Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli (pichani), amesema
serikali imeokoa Sh. bilioni 18 kwa kutumia makandarasi wa kizalendo
kujenga Daraja la Mbutu, lililoko Wilaya ya Igunga, mkoani Tabora.Alisema hayo katika ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo na kubainisha kuwa ujenzi wa daraja hilo umegharimu Sh. bilioni 12 badala ya Sh. bilioni 30 endapo lingejengwa na makandarasi wa nje.
Daraja hilo pamoja na tuta la barabara lenye urefu wa kilometa tatu linajengwa na muungano wa makandarasi wa kizalendo 13 unaojulikana kama “Mbutu Bridge Joint Venture' chini ya usimamizi wa muungano wa wahandisi washauri wawili unaojulikana kama Pidael Joint Venture.
Makandarasi hao wanafanya kazi ya kusanifu na kujenga kwa wakati mmoja kwa gharama ya Sh. bilioni 12 na fedha zote zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Mkataba wa ujenzi wa daraja hilo ulisainiwa Aprili, mwaka jana na umepangwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.
“Nimeridhishwa na kasi ya ujenzi wa daraja hili na nimeona tayari mmefikia karibu asilimia 80. Hii ni kazi nzuri inayostahili kupongezwa, kwani mmeanza kudhihirisha uwezo wenu kama makandarasi wazalendo,” alisema Waziri Magufuli na kuwataka makandarasi hao kuhakikisha wanaukamilisha mradi huo kwa muda na viwango vilivyopangwa.
Pia aliwataka wananchi wa maeneo hayo kuhakikisha wanalitumia daraja hilo vizuri, kwani hiyo ni fursa nyingine ya kuwaletea maendeleo.
Hata hivyo, aliwatahadharisha wasafirishaji watakaotumia daraja hilo kuzingatia sheria za usalama barabarani kwa kutozidisha uzito uliowekwa kisheria.
Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Elibariki Kingu, alimshukuru Waziri Magufuli na kusema mambo aliyojionea na kuyatolea maelekezo yatasaidia kukamilika kwa daraja hilo kwa wakati na hivyo kuleta faraja kubwa kwa wananchi wengi wanaoitumia barabara hiyo.
Katika hatua nyingine, Waziri Magufuli aliwahakikishia wananchi wa Igunga kuwa serikali itajenga barabara ya lami kutoka mji wa Igunga hadi Mbutu.
Azma hiyo imetokana na maombi ya wananchi wa maeneo hayo waliyoyatoa katika nyakati tofauti na pia kwa kuzingatia adha iliyokuwa ikiwakabili kiasi cha kufikia baadhi ya wananchi na mifugo yao kupoteza maisha kutokana na kutokuwapo kwa mawasiliano ya barabara na daraja la uhakika katika eneo hilo hasa nyakati za mvua.
CHANZO:
NIPASHE


Post a Comment