Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

WABUNGE "WACHAMBWA"


Wananchi kadhaa wamepinga vikali hatua ya wabunge ya kuitaka serikali inawaongezee maslahi ikiwamo mishahara kwa madai kuwa wanalipwa kiasi kidogo kulinganisha na wa nchi zingine.
Wabunge hao walitoa madai hayo Jumanne wiki hii wakati wa mkutano wao mjini Dodoma.

Erick John, mkazi wa Jiji la Tanga, alisema wabunge wana tamaa na kwamba  ndiyo maana wameshindwa kuondoa kero za wapigakura wao majimboni na kutotekeleza ahadi walizozitoa kwa wananchi kutokana na kujali maslahi yao binafsi.

 “Kuomba maslahi na mishahara zaidi huku utendaji wao ukiwa duni ni hujuma na unyonyaji kwa wananchi, hii inatokana na ukweli kwamba baadhi ya wabunge wametumia gharama kubwa kuingia bungeni na sasa badala ya kufikiri kero za wananchi wanafikiria fedha zitarudije,” alisema John.

Naye Salma Miraji, mkazi wa jijini Tanga alisema:  “Nchi  maskini kama Tanzania wabunge kung’ang’ania posho kubwa ni aibu ….. waangalie mishahara midogo ya walimu, wauguzi, polisi na watu wengine, kwa nini wamekaa kimya wao hawastahili!?” alihoji Salma.

Elizabeth Kilindi alisema wabunge watambue kuwa kazi waliyonayo ni wito na siyo sehemu ya kuchuma na kwamba waendelee na jukumu lao la kuisimamia serikali badala ya kutumia muda wao kufikiria posho na mishahara minono.

 David Pallangyo, alisema  wabunge wanalipwa posho na mishahara mikubwa na kumtaka Spika wa Anne Makinda, kutoangalia upande mmoja wa wabunge bali alenge taifa na walalahoi waliowaweka madarakani.

MHADHIRI RUCO
Mhadhiri Mwandamizi wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Ruaha (Ruco) Rwezaura
Kaijage, alisema ili Watanzania wakubaliane na madai ya wabunge, kila mbunge kwenye jimbo lake tena bila ya kuficha ukweli, aorodhesheni wanafunzi wangapi wanakaa chini kwa kukosa madawati, miradi mingapi ya maji ya boma na visima imekwama na wananchi wake wanahaha kusaka maji kila uchao.

“Ili tuwaongeze mishahara, pia kila mbunge atuambie ni zahanati ngapi jimboni kwake hazina dawa wala watumishi na zimeshindwaje kutoa huduma. Je, ni wananchi wangapi ambao wameshindwa kumudu gharama za ujenzi wa nyumba bora wakati serikali imekuwa ikivutia mazingira ya uwekezaji wa viwanda vya saruji ambavyo hata hivyo, inauza kwa bei ya
kupaa,” alisema.

KAULI YA MACHIFU
Katibu Mtendaji wa Baraza la Machifu Tanzania, Chifu Cuthbert Kiritta kutoka mkoa wa Kilimanjaro, alisema kuwa kamwe baraza hilo haliwezi kuunga mkono madai hayo ya wabunge kwa kuwa hayaendani na uhalisia wa sasa wa maisha ya Watanzania ambao baadhi yao wanapigika kwa kukosa hata mlo mmoja kwa siku.

“Kwanza ni vyema hivi viwango vya mishahara kwa sekta zote za umma na sekta binafsi vikatazamwa upya, lakini kimsingi zipo sekta ambazo hata Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi nchini (Tucta) na hata Chama cha Walimu (CWT) vimekuwa vikilalama juu ya nyongeza ya mishahara na malimbikizo ya stahili za watumishi, lakini serikali ilisema haina,” alisema.

MHADHIRI UDOM

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Paulo Loisulie, alisema Watanzania kwa asilimia kubwa hawawezi kukubaliana na wabunge hao kuongezwa mshahara kwa sababu wana marupurupu mengi ambayo hayakatwi kodi, hivyo siyo sahihi kudai nyongeza.

“Suala hili ni la ubinafsi kwani wanajua fika hali halisi ya Watanzania, hivyo hawapaswi kudai. Wao ndiyo watengeneza sheria zote za nchini, lakini pia wanajua hali ya maisha ni ngumu,” alisema.

Alisema Bunge limeshajadili kuwa kuna fedha zipo Uswisi na fedha za EPA, hivyo ni vyema wakatengeneza sheria zitakazoisimamia serikali kukusanya mapato na sheria ya mapato waisimamie ipasavyo.

WANA MISHAHARA MIKUBWA

Mkazi wa Manispaa ya Dodoma, George Mbara, alisema anapinga wabunge kuongezewa mshahara kwa sababu mishahara wanayolipwa pamoja na posho ni mikubwa kulinganisha na Watanzania wengine.

Alisema haitawezekana kuongezwa mshahara wakati kima cha chini cha mshahara wa mtumishi ni Sh. 150,000 na wapo watumishi wenye utaalamu wanaolipwa mishahara midogo kulinganisha ya wabunge wengi ambao hawana utaalamu wowote.

