Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Waraka wa elimu wazua mvutano Bara, Visiwani

 

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi,Shukuru Kawambwa
*****
Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Zanzibar zimeingia katika mvutano kuhusiana na waraka wa elimu unaopendekeza baadhi ya masomo ya sekondari kuwa ya hiari badala ya kutumiwa katika kupanga viwango vya madaraja ya ufaulu wa mitihani.

Zanzibar imeukataa waraka huo ambao inadaiwa kuwa uliandaliwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi bila kuishirikisha Wizara yenye dhamana ya Elimu Zanzibar.

Inaelezwa kuwa waraka huo unapendekeza kuwa baadhi ya masomo katika shule za sekondari wanafunzi wayasome kwa hiari bila kuyafanyia mtihani wa taifa na yasitumike katika kupanga viwango vya ufaulu.

Masomo yaliyopendekezwa katika waraka huo kutotumika katika kupanga madaraja ya ufaulu badala yake yawe ya hiari ni ya dini za Kiislamu na Kikristo, Lugha ya Kiarabu, Kifaransa, Kompyuta na Muziki.


Baada ya Zanzibar kukataa mapendekezo ya waraka huo, Serikali ya Zanzibar jana ilitoa taarifa ya Serikali ikisema kuwa masomo ya Dini, Kiarabu na mengine, hayajafutwa na yataendelea kufundishwa na kufanyiwa mitihani katika ngazi zote kama ilivyokuwa awali.

Aidha, imesema Wizara hiyo haijakubaliana na waraka wa elimu kutoka Tanzania Bara wa kuyafanya masomo hayo kuwa ya hiari,  hivyo yasichangie asilimia yoyote katika ufaulu wa mtahiniwa.

Taarifa ya Serikali ya Zanzibar ilitolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Abdallah Mzee, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kufafanua taarifa zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari zilizodai kuwa Wizara hiyo imeondoa mtaala wa masomo hayo kwenye mitihani ya taifa.

Mzee alisema kuwa watendaji kutoka Wizara ya Elimu Tanzania Bara, walikutana na wenzao wa Zanzibar kwa lengo la kujadili waraka wa elimu uliokuwa unataka yafanyike marekebisho katika mfumo wa kupanga viwango vya ufaulu bila kuhusisha masomo hayo.

Mzee alisema katika waraka huo, wajumbe wa Bara walipendekeza masomo ya dini za Kiislamu na Kikristo, Lugha ya Kiarabu, Kifaransa, Kompyuta, Muziki yawe ya hiari, lakini pia yasisaidie ufaulu wowote katika viwango vya madaraja ya ufaulu.

“Waraka ulipendekeza masomo hayo yakiwamo dini na Kiarabu kuwa optional (hiari) na wala yasisaidie chochote katika kupandisha au kushusha division (daraja) la mtahiniwa,” alisema Mzee.

Mzee alifafanua kuwa waraka huo pia ulipendekeza kuwa utaratibu huo mpya uanze kufanyiwa kazi kwa wanafunzi watakaoingia kidato cha kwanza mwakani ili ifikapo mwaka 2017, wanafunzi hao wautumie katika kidato cha nne.

Hata hivyo, alisema watendaji wa Zanzibar waliupinga utaratibu huo kwa vile haukidhi matakwa ya Zanzibar.

“Watendaji wetu waliupinga waraka huo kwani hautufai na unatofautiana sana na sisi kulingana na hoja zetu tulizotoa, lakini pia walikubali kuurudisha ili usifanyiwe kazi, ” alisema.

Alisema kwa Zanzibar, Wizara ya Elimu inatoa mchepuo wa masomo ya lugha katika shule tofauti ikiwamo Sekondari ya Kiponda hivyo itakuwa vigumu kufuata utaratibu huo.

Alisema somo la Dini kwa Zanzibar ni muhimu sana na ni miongoni mwa masomo yenye walimu wazuri wa ngazi za Stashahada ya kwanza hadi ya Uzamivu na kwamba ufundishwaji wake huanzia darasa la kwanza hadi Chuo Kikuu, hivyo isingewezekana kubadili utaratibu.

Alisema katika dunia ya sasa, masomo kama Kompyuta ni muhimu sana na kwamba kutokulipa kipaumbele ni kujirudisha nyuma kimaendeleo.

Alisema licha ya mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Wizara za Elimu za Zanzibar na Bara, lakini Zanzibar hawakushirikishwa katika kuandaa waraka huo. Alipoulizwa kuhusiana na sakata hilo, Ofisa Habari wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ntambi Bunyazu, alisema mawaziri wenye dhamana ya Elimu wa Zanzibar na Bara, Ali Juma Shamhuna na Dk. Shukuru Kawambwa, jana walikuwa na kikao cha kujadili suala hilo.

Kwa mujibu wa Bunyazu, mawaziri hao walikuwa wanakutana mjini Bagamoyo na kikao hicho kilianza saa 10:30 jioni.
 

CHANZO: NIPASHE
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top