TANGU kuanza kwa Bunge Maalumu la Katiba (BMK), nimekuwa mkimya
kuliko nilivyozoeleka katika maisha yangu ya kisiasa. Watu wengi
wamekuwa wakiniuliza maswali kuhusu nini msimamo wangu katika masuala
anuai yanayojadiliwa ndani ya Bunge.
Hata hivyo, kuliko jambo lingine lolote, ukimya wangu ulitokana na uzito wenyewe wa jambo ambalo BMK
unatakiwa kulifanya. Inapaswa kufanya utafiti mkubwa kabla ya
kuzungumza maana haya tunayoyafanya sasa yatakuja kusomwa katika vitabu
vya historia miaka mingi baada ya sisi sote kuondoka katika ulimwengu
huu.
Bila shaka,
uamuzi mkubwa zaidi ambao BMK linatarajiwa kuufanya ni kuhusu aina ipi
ya ushirika au mahusiano ambao nchi yetu sasa itaamua kuufuata kupitia
Katiba Mpya tunayotaka kuipitia.
Ni kuhusu idadi ya serikali tutakazokuwa nazo na uhusiano
utakaokuwepo. Serikali mbili au tatu. Tume ya Jaji Joseph Warioba
ilipendekeza muundo wa serikali tatu lakini inaonekana Rais Jakaya
Kikwete na serikali yake ya CCM wanapendelea kuendelea na mfumo wa sasa
wa serikali mbili.
Jambo moja ambalo nimejifunza wakati nikifanya utafiti na kufuatilia
mijadala mbalimbali inayoendelea kuhusu suala hili ni kwamba Watanzania
wengi wanapenda Muungano wetu uendelee.
Niseme mapema kwamba Watanzania hatupaswi kuiga isipokuwa kujifunza
kwa nchi nyingine. Hivyo muundo gani unafaa ni uamuzi wetu wenyewe. Hata
hivyo uamuzi huo ni lazima ujibu vigezo fulani fulani.
Vigezo vikubwa ni viwili; Je, Muundo tunaoutaka utajibu kero
(malalamiko) za Muungano wa sasa? Je, Muundo tunaoutaka utajibu hofu za
Muungano kuvunjika. Muundo utakaojibu hofu hizo ndio utakaotufaa. Suala
la serikali ngapi zinatakiwa ni suala linalokuja baadaye baada ya kujibu
hoja hizo za msingi.
Kwa sasa, bado kuna utata iwapo Tanzania ni Shirikisho (Federation)
au ni Muungano (Union). Katika vikao vya Kamati za BMK vinavyoendelea
sasa, jambo hili limezua mjadala mkubwa ambapo baadhi ya wajumbe
wanapendekeza kuwa neno Shirikisho litoke kwenye Sura ya Kwanza ya
Rasimu ya Katiba na wengine wakipendekeza libakie au hata kuweka wazi
kabisa kuwa Tanzania ni Jamhuri ya Shirikisho la Tanganyika na Zanzibar.
Ni vema, kama mtu mwenye mapenzi mema na Taifa lake, nikatumia fursa
hii kuzieleza dhana hizi za muundo ili zieleweke vizuri na watumiaji
waweze kuzitumia kwa usahihi. Kwa ufupi tutazame maana ya kila dhana na
mifano mbalimbali duniani. Tutatazama dhana tatu kuu - Muungano (Union),
Shirikisho (Federation) na Jumuiya (Confederation/Community).
Muungano
Katika mfumo huu, Nchi kuungana kuunda Taifa moja, Dola moja ndani ya
Nchi moja. Serikali za Washirika huachia sehemu kubwa ya madaraka yao
kwa Serikali ya Muungano. Mara nyingi muundo huu hupelekea kuwapo kwa
Serikali moja yenye nguvu (ya Muungano) na kama Washirika wanabakia na
serikali zao, basi hubakia na mambo machache sana. Faida ya Muundo huu
iko kwenye uimara wake na si rahisi kuvunjika.
