PICHA NA MAKTABA |
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
TAARIFA KWA UMMA
MATUKIO YA UJANGILI WA CHUI NA TEMBO
Jumamosi,
tarehe 19 Januari 2014, majira ya saa 12:45 jioni katika eneo la Yombo
Vituka, Jijini Dar Es Salaam, askari wa wanyamapori wa Kikosi Dhidi ya
Ujangili (KDU) Kanda ya Mashariki walifanikiwa kumtia mbaroni mtuhumiwa
wa ujangili kwa jina Mwajuma Hamis. Mwajuma alikutwa akiwa na nyara za
Serikali ambazo ni ngozi mbili za chui ndani ya nyumba anamoishi kinyume
cha Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009. Mtuhumiwa huyo
amekabidhiwa kwa Polisi kwa hatua zaidi za kisheria na amefunguliwa
jalada na. CHA/RB/564/2014.
Pia,
siku ya Ijumaa, tarehe 17 Januari 2014, jioni kwenye uwanja wa ndege wa
kimataifa wa Julius Nyerere, askari wa KDU kanda ya Mashariki
walimkamata raia wa China aliyefahamika kwa jina la LING TIAN mwenye
hati ya Kusafiria na. G28214172. Bwana Tian alikutwa akiwa na bangili 2
na mkufu 1 wenye golori 11 zilizotengenezwa kutoka meno ya tembo.
Mtuhumiwa amefikishwa Polisi na kufunguliwa jalada na. JNIA/IR/16/2013
kwa hatua zaidi za kisheria. Mtuhumiwa huyo, ambaye kwa sasa yuko
rumande, alikuwa anatokea Msumbiji kwenda China.
Serikali
haitalala hadi majangili wote wanapatikana na kufikishwa katika vyombo
vya sheria. Ilani inatolewa kuwa Tanzania si kichaka cha kupitishia meno
ya tembo au magendo ya aina yoyote. Wizara inawahakikishia wananchi
kuwa imejizatiti vilivyo kupambana na vitendo vya ujangili katika mapori
yote, maeneo yote ya mipaka ya nchi yetu na kwenye viwanja vyote vya
ndege pamoja na bandari zote.
Wizara
inatoa pongezi kwa raia wote ambao wanaisaidia kuwabaini waalifu.
Tunatambua kuwa wengi wa wahalifu ni raia walio miongoni mwetu.
Tunawaomba wananchi waendelee kutoa kwa Wizara habari zinazohusu
ujangili ili tuendelee kuwabana na hatimaye kuusambaratisha mtandao wa
ujangili ili tusalimishe maliasili zetu na kuokoa uchumi wa nchi.
Imetolewa na:
Chikambi K. Rumisha
Msemaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii
Post a Comment