Meneja wa Takwimu za Ajira na
Bei toka ofisi ya Taifa ya Takwimu Bi. Ruth Minja akisisitiza jambo kwa
waandishi wa habari (hawapo pichani)Jana jijini Dar es Salaam kuhusu hali ya mfumuko wa bei kwa mwezi Septemba 2013 ambapo umepungua hadi kufikia
asilimia 6.1 kutoka asilimia 6.7 ya mwezi Agosti 2013.
Badhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza kwa makini Meneja wa Takwimu za Ajira na Bei toka ofisi ya Taifa ya Takwimu Bi. Ruth Minja
(hayupo pichani) wakati akielezea hali ya mfumuko wa bei kwa mwezi septemba 2013 ambapo umepungua hadi kufikia
asilimia 6.1 kutoka asilimia 6.7 ya mwezi Agosti 2013 jana jijini Dar es
Salaam.
----
MFUMUKO WA BEI WA
MWEZI SEPTEMBA, 2013
Ndugu waandishi wa habari, Kwanza kabisa napenda kuchukua fursa hii
kuwakaribisha katika Ofisi ya Taifa ya Takwimu na kuwashukuru kwa kuitikia
mwito wa kuhudhuria mkutano huu. Naomba ifahamike kwamba, Ofisi ya Taifa ya
Takwimu ina mamlaka ya kukusanya, kuchambua na kutoa takwimu rasmi za nchi kwa
mujibu wa Sheria ya Takwimu Sura 351. Lengo la mkutano huu ni kuwafahamisha
mambo makuu matatu;
Kwanza ni kuhusu
mfumuko wa bei wa mwezi Septemba 2013 unaopimwa
kwa kigezo cha mwaka, yaani; kwa
kulinganisha fahirisi za bei za mwezi Septemba, 2013 na zile za mwezi Septemba,
2012;
Pili ni kuhusu
mfumuko wa bei wa mwezi Septemba, 2013 unaopimwa
kwa kigezo cha mwezi yaani; kwa
kulinganisha fahirisi za bei za mwezi Septemba, 2013 na zile za mwezi Agosti,
2013 na;
Tatu, Wastani wa
thamani ya Shilingi ya Tanzania mwezi septemba, 2013 ikilinganishwa na mwaka wa
kizio, yaani septemba, 2010.
Ndugu waandishi wa habari, Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Septemba, 2013
umepungua hadi kufikia asilimia 6.1 kutoka asilimia 6.7 mwezi Agosti, 2013.
Kupungua kwa Mfumuko wa Bei wa mwezi Septemba, 2013 kunamaanisha kuwa; kasi ya
upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa mwezi Septemba, 2013 imepungua
ikilinganishwa na kasi ya kupanda kwa bei kwa mwezi Agosti, 2013.
Kupungua kwa Mfumuko
wa Bei kwa mwezi Septemba kumechangiwa na kupungua kwa Mfumuko wa Bei wa bidhaa
za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula.
Aidha, Mfumuko wa Bei
wa bidhaa za vyakula majumbani na migahawani umepungua hadi asilimia 6.9 mwezi
Septemba, 2013 ikilinganishwa na asilimia 7.1 mwezi Agosti, 2013. Kwa upande wa
bidhaa zisizo za vyakula, kasi ya ongezeko la bei imepungua hadi asilimia 6.0
kwa mwezi Septemba, 2013 kutoka asilimia 7.3 mwezi Agosti, 2013.
Ndugu waandishi wa habari, mwenendo wa bei za bidhaa za vyakula hasa mchele
umeonyesha kupungua kwa kiasi kikubwa mwezi Septemba, 2013 zikilinganishwa na
bei za mwezi Septemba, 2012. Kwa wastani bei za mchele zimepungua kwa asilimia
17.2 kwa kipindi cha mwezi Septemba, 2012 na Septemba, 2013. Baadhi ya Mikoa
ambayo imepata unafuu wa bei za mchele ni pamoja na Morogoro (asilimia 29.7),
Singida (asilimia 26.7), Kagera (asilimia 25.0), Manyara (asilimia 16.7) na Dar
es Salaam (asilimia 13.5).
Kwa upande wa bidhaa
za mahindi, matokeo yanaonyesha kuwa bei za bidhaa hiyo zimepungua kwa baadhi
ya mikoa kama; Arusha (asilimia 11.1), Pwani (asilimia 12.5), Rukwa (asilimia
5.0) na Mwanza (asilimia 18.9). Bidhaa nyingine za vyakula zilizoonyesha
kupungua kwa bei kwa baadhi ya mikoa ni pamoja na mafuta ya kupikia ambapo mkoa
wa Mtwara zimeshuka kwa asilimia (4.0), Kagera (asilimia 11.9) na Mwanza
(asilimia 12.1). Bei za maharage mkoani Singida zimeshuka kwa asilimia 33.3,
Dodoma (asilimia 6.3) na Arusha (asilimia 7.7).
