Mfuko wa
Taifa wa Bima ya afya (NHIF) mkoa wa Iringa umekusanya Sh236.8m ikiwa ni
michango ya wanachama kutoka kwa waajiri wao katika kipindi cha mwaka
2013/2014.
Akizungumza
na mwandishi wa gazeti hili, Meneja wa NHIF mkoa wa Iringa, Emmanuel
Mwikabe amesema kuwa kiasi cha Sh milioni sita hakijakusanywa kutoka kwa
waajiri kutokana na kutowasilisha kwa wakati na wengine kuwa na
malimbikizo ya michango.
Akichanganua
Mwikabe amesema Hospitali teule ya Tosamaganga inadaiwa malimbikizo ya
sh490, 298, Halmashauri ya wilaya ya Iringa Sh3.2milioni na Halmashauri
ya wilaya ya Mufindi Sh2.4milioni.
Aidha
amesema moja ya changamoto waliyoibaini baada ya kufanya ukaguzi ni
vituo na hospitali kutokuwa na uwazi wa mapato yatokanayo na bima ya
afya na fomu za bima ya afya hasa kwenye vituo vya serikali hazijazwi
vizuri.
Changamoto
nyingine ni baadhi ya watumishi katika vituo vinavyotoa huduma
kujihusisha na vitendo vya kughushi ambapo madai ya Sh6.7 milioni
hayakulipwa kutokana na sababu hiyo.
Amezitaja
sehemu ambazo hazikulipwa kutokana na kughushi kuwa ni pamoja na
Hospitali ya wilaya ya Mufindi Sh 1.8milioni, Zahanati ya polisi ya
Iringa Sh1.4milioni, Zahanati ya Magereza ya Iringa Sh1.2 milioni na
Kituo cha afya cha Mkwawa Sh 2.2milioni.
Amesema pia
katika kipindi cha miezi sita wanachama 50,778 walihudhuria kwenye vituo
vya matibabu ambapo gharama zilizowasilishwa kwa ajili ya malipo ni
Sh651milioni.
Amesema
Sh80.1 milioni zililipwa kwa madhehebu ya dini, Sh124.6 milioni
zililipwa kwenye vituo binafsi, na Sh378.4 milioni zililipwa kwenye
vituo vya serikali na kuwa Sh68.3 milioni hazikulipwa kutokana na
kutofuata taratibu na misingi ya tiba, bei elekezi ya bima ya afya na
kutojaza taarifa muhimu katika fomu ya madai. Chanzo: Hakimu Mwafongo


Post a Comment