“Serikali isiwaongezee mshahara kwani wabunge ndio wanaotakiwa kutetea maslahi ya watumishi wa umma kuongezewa mshahara kwa kuwa hawajaongezewa kwa muda mrefu,” alisema Mbara.

TLS WANENA
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS), Francis Stolla, alisema wabunge lazima watambue kuwa kupanda kwa gharama za maisha hakujawaathiri wao tu bali ni kila mwananchi.

Stolla alisema kama serikali itakubali kuwaongeza posho na mishahara wabunge ifanye hivyo kwa watumishi wote wa sekta zote za serikali kwa kuwa hali ngumu ya maisha imewakumba wote.

DK. BANA MISHAHARA HAIJAWAHI KUTOSHA

Naye Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema hakuna mshahara unaoweza kumtosheleza mtu kwani mishahara midogo ni kilio cha watumishi duniani kote.

Alisema wabunge wanapaswa kutambua kuwa kiwango wanachotaka walipweje hakuna uwezo wa kutoa kulingana na hali ya maisha ilivyo sasa vinginevyo itakuwa ni kuwabebesha mzigo wananchi ambao serikali italazimika kuongeza kodi zisizokuwa za lazima ili kufikia kiwango kinachotakiwa.

Dk. Bana alisema inashangaza wakati wananchi wanatambua kuwa wabunge ndiyo wafanyakazi wanaolipwa zaidi kuliko wengine, lakini wanalalamika na kutaka kiwango wanacholipwa kiongozeke.

“Wabunge kama wanaona kiwango wanacholipwa hakiwatoshi waachane na kazi ya ubunge na kuangalia kazi nyingine ambazo wanaona zinalipa kama vile ushauri kwani wengi wao ni wasomi,” alisema.

MKUMBO: WATAFAKARI UWEZO

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki Cha Elimu Cha Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (DUCE), Dk. Kitila Mkumbo, alisema hakuna mshahara unaomtosha mfanyakazi, hivyo wabunge kama wanataka kuongezwa mishahara wanapaswa kutafakari kama mwajiri wao ana uwezo wa kuwalipa kiwango hicho.

BASHIRU WAFANYE UTAFITI KWANZA
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ally, alisema wabunge kabla ya kutaka waongezwe mishahara walipaswa kufanya utafiti wa kiwango wanacholipwa na wafanyakazi wengine.

“Wabunge wanataka waongezwe tu wao, lakini hivi wanatambua kuwa wapo watumishi wa serikali ambao wanalipwa kiwango kidogo sana, walitafakari kwa kina suala hili,” alisema.

TUCTA: NI UBINAFSI, UTOVU WA NIDHAMU

Makamu Mwenyekiti wa Tucta, Nortiburga Maskini, alisema kitendo cha wabunge kutaka waongezwe mishahara na posho ni utovu wa nidhamu kwani kinaonyesha jinsi wanavyojali maslahi yao binafsi kuliko wananchi waliowachagua.

“Huku ni kuwanyonya watanzania na kukosa maadili ya uzalendo wa nchi yao, kwani viongozi wenye maadili ya utaifa hawawezi kujipangilia mishahara yao, inadhihirisha wazi kuwa wana utovu wa maadili ya utumishi kwenye uongozi wa umma,” alisema Maskini.

Alisema hali hiyo inaonyesha kuwa uongozi  Tanzania ni sehemu ya kujishibisha badala ya kutumikia wananchi na taifa.

WANASTAHILI NYONGEZA

Hata hivyo, Joseph Sanga mkazi wa Jacaranda jijini Mbeya, aliwatetea wabunge kwa kusema waongezewe fedha kutokana na kufuatwa na watu wengi wenye shida.
Alisema kuwa mbunge wa Tanzania ndiye anaye pokea mshahara mdogo kuliko wabunge wa Kenya na Uganda.
WANACHOLIPWA WABUNGE

Wakati wabunge hao wakilalamikia maslahi madogo, mbunge mmoja hulipwa mshahara wa Sh. milioni 11 kwa mwezi.

Hiyo ni mbali na posho ya Sh. 330,000 anayolipwa mbunge kwa kuhudhuria kikao kimoja kwa siku. Posho ni Sh. 80,000 za kujikimu akiwa nje ya jimbo lake, posho ya vikao Sh. 200,000 kwa siku na mafuta ya gari Sh. 50,000, jumla kuwa Sh. 330,000 kwa siku.

Aidha, mbunge mmoja hulipwa ‘gratuity’ (kiinua mgongo au bahashishi) ya Sh. milioni 72 baada ya kumaliza kipindi chake cha miaka mitano cha ubunge.

Posho ya Sh. 330,000 anayolipwa mbunge kwa siku inazidi kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa serikali wa Sh. 150,000 kwa mwezi.

Aidha, wabunge hupewa fedha za Mfuko wa Jimbo Sh. milioni 30 kila mwaka kwa ajili ya kusaidia shughuli za maendeleo katika majimbo yao.Serikali hadi sasa imeshindwa kuongeza kima cha chini kufikia Sh. 350,000

Imeandikwa na Augusta Njoji, Dodoma; Godfrey Mushi, Moshi, Thobias Mwanakatwe, Samson Fridolin, Mery Godfrey, Dar; Dege Masoli, Tanga na Furaha Eliab, Mbeya.
CHANZO: NIPASHE
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top