Hasara za muundo huu ni athari ya moja ya nchi, hasa kama ni ndogo,
kumezwa na Mshirika mkubwa. Hapa Afrika, Nchi ya Afrika ya Kusini
inafuata muundo huu wa Muugano ambapo Serikali ya Muungano ina nguvu na
mamlaka mengi kuliko zile za Majimbo yanayounda Jamhuri ya Afrika ya
Kusini. Huko Asia mfano mzuri ni India ambapo japo muundo wake unatoa
nguvu kubwa kwa Majimbo kujitawala, Serikali ya Muungano (Union
Government) ina nguvu kubwa zinazoondoa sifa ya kuitwa Shirikisho.
Si lazima 'Union' kuwa na Serikali moja (Unitary State) isipokuwa
mazingira ya nchi husika ndio yanaweza kuamua. Mfano mzuri hapa ni ule
wa Afrika ya Kusini ambayo ni 'unitary state' yenye Serikali 10, tisa za
Majimbo na Moja ya Muungano.
Shirikisho
Katika muundo huu, serikali za washirika hukasimu sehemu ndogo ya
madaraka yake kwa Serikali ya Muungano. Mambo ya kidola (sovereign
functions) hufanywa na Serikali ya Shirikisho na Serikali za Washirika
kubakia na mambo yake yenyewe.
Faida kubwa ya muundo huu ni kuondoa hofu ya mkubwa kummeza mdogo na
ule uhuru wa kujiamulia mambo mengi. Hasara ya muundo huu ni kujengwa
kwa utaifa au hisia za utaifa za Washirika ambazo hatimaye hupelekea
Shirikisho kuvunjika. Hapa Afrika mfano mzuri wa Shirikisho ni nchi ya
Ethiopia ambapo Majimbo yake yanao uwezo hata wa kujitoa katika
Shirikisho kikatiba.
Eritrea ilitumia fursa hii na kujitoa kuwa sehemu ya Ethiopia mara
baada ya mapinduzi yaliyomtoa Mengistu Haile Mariam. Ujerumani pia ni
Shirikisho.
Jumuiya
Katika muundo huu kila Mshirika anakuwa na uhuru wa mambo yake yote
isipokuwa tu kunakuwa na mambo ya uratibu wa pamoja. Aina hii ya Muundo
ndio unapaswa kwa kinachoitwa Muungano wa Mkataba.
Faida kubwa ya muundo huu ni kwamba hakuna kubanana na pale
kunapotokea hofu Mshirika hujitoa. Mfano mzuri ni Uswisi na Jumuiya ya
Ulaya. Hata Jumuiya ya Afrika Mashariki pia inaitwa ni Muungano wa
Mkataba.
Muundo gani Tanzania?
Tanzania kuwa Shirikisho au Muungano ni mjadala ambao utaendelea
kuwapo licha ya kuamua kuchagua muundo mmoja wapo. Wakati wa kuandika
Katiba ya India mwaka 1947 ubishani huu ulikuwa mkubwa sana pia.
Katiba ya India imegawanya mamlaka katika sehemu tatu - Mambo ya
Muungano, Mambo ya Washirika na Mambo ya Pamoja (concurrent). Wajumbe wa
Bunge la Katiba la India wanaotaka Shirikisho walipinga muundo huo na
kukataa 'Washirika kuwa ombaomba kwa Serikali ya Muungano'.
Hata hivyo ubishi huo ulimalizwa na Mwanasheria mahiri wa India, BM
Ambedkar, kwa kusema 'tunataka Serikali imara ya Muungano na yenye nguvu
iwezekanvyo' na alifunga mjadala kwa kusema 'Muungano wa Washirika
unatakiwa zaidi kuliko Shirikisho la Washirika'.
Tanzania inaweza kuwa na Muundo wa Muungano wenye Serikali tatu ama
Muundo wa Shirikisho wenye Serikali mbili, ama kinyume chake.
Idadi ya
Serikali haina uhusiano wowote na ama tunaitwa Shirikisho au Muungano.
Mifano miwili hapo juu ituongoze, India ni Muungano unaitwa Shirikisho
na Afrika Kusini ni Shirikisho linaloitwa Muungano.
