CHAMA Cha
Mapinduzi (CCM) kimetaka wabunge wake, kuhakikisha wanafanya tathmini
na kupitia upya Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na kuweka
viwango vya tozo hiyo, kulingana na huduma inayotolewa kupunguza
malalamiko ya wananchi.
Hayo
yalisemwa mjini hapa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana,
alipotembelea mradi wa ujenzi wa nyumba 60 za Shirika la Nyumba la Taifa
(NHC) katika kijiji cha Inyonga wilayani Mlele mkoani Katavi.(Martha Magessa)
Viongozi
wa shirika hilo, walimlalamikia kiongozi huyo wakitaka asaidie kodi ya
asilimia 17, inayotozwa kwa kila nyumba za shirika hilo ipunguzwe
kulingana na matumizi yake, gharama za uuzaji wa nyumba hizo nayo
ipungue na wananchi wengi waweze kuimudu.
Akijibu
hoja hiyo, Kinana alisema wakati umefika kwa Serikali kuanza kupitia
sheria zake zinazoleta migogoro katika jamii ikiwemo sheria hiyo ya VAT,
ambayo kwa sasa inatoza kila kitu kwa asilimia 17 bila kujali aina ya
huduma inayotolewa.
“Ziko
nyumba kweli za kutozwa kodi kubwa kama vile zile za biashara, au
kampuni za madini, gesi na mahoteli makubwa, lakini nyumba hizi za
wananchi wa chini nazo kutozwa VAT ya asilimia 17 ni uonevu,
nitafuatilia ili hili nalo lishughulikiwe,” alisisitiza Kinana.
Akiwasilisha
taarifa ya mradi huo wa ujenzi wa nyumba 60 katika Wilaya ya Mlele,
Meneja wa NHC katika mikoa ya Katavi na Rukwa, Nehemia Msigwa, alisema
tayari shirika hilo limeanza ujenzi wa nyumba hizo katika eneo la ekari
nane lililonunuliwa kwa thamani ya Sh milioni 19.
“Huu ni
mwendelezo wa utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2010 ambayo inalitaka
shirika hili kujenga nyumba 15,000 hadi kufikia mwakani, hadi sasa
lengo hili tumelitekeleza kwa asilimia 90 na tunauhakika hadi ifikapo
mwakani tutakuwa tumefikia lengo,” alisema Msigwa.
Alisema
ujenzi wa nyumba hizo ambao utachukua muda wa miezi nane, ukikamilika,
nyumba hizo zitauzwa kwa viwango tofauti ikiwemo gharama za juu, kati na
bei nafuu ili wananchi wengi waweze kumudu.
Post a Comment