Aidha, bidhaa zisizo
za vyakula zilizosababisha kupungua kwa bei mwezi Septemba, 2013
zikilinganishwa na bei za mwezi Septemba, 2012 ni pamoja na petroli na dizeli
ambapo bei za petroli zimepungua kwa asilimia 4.0 na Dizeli kwa asilimia 2.2
katika kipindi hicho. Bidhaa nyingine ni pamoja na gesi kwa baadhi ya mikoa
kama Ruvuma (asilimia 7.0), Rukwa (asilimia 7.0) na Kigoma (asilimia 8.3).
Ikumbukwe kwamba
kupungua kwa Mfumuko wa Bei kunamaanisha kuwa, kuna unafuu wa maisha kwa mlaji,
kwa maana hiyo Tanzania inapiga hatua nzuri katika maendeleo ya kiuchumi.
MFUMUKO WA BEI KWA
KIPIMO CHA MWEZI
Ndugu waandishi wa habari, kwa upande wa mfumko wa bei kwa kipimo cha mwezi,
matokeo yanaonyesha kuwa, Mfumuko wa
Bei wa mwezi Septemba, 2013 umeongezeka kwa asilimia 0.5 ikilinganishwa na
kupungua kwa asilimia 0.1 mwezi Agosti, 2013. Kuongezeka kwa Mfumuko wa Bei kwa
Kipimo cha Mwezi, kumechangiwa na kuongezeka kwa bei za bidhaa za vyakula na
bidhaa zisizo za vyakula.
Baadhi ya bidhaa za
vyakula zilizochangia kuongezeka kwa Mfumuko wa Bei kwa kipimo cha mwezi ni
pamoja na; mahindi (asilimia 0.8), unga wa ngano (asilimia 2.2), samaki wabichi
(asilimia 4.1), matunda (asilimia 4.5), karanga (asilimia 1.6), viazi mviringo
(asilimia 0.9), unga wa muhogo (asilimia 5.2), sukari (asilimia 0.3), asali
(asilimia 3.5) na vitafunwa (asilimia 1.1).
Bidhaa zisizo za
chakula zilizochangia kuongezeka kwa Mfumuko wa Bei kwa kipimo cha mwezi ni;
vitambaa vya nguo (asilimia 0.2), mavazi ya kike (asilimia 0.3), viatu
(asilimia 0.3), mafuta ya taa (asilimia 1.0), samani (asilimia 1.1), vifaa vya
nyumbani vya malazi (asilimia 0.3), vifaa vya nyumbani vya usafi (asilimia
0.3), dizeli (asilimia 1.7) na petroli (asilimia 2.7).
THAMANI YA SHILINGI
YA TANZANIA MWEZI SEPTEMBA, 2013 IKILINGANISHWA NA MWAKA WA KIZIO, YAANI
SEPTEMBA, 2010
Ndugu waandishi wa habari, Wataalamu wa uchumi, takwimu na falsafa wanasema
kwamba, uwezo wa fedha katika kununua bidhaa na huduma mbalimbali una uhusiano
unaokinzana na mwelekeo wa Fahirisi za Bei. Hii ina maana kuwa, kama Fahirisi
za Bei zikipungua, uwezo wa fedha katika kununua bidhaa na huduma unaongezeka.
Kwa maana hiyo, uwezo
wa Shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma umeonyesha kuwa na
mwelekeo imara kwa kipindi chote cha mwaka, yaani kutoka Januari, 2013 hadi
Septemba, 2013. Hii ni kwa sababu fahirisi za bei za Taifa kwa kipindi chote
hicho zimekuwa na mwelekeo ulio imara.
HALI YA MFUMUKO WA
BEI KWA BAADHI YA NCHI ZA AFRIKA MASHARIKI
Ndugu waandishi wa habari, Kwa ujumla, Mfumuko wa Bei nchini una mwelekeo
unaofanana na nchi nyingine za Afrika Mashariki. Mfano; Mfumuko wa Bei nchini
Kenya umeongezeka hadi asilimia 8.29 mwezi Septemba, 2013 kutoka asilimia 6.67
mwezi Agosti, 2013. Nchini Uganda Mfumuko wa Bei umeongezeka pia hadi asilimia
8.0 mwezi Septemba, 2013 kutoka asilimia 7.3 mwezi Agosti, 2013.
Ndugu waandishi wa habari, napenda kuwashukuru kwa mara nyingine tena kwa
kuhudhuria mkutano huu, na natoa wito kwenu juu ya umuhimu wa kuwaelimisha
Watunga Sera, Wafanyabiashara na Wananchi wote kwa ujumla kuhusu umuhimu wa
matumizi ya takwimu hizi za bei na nyinginezo zinazotolewa na Ofisi ya Taifa ya
Takwimu katika kuendesha shughuli zao za kila siku.
Pia ninawaomba sana
wananchi wote kwa ujumla kutoa ushirikiano wa dhati kwa Ofisi zetu za Takwimu
za Mikoa wakati wa ukusanyaji wa takwimu mbali mbali kwa kutoa taarifa zilizo
sahihi na kwa wakati kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.
Kwa hayo machache
ninaomba niishie hapo na ninawakaribisha tena tarehe 08 mwezi Novemba, 2013 kwa
ajilili ya kuwafahamisha Mfumuko wa Bei wa mwezi Oktoba, 2013.
Asanteni kwa kunisikiliza.
Post a Comment