Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba
(pichani) amesema baadhi ya wabunge walitoa lugha za kuudhi dhidi ya tume hiyo
katika Mkutano wa 13 wa Bunge uliomalizika juzi mjini Dodoma.
Akizungumza katika mahojiano maalumu nyumbani
kwake Oysterbay, Dar es Salaam jana, Jaji Wariona aliwataka kutoingilia
majukumu ya tume hiyo.
“Wabunge wasijiingize vinywani mwetu na katika
akili zetu. Wapo waliosema kuwa sisi (Tume) siyo wataalamu pekee wa
masuala ya Katiba…
Katika maandalizi yetu hatukufikiria wala
hatukutaka kuwa wabunge. Tuliona kazi yetu ni kutoa ufafanuzi na uamuzi
utakuwa wa Bunge, tulitegemea kuwa tutatoa ufafanuzi katika Kamati za
Bunge, siyo Bunge la Katiba.”
Katika mkutano huo, wabunge walipitisha Muswada wa
Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013, baada ya
kufanyiwa marekebisho kwa baadhi ya vifungu vilivyokuwa vikilalamikiwa,
kikiwemo cha wajumbe wa tume hiyo kutoingia kwenye vikao vya Bunge la
Katiba.
Katika mjadala wa muswada huo, baadhi ya wabunge
walisema kuwa hakuna ulazima wa tume hiyo kuwepo katika Bunge hilo, huku
baadhi yao wakieleza kuwa wajumbe wa tume hiyo siyo wataalamu pekee wa
masuala ya Katiba.
“Wasije wakasema tume ina lake jambo katika Sheria
ya Marekebisho ya Katiba. Wabunge ndiyo walitengeneza sheria hiyo, pia
wanajua sababu za awali kutupa jukumu kwenye Bunge la Katiba na Kura ya
Maoni na baadaye kutuondoa.”
Jaji Warioba alisema hivi karibuni wanasiasa
wamediriki kusema wazi kuwa baadhi ya wajumbe wa tume hiyo hawana uwezo
na wanalipwa fedha za bure.
“Kila mjumbe ana umuhimu wake, kauli
ninazozungumza ndiyo msimamo wa Tume, ndani ya tume hii kila mtu ana
umuhimu wake,” alisema.
Akizungumzia Bunge la Katiba, Jaji Wariona alisema
ili kufanikisha kazi hiyo ya kihistoria kwa Taifa, wabunge wote hawana
budi kuwa kitu kimoja na kuweka mbele masilahi ya taifa.
Amkumbuka Dk Mvungi
Akizungumzia hali ya Mjumbe wa Tume hiyo, Dk
Sengondo Mvungi ambaye yuko Afrika Kusini kwa matibabu baada ya
kujeruhiwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake wiki moja iliyopita,
Jaji Warioba alisema wameelezwa kwamba anaendelea vizuri.
MWANANCHI
MWANANCHI


Post a Comment