Muungano wa Serikali 3 na sio Shirikisho la Serikali 3 ndio
mapendekezo yangu. Muungano (Union) wa Washirika ni bora, imara na
endelevu zaidi kwa mazingira ya Afrika kuliko Shirikisho (Federation) la
Washirika.
Mapendekezo yangu mahususi yaliyowasilishwa kwenye kamati namba 12 ya BMK ni kama ilivyo hapa chini.
SURA YA KWANZA
SEHEMU YA KWANZA
1(1) Irekebishwe na kuandikwa upya na isomeke
Tanzania ni Nchi Moja na ni Jamhuri ya Muungano yenye mamlaka kamili
ambayo imetokana na Muungano wa Nchi za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri
ya Watu wa Zanzibar ambazo kabla ya Hati ya Makubaliano ya Muungano ya
Mwaka 1964, zilikuwa nchi huru.
1(2) neno Shirikisho lifutwe na kuongeza maneno ....Nchi ya.... baada
ya neno 'ni' na kabla ya neno 'kidemokrasia'
Ongeza ibara ya mpya ya 3 itakayosomeka
3(1) Shughuli zote za Mamlaka ya Nchi katika Jamhuri ya Muungano
zitatekelezwa na kudhibitiwa na vyombo vitatu vyenye mamlaka ya
Utendaji, vyombo vitatu vyenye mamlaka ya kutekeleza utoaji haki, na
pia vyombo vitatu vyenye madaraka ya kutunga sheria na kusimamia
utekelezaji wa shughuli za umma
3(2) Vyombo vyenye Mamlaka ya Utendaji vitakuwa ni Serikali ya
Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Tanganyika;
vyombo vyenye Mamlaka ya kutekeleza utoaji haki vitakuwa ni mahakama ya
Juu ya Jamhuri ya Muungano, Mahakama ya Tanganyika na Mahakama ya
Zanzibar na vyombo vyenye Mamlaka ya ya kutunga sheria na kusimamia
utekelezaji wa shughuli za umma vitakuwa ni Bunge la Jamhuri ya
Muungano, Baraza la Wawakilishi la Tanganyika na Baraza la Wawakilishi
la Zanzibar.
3(3) Kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za umma katika Jamhuri
ya Muungano, na kwa ajili ya mgawanyo wa madaraka juu ya shughuli
hizo baina ya vyombo vilivyotajwa katika ibara hii, kutakuwa na mambo ya
Muungano kama yalivyoorodheshwa katika Nyongeza ya Kwanza ya Katibahii,
kutakuwa na mambo ya uratibu wa pamoja na kutakuwa na mambo yasiyo ya
Muungano ambayo ni mambo mengine yote yasiyo mambo ya Muungano na yasiyo
ya uratibu wa pamoja.
3(4) Kila chombo kilichotajwa katika ibara hii kitaundwa na kutekeleza
majukumu yake na Katiba za Serikali za Washirika na kwa kufuata
masharti ya katiba hii.
3(5) Kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za Serikali ya Jamhuri
ya Muungano au Serikali ya Tanganyika au Serikali ya Zanzibar Bunge
laweza kuigawa Jamhuri ya Muungano katika Mikoa kwa mujibu wa Sheria
iliyotungwa na Bunge; Isipokuwa kwamba Bunge litapata kwanza Azimio la
Baraza la Wawakilishi la Tanganyika kwa mikoa ya Tanganyika au Baraza la
Wawakilishi Zanzibar kwa mikoa ya Zanzibar.
SABABU ZA MAREKEBISHO YANAYOPENDEKEZWA.
Rasimu ya Katiba imetangaza tu kuwa 'Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
(JMT) ni Nchi' na kuacha 'ambiguity' ya kwamba Tanzania ni nchi ngapi.
Katiba ya sasa imetamka bayana kuwa 'Tanzania ni Nchi Moja'.
Rasimu pia imetamka kwamba JMT inatokana na 'muungano wa nchi mbili'.
