
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akikata utepe kufungua rasmi Chuo cha Ufundi Stadi cha VETA cha Wilaya ya Makete mwishoni mwa juma.
Rais
Jakaya Mrisho Kikwete akishuhudia ubora wa shati lililotengenezwa na
wanafunzio wa Chuo cha Ufundi Stadi cha VETA cha Wilaya ya Makete baada
ya kukifungua rasmi chuo hicho mwishoni mwa juma.
******
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na
serikali yake wameombwa na Mamlaka ya Elimu ya Mafunzo na Ufundi (VETA)
nchini kuangalia upya na kwa haraka, umuhimu wa kuifanya marekebisho
Sheria ya Manunuzi nchini kwa sababu sheria hiyo katika hali yake ya
sasa inarudisha nyuma maendeleo ya VETA na taasisi nyingine nchini.
Mkurugenzi
Mkuu wa VETA, Eng. Zebadayo Moshi amemwambia Rais Kikwete leo, Jumamosi,
Oktoba 19, 2013, kuwa ni vigumu kwa VETA kulazimika kwenda makampuni ya
Toyota ama Scania kila mara kununua magari mapya kwa ajili ya mafunzo
ya wanafunzi wao kwa sababu Sheria hiyo inazuia taasisi za umma kununua
na kutumia vifaa vilivyokwishatumika.
Mkurugenzi
huyo alikuwa akizungumza leo kwenye Sherehe ya Ufunguzi wa Kituo cha
Mafunzo ya Ufundi cha Wilaya ya Makete (MDVTC) cha VETA, mjini Iwawa,
mji mkuu wa Wilaya ya Makete, ambako Rais Kikwete alikuwa mgeni rasmi na
ambaye amefungua rasmi Kituo hicho.
Amesema Eng. Mosha: “Sheria
hii ya manunuzi itaua kabisa shughuli za VETA na taasisi nyingine za
umma nchini. Sisi siku zote, tunafundisha kwa vitendo na hivyo
tunapotaka kumfundisha mwanafunzi gari ni lazima tuwe na gari ama jinsi
injini ya gari inavyofanya kazi ni lazima tuwe na injini. Lakini kwa
sababu Sheria hii inatuzuia kununua vifaa vilivyotumika, tunalazimika
kwenda Toyota ama Scania kununua gari jipya ama injini ya gari mpya.
Hili litatufikisha mbali kweli?”
“Majuzi
tumeanzisha mafunzo ya ndege na injini za ndege zinavyofanyakazi na kwa
sababu ya Sheria hii ni lazima twende Kampuni ya Boeing ya Marekani
kununua injini ya ndege hiyo,” amesema kuwa wananchi walioshiriki sherehe hiyo wakiangua vicheko.
Rais Kikwete amemwambia Mkurugenzi Mkuu huyo wa VETA: “Nimesikia.
Tutazungumza na wahusika kuona nini kinaweza kufanyika. Tulipata
kujaribu kuifanyia marekebisho sheria hii lakini wakubwa wale wakakataa
na kuruhusu taasisi moja tu ya Serikali kuweza kununua vifaa
vilivyokwishakutumika.”
Kituo hicho
cha Ufundi cha VETA cha Wilaya ya Makete ni cha kwanza cha aina yake
kujengwa nchini kwa sababu ni cha kwanza kujengwa kwa dhana ya Ilani ya
Uchaguzi Mkuu ya CCM mwaka 2013 ambayo iliahidi kuanza kujenga vyuo vya
ufundi katika wilaya badala ya mikoa.
Aidha,
Kituo hicho ni cha kwanza cha aina yake nchini kwa kuwa kimejengwa na
wanafunzi na wakufunzi wa Chuo cha VETA Mpanda, Mkoa wa Katavi, jambo
ambalo limeokoa gharama za ujenzi kwa kiasi cha Sh. bilioni 1.45 pamoja
na kwamba mchanga wa ujenzi uliokuwa unachukuliwa kutoka Makambako, mji
mwingine wa Mkoa wa Njombe kwa sababu Makete hakuna mchanga unaofaa kwa
ujenzi wa mithili ya chuo hicho.
Chuo hicho
ambacho ujenzi wake ulianza Aprili 27 mwaka huu kwenye eneo la Kituo
hicho la ekari 124 tayari kina wanafunzi 37 wanaoshiriki mafunzo ya
ufundi ya ushonaji na uashi wakiwa ni miongoni mwa wanafunzi 145,511
ambao wanaendelea na mafunzo katika vyuo vya ufundi pote nchini.
Akizungumza
na wananchi baada ya kufungua Kituo hicho cha kisasa na cha kuvutia,
Rais Kikwete ameipongeza VETA kwa kujenga chuo hicho cha kwanza kwa
dhana mpya ya kufikisha elimu ya ufundi wilayani.
Rais
Kikwete pia ameitaka VETA kuendelea kutoa mafunzo kulingana na mahitaji
ya eneo husika na kutumia raslimali zinazopatikana katika eneo ambako
chuo kipo na kwa Mkoa wa Njombe amesema kuwa anataraji kuwa VETA
itajiekeleza katika ufundi unaohusiana na mazao ya mbao na wa viazi
mviringo.
“Uhodari
wa watu wa Makete hauwezi kuendelea kuwa kupanga viazi ama mbao tayari
kuzipeleka sokoni Dar Es Salaam, Uhodari sasa uwe ni wa kuanzisha
viwanda vya fenicha baada ya vijana wenu kupata mafunzo katika Kituo
hiki ama kutengeneza mapochopocho yanayotokana na viazi. Tunahitaji siku
moja na sisi kusema kuwa fenicha hii safi imetengenezwa Makete.”
Aidha, Rais
Kikwete amesema kuwa VEAT iangalie uwezekano wa kuwapatia wahitimu wake
zana na vifaa vya kuanzia kazi za kujitegemea baada ya kumaliza mafunzo
yao. “Lazima vijana hawa tuwasaidie kujiajiri kwa sababu
tunahitaji sana mafundi stadi na mafundi mchundo kuongeza thamani kwenye
uchumi wetu.”
Rais Kikwete yuko katika ziara ya siku saba kukagua na kuzindua shughuli za maendeleo katika Mkoa wa Njombe.



Post a Comment