Bunge la
Bajeti la mwaka wa fedha wa 2014/15 linatarajia kufanya vikao vyake hadi
saa mbili usiku pamoja na siku za Jumamosi ikiwa ni moja ya njia za
kufidia siku 28 zilizopunguzwa kufanya vikao hivyo.
Tofauti
na Bunge la Bajeti lililopita ambalo lilifanya vikao kwa siku 80, mwaka
huu litafanya vikao vyake kwa siku 52 kuanzia Mei 6 hadi Juni 27, mwaka
huu.
Mabadiliko
hayo yametokana na kuliwa kwa baadhi ya siku na Bunge Maalumu la Katiba
lililoahirisha vikao vyake Ijumaa iliyopita hadi Agosti mwaka huu.
Kutokana
na uchache huo wa siku, Bunge linatarajiwa kupitisha mapendekezo ya
kuongeza dakika 65 zaidi ya muda uliopangwa kwa mujibu wa Kanuni za
Bunge za mwaka 2013, pia vikao kufanyika hadi Jumamosi.
Kwa
mujibu wa Kanuni ya 28, vikao vya Bunge hutakiwa kuanza saa tatu asubuhi
hadi saa saba mchana kwa Jumatatu hadi Ijumaa na kuahirishwa hadi saa
11:00 jioni ambako huendelea hadi saa 1:45 jioni.
Katika
mapendekezo mapya, Bunge linakusudia kuanza vikao saa 3:00 asubuhi hadi
saa 7:00 mchana na kurudi saa 10:00 jioni hadi saa mbili usiku.
Taarifa
iliyotolewa juzi na Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa
Kimataifa ya Ofisi ya Bunge ilisema siku za Ijumaa Bunge litaahirisha
vikao vyake vya mchana saa moja kabla ya muda wa kawaida wa saa 7:00.
Iwapo
Bunge litapitisha mapendekezo hayo, kutakuwa na ongezeko la saa sita na
nusu kila wiki, hatua ambayo inaweza ikaongeza kidogo muda wa kujadili
masuala mbalimbali ya Bajeti ya Serikali.
on Tuesday, April 29, 2014


Post a Comment