Dar es Salaam/Arusha. Siku moja baada ya Rais
Jakaya Kikwete kufanya uteuzi wa majina ya Wajumbe 201 wa Bunge Maalumu
la Katiba, wasomi, wanasiasa na wanaharakati wameuponda wakisema
umependelea wanasiasa, badala ya wananchi walio nje ya mfumo huo.
Pia wamo Mwenyekiti wa Chama cha Democratic Party
(DP), Mchungaji Christopher Mtikila na John Chipaka ambaye ni Mwenyekiti
wa Chama cha Tadea.
Wakizungumza na Mwananchi Jumapili jana walisema
kuwa licha ya kuteuliwa kwao, wajumbe hao wanatakiwa kuweka mbele
maslahi ya taifa na kusahau vyama na makundi kwa kuyaweka kando.
Dk Hellen Kijo-Bisimba
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema: “Tunashangaa kuona
watu walioteuliwa wengi ni wanasiasa. Tulitarajia wengetoka nje ya vyama
vya siasa, lakini ndiyo Rais kaamua.”
Dk Bisimba alisema kuwa marehemu Dk Sengondo
Mvungi aliwahi kusema kwamba, Bunge la Katiba ndiyo Katiba yenyewe,
hivyo wajumbe wake wasipowawakilisha vyema wananchi taifa halitapata
Katiba yenye sura ya Kitaifa.
“Wanatakiwa kujua wanakwenda kufanya nini. Rasimu
iliyopo inahitaji marekebisho madogo sana, kama watafanya hivyo tutapata
Katiba nzuri, lakini kama wataingiza mambo yao ya siasa wataiharibu
kabisa,” alisema Dk Bisimba.
Naye Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la
Haki Ardhi, Yefus Myenzi alisema kuwa baadhi ya walioteuliwa wamekuwa
katika mfumo wa Serikali kwa kipindi kirefu.
“Kingunge Ngombale Mwiru na Paul Kimiti
wamehudumia kwa muda mrefu serikalini, lakini leo wamejipenyeza kupitia
makundi mengine, imekuwa tofauti,” alisema Myenzi
Aliongeza: “Tunaandaa Katiba inayotakiwa kuweka
maslahi ya taifa mbele, lakini kwa hali hii inatia shaka, kwani
wanasiasa wamekuwa wengie sana.”
Myenzi alisema kinachotakiwa sasa ni kutoa elimu
kwa Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba watakaoijadili Rasimu ya Katiba
ili kuhakikisha mambo yanahusu utaifa wanayaweke mbele na kuweka kando
yale yanayohusu makundi yao aliyosema hayatakuwa na tija kwa taifa.
Ali Mafuruki
Mwenyekiti wa Jukwaa la Maofisa Watendaji Wakuu wa Kampuni
Binafsi Tanzania, Ali Mafuruki aliwataka wajumbe walioteuliwa kutambua
kuwa jukumu la Watanzania wote kuhusu Katiba lipo mikononi mwao, hivyo
wakatae kutumika kwa maslahi binafsi ya baadhi ya watu.
“Wasikubali kutumika na watu bali watambue ya kuwa
hatima ya Watanzania iko mikononi mwao, wala haiko kwa Rais au chama
kinachotawala. Waache kwenda huko kufanya mambo kulingana na makundi
yao,” Mafuruki alionya.
Aliongeza: “Hii siyo kazi ya mtu mmoja,
washirikiane na kama hawatashirikiana kwa pamoja hatutapata Katiba Mpya
inayoweka maslahi ya taifa mbele.”
Profesa Samuel Wangwe
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa
Kuondoa Umaskini (Repoa), Profesa Samuel Wangwe kwa upande wake alisema
uteuzi wa Rais Kikwete ni uteuzi mzuri, lakini utategemea utendaji kazi
wao.
“Watanzania wanawategemea kwenda kuwawakilisha
vyema, lakini kama hawatafanya hivyo, watakuwa wamewatenga na hatutapata
Katiba inayosubiriwa na watu wengi,” alisema Profesa Wangwe.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi isiyo ya Serikali ya
Sikika, Irenei Kiria alisema kuwa kundi lililoitwa lenye Malengo
Yanayofanana wamejaa wanasiasa, akieleza kundi hilo lingeweza
kuunganishwa na Kundi la Vyama vya Siasa.
“Mapendekezo yaliyopelekwa kwa Rais
hayakuzingatiwa kama yalivyopendekezwa, kuna baadhi wameteuliwa kwenda
kulala bungeni, wengine kwa misingi ya itikadi za kisiasa,” alisema
Kiria.
Alisema kwamba kuna mambo mengi ya kujadili katika
Rasimu ya Katiba Mpya akiyataja baadhi kuwa ni haki ya kupata afya
aliyosema haimo kwenye rasimu hiyo akiwataka wajumbe waache kwenda
Dodoma kwa Bunge la Katiba wakiwa na fikra za kujadili Muundo wa
Muungano pekee, bali wajali na afya za Watanzania walio wengi aliosema
wanaokufa kwa kukosa huduma stahiki.
Chama cha Viziwi
Mkurugenzi wa Chama cha Viziwi Tanzania (Chavita),
Dickson Mveyange alisema kitendo alichokifanya Rais Kikwete kushindwa
kumteua mwakilishi wao kimewasononesha.
lisema nchi nzima kuna wanachama zaidi ya milioni
mbili wa chama hicho, lakini kundi hilo halitakuwa na mwakilishi katika
Bunge hilo linalotarajiwa kuanza Februari 18 mwaka huu.
“Rais ameteua wawakilishi wengi wenye ulemavu wa viungo,
wasioona na kutusahau kabisa sisi viziwi. Sasa hatujui nani atakwenda
kututetea bungeni ili Katiba ijayo itutambue na sisi,” alisema Mveyange.
Onesmo ole Ngulumwa
Mratibu wa Shirika la Watetezi wa Haki za Binadamu
(THRDS), Onesmo ole Ngulumwa alisema ingawa bado wanatafakari uteuzi
uliofanywa na Rais Kikwete, lakini wamesikitishwa kwa kutoteuliwa
watetezi wa haki za binadamu.
“Kuna Mashirika ya Haki za Binadamu yalipeleka
majina, lakini tunasikitika katika orodha hii hakuna wajumbe,
tumeshangaa sana, lakini binafsi nilitegemea hii,”alisema Ole Ngulumwa.
Alisema kinachoonekana wengi walioteuliwa ni wanasiasa kutoka chama kimoja, hivyo kutishia upatikanaji wa Katiba bora.
Naye Joram Madula alisema, wamesikitishwa
kutoteuliwa mjumbe kutoka jamii yao ya Wahadzabe kwani walikuwa na maoni
yao ambayo wangeweza kuyatetea kwenye Katiba Mpya.
“Tulipeleka majina kupitia taasisi ya Pingos
forums, lakini hatujateuliwa , ila tunaomba wajumbe wengine kutusemea
hoja zetu hasa juu ya umiliki wa ardhi, kulindwa tamaduni zetu na
mengine,”alisema Madula.
Habari hii imeandaliwa na Ibrahim Yamola, Dar na Mussa Juma, Arusha.
MWANANCHI
MWANANCHI
Post a Comment