THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

Rais Kikwete: Kero hii imetosha, sasa ni kitabu kimoja mwanafunzi
mmoja
·
Asema tunao wanasiasa wa kutosha, sasa tunahitaji wanasayansi
·
Aaagiza viongozi katika ngazi zote kutenga fedha za kuwajengea
walimu nyumba katika bajeti zao
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Serikali
yake itakomesha kero ya wanafunzi na watoto wa shule nchini kuchangia vitabu
vya kiada katika masomo yao.
Aidha, Rais Kikwete
amesema kuwa wajibu wa kuhimiza ujenzi wa maabara za sayansi katika shule
nchini siyo tu matakwa ya Rais bali suala hili linatakiwa kuwa wajibu wa kufa
na kupona kwa kila kiongozi katika ngazi zote za uongozi kwa sababu nchi
haiwezi kuendelea bila wanasayansi.
Vile vile, Rais Kikwete
amewaagiza viongozi wote katika ngazi zote na hasa kwenye ngazi ya wilaya na
halmashauri kutenga katika bajeti zao fedha za kujenga nyumba za walimu kwa nia
ya kuboresha mazingira ya kazi ya walimu nchini.
Rais Kikwete amesema na
kutoa maagizo hayo jana, Jumatano, Oktoba 23, 2013, alipozungumza na uongozi wa
Mkoa wa Njombe wakati anakamilisha na kujumuisha ziara yake ya siku saba katika
Mkoa huo kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe.
Rais ambaye alizungumza
masuala mengi kuhusiana na aliyoyaona wakati wa ziara hiyo alijielekeza kwa
muda mrefu katika masuala ya elimu na nafasi ya viongozi katika kusuma mbele
sekta ya elimu kama mkombozi mkuu wa Watanzania.
Kuhusu kupatikana kwa
vitabu vya kiada kwa watoto na wanafunzi nchini, Rais Kikwete amewaambia
viongozi hao wa Njombe:
“Nimeilekeza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
ufundi kuwasilisha kwangu bajeti inayotakiwa kutuwezesha sisi, kama Taifa,
kuhakikisha kuwa kila mtoto wetu na mwanafunzi wa nchi yetu hii anakuwa na kila
kitabu cha kiada kwa kila somo.”
“Hili ni jambo ambalo
tumelizungumza kwa muda mrefu. Hakuwezi kamwe kuendelea kuahirisha majawabu ya
suala hili. Nataka kujua itatugharimu kiasi gani kwa kila mtoto na mwanafunzi
nchini kuwa na kitabu chake cha kiada kwa kila somo. Tumepata msaada wa
marafiki wetu. Tunawashukuru. Lakini sasa wakati umefika kwa sisi wenyewe
kuelekeza nguvu zetu zote kumaliza tatizo hilo,” amesema Rais Kikwete na kusisitiza:
“Ilikuwa wanafunzi 10
kwa kitabu kimoja, tumeshuka hadi wanafunzi watatu kwa kitabu kimoja. Hili
halitoshi na hali hii haikubaliwi ni lazima iwe ni mwanafunzi mmoja na kitabu
kimoja, kitabu chake.”
Kuhusu ujenzi wa maabara
ya sayansi katika kila sekondari nchini na umuhimu wa kufundisha masomo ya
sayansi nchini, Rais Kikwete amesema “ni lazima tujenge hizi maabara haraka, ni
lazima tuongeze kasi yetu ya kufundisha masomo ya sayansi na ni lazima
tukabiliane na uhaba wa walimu wa kufundisha sayansi nchini.”
“Maendeleo ya nchi
huletwa na wanasayansi. Na kama mfumo wa elimu wa nchi yoyote hautoi nafasi ya
kutosha kulea na kujenga wanasayansi basi nchi hiyo inapiga hatua ya kurudi
nyuma. Kwenye hili, tayari tumeachwa na treni na wala suala hili siyo matakwa
ya Rais bali ni suala la kufa na kupona kwa viongozi wote wa ngazi zote,” amesema Rais Kikwete.
Ameongeza: “Siyo
kila mtu katika nchi yetu atakuwa mwanasiasa. Hawa tayari tunao wa kutosha na
wengine kazi yao sasa ni kusababisha ghasia nchini. Tunahitaji wanasayansi
zaidi – tunahitaji madaktari, tunahitaji wahandisi. Ni lazima tuwekeze ipasavyo
katika eneo hili kwa sababu tukikosea sasa tutakuwa tumekosa hatua moja kubwa
na muhimu katika jitihada za kujiletea maendeleo.”
Amesema kuwa anatambua
matatizo yaliyoko katika ufundishaji wa masomo ya sayansi nchini na kuwa kwa
sababu hiyo ameitisha mkutano wa wadau wote wanaohusika na elimu na eneo la
sayansi nchini ambao utafanyika Novemba 3, mwaka huu, kwa nia ya kutafuta
majawabu ya matatizo hayo.
Tanzania inahitaji
walimu 44,007 wa sayansi katika shule zake za sekondari. Waliopo kwa sasa ni
walimu 17,059 na hivyo kuwepo na upungufu wa walimu 26,948 wakati vyuo vyote
nchini vina uwezo wa kuhitimisha walimu 2,100 kwa masomo ya sayansi kila mwaka.
Kuhusu ujenzi wa nyumba
za walimu, Rais Kikwete amesema kuwa kila kiongozi popote alipo ni lazima awe
na mpango kabambe wa kuhimiza ujenzi wa nyumba za walimu na kuweka katika
bajeti yake ya kila mwaka fedha za ujenzi huo.
“Kwenye ngazi ya taifa
tumetoa Sh. Milioni 500 kwa kila Halmashauri nchini mwaka huu kama namna ya
kuanza kukabiliana na tatizo hilo. Mwaka huu wa fedha, tunaanza kwa majaribio
na Halmashauri 40 na ile ya Makete katika Mkoa huu wa Njombe ni mojawapo.
Tutaendelea kutoka fedha kila mwaka huu kwa nia ya kumaliza tatizo hili.”
Ameongeza: “Sasa
kwenye kila ngazi ya wilaya, kaeni chini mtafakari jinsi gani ya kuzitumia
fedha hizo vizuri ili ziweze kujenga nyumba nyingi. Natambua kuwa kwenye sehemu
nyingine shughuli hii itakuwa ngumu unapokuwa na madiwani ambao pia ni
wakandarasi. Lakini hii tutakabiliana nalo.”
Ameelekeza kuwa mbali na
kuzitumia fedha hizo vizuri, pia ametaka kila Halmashauri nchini kutenga fedha
katika bajeti zao za ujenzi wa nyumba za walimu.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
24 Oktoba, 2013


Post a Comment