Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda akihutubia Mkutano wa hadhara katika kijiji cha
Kagunga Kigoma Vijijini akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya
mkoa wa Kigoma Oktoba 1, 2013. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Baadhi
ya wananchi wa kijiji cha Kagunga wilayani Kigoma vijijini wakifurahia
hotuba ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakati alipohutubia Mkutano wa
hadhara kijijini hapo akiwa katika ziara ya mkoa wa Kigoma Oktoba 1,
2013. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
……………………………………………………………………………….
*Alazimika kusafiri majini kwa zaidi ya saa moja
WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya
Wilaya ya Kigoma Bi. Mariam Mmbaga kuhakikisha kuwa anafuatilia suala la
mkopo kwa ajili ya ujenzi wa soko la Kagunga hadi alikamilishe.
Ametoa
agizo hilo jana jioni (Jumanne, Oktoba mosi, 2013) wakati akizungumza
na mamia ya wakazi wa kata ya Kagunga mara baada ya kuweka jiwe la
msingi la soko la kimataifa la Kagunga ambalo liko umbali wa kilometa
1.5 kutoka mpakani mwa Tanzania na Burundi kwenye mwambao wa Ziwa
Tanganyika.
Waziri
Mkuu alisema kukamilika kwa ujenzi wa soko hilo kutatoa fursa za
kibiashara baina wakazi wa Kagunga na vijiji jirani pamoja na nchi ya
Burundi ambayo milima yake inaonekana kutokea mahali soko lililojengwa.
Mji wa karibu na Kagunga ni Nyanza Lac ulioko kwenye jimbo la Makamba,
nchini Burundi.
“Msingi
wa ujenzi wa soko hili ni makubaliano baina ya Wizara ya Viwanda na
Biashara kwa kushirikiana na Benki ya Rasilmali Tanzania (TIB).
Mkurugenzi simamia hilo zoezi, lifukue kila mahali ulete kwa Waziri
Ghasia ili tukamilishe taratibu za mkopo na soko liweze kukamilika,”
alisema.
Alisema
umuhimu wa soko hilo ni ka pande zote mbili kwani litafungua milango ya
biashara baina ya Tanzania na Burundi. “Kukamilika kwa soko hili pamoja
na barabara ya Kigoma hadi Kagunga kutasaidia sana kuharakisha
upatikanaji wa bidhaa za kuuza nchi jirani ya Burundi,” alisema Waziri
Mkuu.
Waziri
Mkuu ambaye alilazimika kusafiri kwa boti kwa zaidi ya saa moja kutoka
Kigoma mjini hadi Kagunga umbali wa kilometa 49 kwenda tu (sawa na
nautical miles 26.5) alisema anatambua umuhimu wa barabara hiyo na
kuahidi kufuatilia upatikanaji wa fedha ili iweze kukamilika mapema. Kwa
njia ya kawaida, Kagunga iko umbali wa kilometa 130 kutoka Kigoma
mjini na msafiri analazimika kupitia kwanza Burundi ndipo aweze kuingia
Kagunga.
Mapema, akisoma risala kuhusu ujenzi wa soko hilo, Mkurugenzi wa
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Bi. Miriam Mmbaga alisema
mradi huo wa soko uliibuliwa na wananchi mwaka 2008 ili wapate soko la
kuuzia mazao ya kilimo, mifugo, samaki na dagaa. “Mwaka 2008/2009
zilitengwa sh. milioni 365 na ujenzi ulianza mwaka 2009 ambapo fedha
zote zimetumika,” alisema.
Kabla ya kuibuliwa kwa mradi huo, eneo hilo lilikuwa likitumika kama gulio kati wajasiriamali wa Tanzania na Burundi.
Alisema hadi kukamilika kwake, mradi huo utagharimu sh. bilioni 2.6 na kwamba hivi sasa inahitaji
sh. bilioni 2.24 ambapo kati ya hizo sh. bilioni 1,57 zitakuwa ni mkopo
kutoka TIB na sh. milioni 668 zitatolewa kwenye bajeti ya maendeleo ya
Halmashauri kwa kipindi cha miaka mitatu.
“Kwa mwaka 2013/ 2014, Halmashauri imetenga kiasi cha sh. milioni 245.9 kwa ajili ya mradi huu,” alisema Mkurugenzi huyo.
Katika
ziara hiyo ya siku sita mkoani Kigoma, Waziri Mkuu amefuatana na mkewe
Mama Tunu Pinda, Waziri wa Nchi (OWM-TAMISEMI), Bibi Hawa Ghasia, Naibu
Waziri wa Maji, Dk. Binilith Mahenge pamoja na Naibu Waziri Nishati na
Madini, Bw. George Simbachawene.
Post a Comment