**********
Suala la baadhi ya viongozi nchini kuanza kampeni za kuwania
urais mwaka 2015 kwa kumwaga fedha ili kujijengea mazingira ya ushindi,
limechukua sura mpya baada ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa
Umma kuanza kuwabana.
Habari zilizolifikia gazeti hili na baadaye
kuthibitishwa na Kamishna wa Sekretarieti hiyo, Jaji Mstaafu Salome
Kaganda, zinaeleza kuwa chombo hicho cha Serikali tayari kimewaita watu
hao na kuwapa onyo baadhi yao wakiwamo mawaziri na wabunge walioanza
kufanya kampeni.
Jaji Kaganda alisema kuwa waliwaita baadhi ya
wanasiasa hao ambao wengi wana hadhi ya ubunge na kuwaonya kutokana na
kubainika kwamba wanakiuka kanuni za maadili.
“Kwa upande wetu tumeshawaita baadhi, tulizungumza
nao na kuwaonya kuhusu nyendo zao. Wapo waliotuelewa, naona wamekuwa
kimya wakiendelea na shughuli zao nyingine za ujenzi wa taifa kwa
nyadhifa walizonazo, ingawa pia wapo wengine tunasikia wanaendelea,”
alisema Jaji Kaganda.
Tayari Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimepanga
kuwachukulia hatua baadhi ya makada wake wanaodaiwa kuanza kufanya
kampeni kabla ya wakati.
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangula wiki hii
alikaririwa akiwa mjini Morogoro akisema kwamba tayari wamefungua
mafaili ya watu wenye mitandao ya kampeni akisema wanaitambua mitandao
hiyo hadi ngazi za mikoa na wataishughulikia.
Alisema kuwa muda wa kampeni za urais, udiwani, ubunge haujafika, hivyo wanaofanya kampeni sasa wanakiuka Katiba na Kanuni.
Kwa upande wake, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji
Francis Mutungi, alipoulizwa kuhusu hatua zinazochukuliwa dhidi ya
wanaodaiwa kujipitisha kabla ya muda wa kampeni za Uchaguzi Mkuu,
alisema ofisi yake ipo tayari kuwashughulikia kwa mujibu wa utaratibu,
ikiwamo kuwashtaki kwenye Sekretarieti ya Maadili, iwapo barua za
malalamiko zitafikishwa kwake.
“Kwa jambo hili hatuwezi kuchukua hatua yoyote
kama hakuna barua ya malalamiko iliyoletwa kwetu, hasa na vyama husika.
Hivi sasa na sisi tumebaki tunaona na kusikia tu kwenye vyombo vya
habari,” alisema Jaji Mutungi.
Wiki iliyopita wabunge wa Kamati ya Bunge ya
Katiba na Sheria walipokuwa kwenye ziara kwenye Ofisi ya Sekretarieti ya
Maadili, walihoji jinsi chombo hicho cha umma kilivyojipanga
kuwashughulikia viongozi wanaodaiwa kumwaga fedha wakiwa katika
maandalizi ya kugombea urais na ubunge.
Wabunge
Mjumbe wa Kamati hiyo, Nyambari Nyangwine ambaye
pia ni Mbunge wa Tarime, alitaka kujua jinsi Sekretarieti hiyo,
inavyoweza kuwashughulikia viongozi hao kwa kuwa vitendo hivyo vinakiuka
maadili ya uongozi.
“Sekretarieti itawashughulikia vipi watu hawa ambao katika
kuelekea Uchaguzi Mkuu, wameanza kampeni, wanamwaga fedha ili wapate
uongozi?” Alihoji mbunge huyo.
Akijibu swali hilo, Katibu wa Utumishi wa
Sekretarieti hiyo, Tixon Nzunda, alisema jukumu lao ni kushughulikia
watu ambao tayari wana hadhi ya uongozi na kwamba zipo pia taasisi
nyingine za Serikali zinazoweza kulifanyia kazi suala hilo.
“Ila pia kuna taasisi ambazo zinapaswa kuchukua
hatua dhidi ya jambo hilo, kama vile Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru) na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa,” alisema.
Aliongeza: “Sisi kwa upande wetu tumekuwa
tukishirikiana na vyama hivyo, kwa kuwasisitizia viongozi wao
kuhakikisha wanateua wagombea walio na sifa za maadili ili kulinda
heshima na maana ya uongozi.”
Kuhusu Sheria ya Kutenganisha Uongozi na Biashara,
ambayo baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo waliomba itazamwe upya, alisema
mtu anayetaka kuwa kiongozi, anatakiwa kuepuka mambo yanayoweza
kusababisha mgongano wa kimasilahi.
“Unapokuwa kiongozi lazima uyatambue mazingira
yanayoweza kukusababishia mgongano wa kimasilahi, hivyo hatua hiyo ya
kuzuia viongozi kuwa wafanyabiashara, siyo kwa sababu ya Azimio la
Arusha, bali inalinda pia maadili ya kiongozi,” alisema Nzunda na
kuongeza;
“Hata hivyo, kuna mambo ambayo kiongozi
mfanyabishara anatakiwa kuchagua moja kati ya matatu ambayo ni kuuza
hisa zake katika kipindi cha siku 90 tangu kuchaguliwa, au aipeleke
kwenye taasisi atakayoiamini na ajiondoe kusimamia au asikubali kuwa
kiongozi.”
Akitoa ufafanuzi juu ya hilo, Jaji Kaganda
alisema, viongozi hawakatazwi kuwa matajiri, isipokuwa wanapaswa
kujipatia mali kwa njia halali, kwa kuwa wakiwa na uwezo wa kipato, pia
husaidia kutatua matatizo madogo ya watu wanaowaongoza.
“Naomba muelewe vyema, haikatazwi kiongozi kuwa
tajiri, kwa sababu napo kiongozi akiwa maskini hataweza kuwasaidia
wananchi kutatua matatizo yanayogharimu, hata kwa Sh10,000,” alisema.
MWANANCHI
Post a Comment