Hivyo basi ni vema kuweka wazi kabisa kuwa Nchi hizi mbili zimeunda
nchi moja. Hii itaepusha migongano ya siku za usoni kuhusu tafsiri ya
Katiba na Mamlaka za Nchi. Ifahamike wazi kuwa idadi ya Serikali haina
uhusiano na uundaji wa nchi moja.
Rasimu imetangaza kuwa Tanzania ni Shirikisho ingawa bado imetamka
'Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (United Republic of Tanzania). Dhana za
'Union' na 'Federation' ni dhana mbili tofauti katika miungano.
Idadi ya Serikali haina mahusiano ya moja kwa moja na aina ya
Muungano kama ni 'Union' au ni 'Shirikisho'. Kwa mazingira ya Nchi za
Kiafrika ni salama zaidi kuwa na 'Union' kuliko Shirikisho.
Rasimu imeweka sura ya Kwanza bila kutaja vyombo vya Jamhuri ya
Muungano. Ni vema ili kuondoa 'ambiguity' vyombo vya Jamhuri ya
Muungano kutajwa kinagaubaga katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano
katika sura ya 'uundwaji wa nchi'. Mapendekezo ya ibara mpya za
sehemu ya kwanza ya sura ya kwanza yanazingatia tahadhari hiyo. Katika
kutaja vyombo mapendekezo haya yanaonyesha dhahiri kuwa ugawaji wa Nchi
katika Mikoa inakuwa ni mamlaka ya Bunge.
Serikali za Washirika zaweza kuwa na mamlaka ya Serikali za Mitaa.
Mikoa inapaswa kuwa mamlaka ya Bunge la Muungano kwa sababu yaweza pia
kutumika katika kupata Wabunge wa Muungano lakini pia itasaidia kuondoa
tabia ya kugawa mikoa hovyohovyo.
Kimsingi ilipaswa Mikoa yote ya Nchi itajwe ndani ya Katiba
kuongezeka au kupunguka kwake kutokane na maamuzi maalumu ya Bunge hata
ikibidi iwe kwa theluthi mbili.
SURA YA SITA
Ibara ya 60(1) maneno shirikisho yafutwe na kubaki uwepo wa Serikali 3.
60(3) isomeke
Muundo, madaraka na mambo mengine ya kiutendaji yahusuyo Serikali ya
Tanganyika, na Serikali ya Zanzibar yataainishwa katika Katiba za
Washirika na kwa kuzingatia masharti ya Katiba hii.
Ibara ya 63 iitwe 63(1)
Iongezwe 63(2)
Kwa ajili ya uratibu bora wa shughuli za Mamlaka za Nchi na kwa ajili
ya kuhakikisha ufanisi na weledi katika uendeshaji bora wa Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mgawanyo wa madaraka, Serikali ya
Jamhuri ya Muungano itakuwa na mamlaka ya uratibu juu ya mambo ya
uratibu kama yalivyoorodheshwa katka nyongeza ya pili ya Katiba hii.
64(1) maneno nchi washirika yaondoke na kubakia neno Washirika au
Washirika wa Muungano.
64(5) isomeke
Serikali za Washirika zitakuwa na hadhi na haki sawa ndani ya Jamhuri
ya Muungano na zitatekeleza majukumu yao kwa mambo yote yasiyo ya Muungano katika mamlaka za Serikali za Washirika kwa mujibu wa
masharti yatakayowekwa na Katiba za Serikali za Washirika kwa
kuzingatia masharti ya Katiba hii.
65 maeneo yote yenye maneno Nchi Washirika yafutwe na kuandikwa
Washirika wa Muungano
67 ifutwe yote
69 maneno Nchi yafutwe ....katiba za Washirika.......
