakulima wa Wilaya hiyo pekee walikuwa bado wanaidai Serikali Sh.bilioni 3.115 ambayo ni thamani ya mahindi tani 6,231 ambayo wakulima hao waliiuzia NFRA.
Rais Kikwete ameambiwa kuwa mpaka sasa wakulima
wa Wilaya ya Ludewa wamelipwa kiasi cha Sh.bilioni 2.839 kutokana na tani za
mahindi tani 5,679. NFRA ilikuwa imelenga
kununua kutoka kwa wakulima wa Wilaya ya Ludewa kiasi cha tani 13,000 lakini
mpaka sasa imeweza kununua tani 11,911 ingawa sehemu kubwa ya kiasi hicho
hakijalipiwa na Serikali.
“Hii ni aibu. Serikali haiwezi kudaiwa na
wakulima. Hizi fedha zitalipwa tu,” amesema Rais Kikwete na kuelezea hatua ambazo amezichukua binafsi
katika siku mbili kuhakikisha wakulima wanalipwa fedha zao.
Rais Kikwete pia amesema kuwa Serikali yake
itaangalia uwezekano wa kununua tani
2,972 za mahindi ya msimu uliopita zilizobakia mikononi mwa wakulima wa Wilaya
hiyo.
“Naambiwa kuwa bado NFRA inahitaji kiasi cha
tani 40,000 hivi ili kukamilisha shehena ya idadi ya kiasi cha tani 250,000 za
mahindi kwa ajili ya Hifadhi ya Taifa mwaka huu. Nitawaambia waangalie kama
wanaweza kununua kiasi hiki kilichobakia mikononi mwa wakulima wa Ludewa.”
Kuhusu maombi ya wananchi wa Ludewa kununua meli
ya kuchukua nafasi ya Mv. Mbeya iliyozama katika Ziwa Nyasa ili kurahisisha
usafiri ndani ya Ziwa hilo ambalo linapakana na Wilaya ya Ludewa, Rais amesema
kuwa Serikali yake inanunua meli hiyo.
“Tunajua kuwa meli ya Mv. Mbeya ilizama katika
Ziwa Malawi na kwa kweli meli zimezama katika maziwa mengine makubwa ya
Tanganyika na Victoria, na mimi kwenye Kampeni niliahidi kuwa nitanunua meli
moja kwa kila ziwa,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Tumeagiza meli tatu kutoka Korea Kusini.
Zinajengwa. Tumeagiza meli nyingine tatu kutoka Denmark. Nazo zinajengwa.
Hivyo, tunaweza kupata siyo meli moja bali meli mbili katika maziwa yote
matatu. Ni matumaini yangu kuwa nitaweza kuzizindua meli hizo kabla ya kumaliza
kipindi changu cha uongozi, mwaka 2015.”
Rais Kikwete pia amefafanua kuhusu kero nyingine
zilizoibuliwa na wakazi wa Wilaya ya Ludewa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa daraja
kwenye Mto Ruhuhu ambao amesema litajengwa.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.


Post a Comment