THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa ni wajibu
wa Halmashauri nchini kuhakikisha kuwa zinawabana wafanyabiashara kulipa kodi
baada ya kununua mazao ya wakulima katika halmashauri hizo.
Rais Kikwete ameshangaa
wakati wa ziara yake kusikia malalamiko ya viongozi wa Mkoa wa Njombe kuwa
wafanyabiashara wanaonunua zao la pareto katika Mkoa huo wamekuwa wanakataa
kulipa ushuru.
“Komesheni ujinga huu wa
watu kununua pareto ya wakulima bila kulipa ushuru na kodi kwa Halmashauri.
Mnajinyima wenyewe raslimali muhimu ya maendeleo yenu kwa kushindwa
kuwalazimisha watu kulipa kodi,” alisema Rais Kikwete jana, Jumatano, Oktoba 23, 2013 mjini Njombe
wakati anazungumza na viongozi wote wa Mkoa huo wakati anamaliza na kujumuisha ziara
yake ya siku saba katika Mkoa huo.
Alisema Rais Kikwete: “Mtapata
wapi fedha za kuendesha halmashauri zetu kama mnashindwa kutoza kodi na ushuru
kwa watu wanaofanya biashara. Hakuna
Serikali duniani inayoendeshwa bila kutoza kodi. Hakuna. Haipo duniani.”
Rais Kikwete amesema: “Kwa
kuwatoza wafanyabiashara wakubwa wanaonunua mazao kodi kunazisaidia Halmashauri
na hata Serikali Kuu kuondokana na ulazima wa kuwatoza wananchi wa kawaida kodi
ndogo ambazo sisi tunaziita kodi za kero na tumezifuta.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
24 Oktoba, 2013


Post a Comment