69 (2) maneno Viongozi wakuu yafutwe na kuandikwa ' Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania na Wakuu wa Serikali za Washirika watakuwa ni
Viongozi Wakuu wa Nchi'
69(3) isomeke
Viongozi wanaohusika na masharti ya ibara hii ni
(a) Rais wa Jamhuri ya Muungano
(b) Mkuu wa Serikali ya Tanganyika ambaye pia atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
(c) Mkuu wa Serikali ya Zanzibar ambaye pia atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Ongeza ibara ya 70
(1) Mkuu wa Nchi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ataitwa
Rais atapatikana kwa kuchaguliwa kwa kura na wananchi wote wa Jamhuri ya
Muungano kwa Mujibu wa masharti ya Katiba hii. Rais atakuwa pia Mkuu wa
Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
(2) Wakuu wa Serikali za Washirika watapatikana kutoka kwenye
Mabaraza ya Wawakilishi ya Washirika kutoka Chama cha siasa chenye
wawakilishi wengi kwa mujibu wa masharti yatakayowekwa na Katiba za
Washirika na kwa kuzingatia masharti ya Katiba hii.
SABABU ZA MAPENDEKEZO
Lengo ni kuhakikisha kuwa Jamhuri ya Muungano inabakia ni nchi moja
yenye serikali 3 zenye mamlaka na madaraka yake yaliyofafanuliwa na
katiba.
Kwa kuwa tunaamua kuwa na Nchi moja basi Serikali zinazoundwa
zitakuwa ni Serikali Washirika na sio nchi Washirika tena kama rasimu
inavyoita.
Kuweka wazi kuwa ni kiongozi mmoja tu wa Serikali ndiye atachaguliwa na wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano naye ni Rais -
Mkuu wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya Ulinzi na usalama.
Majina ya Wakuu wa Serikali za Washrika yatatolewa na kwa mujibu wa
Katiba zao na hivyo hakuna sababu kwa Katiba ya Muungano kuunda majina
isipokuwa tu Wakuu wa Serikali za Washirika watakuwa ni Makamu wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano kwa kuzingatia kuwa iwapo Rais wa Muungano
anatoka upande mmoja wa Muungano, makamu wa kwanza atatoka upande wa
pili wa Muungano. Makamu wa Rais wanaweza kukaimu Urais kwa masharti
maalumu yatakayowekwa na Katiba.
Mapato na mgawanyo wa Mapato ya Muungano katika Serikali Tatu
Dola inapaswa kuwa na rasilimali za kutosha na ziada inaweza kugawa
kwa Washirika na Mikoa katika wajibu wa kuhakikisha maendeleo yanawiana.
Dola pia inaweza kuwa na miradi ya Muungano. Kuna haja ya kuangalia kwa
umakini mkubwa suala hili la mapato ya Serikali ya muungano kama kweli
kuna nia ya dhati ya kuendelea kuwa na Muungano. Mapendekezo yangu ni
kama ifuatavyo;
Mapato ya Muungano
1. Ushuru wa Forodha
2. Mrahaba wa uvunaji wa Rasilimali ambapo 25% itabaki kwenye mkoa
wenye rasilimali na 75% itatumika na Serikali ya Muungano kugawa kwenye
mikoa kwa mujibu wa ‘formulae’ itakayokubaliwa kwa kuzingatia idadi ya
watu, kiwango cha umasikini na ukubwa wa kijiografia.
3. Ushuru wa Bidhaa na huduma ambapo 60% itagawiwa kwa nchi Washirika kwa ajili ya miradi maalumu ya muungano.
4. Mapato kutoka kwenye kampuni za kibiashara za Serikali ya Muungano na gawio la Benki Kuu ya Tanzania.
Mapato ya Serikali za Washirika
1. Kodi ya Mapato ya watu binafsi na Makampuni
2. Kodi ya Ongezeko la Thamani au kodi kama hiyo
3. Tozo mbalimbali zitakazotungwa kwa mujibu wa sheria
4. Mapato yasiyo ya kikodi kutoka idara na Wizara za Serikali.
Mapato ya Mikoa
1. 25% ya Mrahaba kutokana na uvunaji wa Rasilimali/maliasili inayopatikana katika mkoa husika
2. 10% ya makusanyo ya kodi ya mapato ya watu binafsi na makampuni kutoka katika mkoa husika
3. Mgawo kutoka Serikali ya Muungano
4. Mgawo kutoka Serikali ya Washirika
5. Tozo mbalimbali zitakazoanzishwa kwa mujibu wa sheria ndogo ndogo zitakazopitishwa na Mabaraza ya Mikoa


Post a Comment