MJUMBE wa
Bunge Maalumu la Katiba, Zarina Madabida amesema kitendo cha wajumbe
wenzao wa Bunge hilo wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutoka
bungeni juzi kinaashiria mizimu ya waasisi waliowafanyia dhihaka,
inawafuatilia.
Madabida
alisema jana akichangia mjadala wa Rasimu ya Katiba, sura ya kwanza na
ya sita mjini hapa kuwa, ni fedheha kubwa kuwakashifu waasisi wa Taifa
la Tanzania na kwamba, hali haiwezi kuwa shwari kwa waliofanya kitendo
hicho.
“Walianza
na Hati ya Muungano, sasa imepatikana wameanzisha chokochoko nyingine,
hapa niseme ‘maweeeee’, Katiba itapatikana kwa udi na uvumba, haya yote
ni mizimu ya wakubwa waliowafanyia dhihaka,” alisema Madabida.
Alisema
ni bora wajumbe hao wakapata aibu kuliko fedheha, wakaamua kurejea
katika Bunge ili kuonesha uzalendo wa kweli na kuandika Katiba kwa
maslahi ya Watanzania.
“Rudini muombe msamaha Watanzania kwa kitendo chenu hicho, rudini tutunge Katiba,” alisema Madabida.
Mjumbe
huyo alishangaa kitendo cha mjumbe Profesa Ibrahimu Lipumba, kuzungumza
kile alichodai uchochezi na ubaguzi ndani ya Bunge na kudai kwa mtu
anayeheshimika ndani na nje ya nchi kama Lipumba, hakupaswa kufanya
alichofanya.
Profesa
Lipumba juzi, alipojadili kuhusu Rasimu hiyo, alisema kumekuwa na
vitendo vya ubaguzi, matusi na vitisho huku akimtaja Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi kuwa
alitoa hotuba ya uchochezi na vitisho kwamba jeshi litachukua nchi ikiwa
serikali tatu itapitishwa.
Alisema
Lukuvi alifanya hivyo na kushawishi wananchi waunge mkono serikali mbili
Jumamosi iliyopita katika Kanisa la Methodist mjini hapa kwenye Ibada
ya kumsimika Mchungaji Joseph Bundala kuwa Askofu.(Martha Magessa)
Lukuvi
alimwakilisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Baada ya kujadili hotuba ya
Lukuvi, Profesa Lipumba aliwaongoza Ukawa wote na baadhi ya wajumbe wa
kundi la 201, kutoka nje ya ukumbi wa Bunge.
“Mtu
mwenye ghariba kama Profesa Ibrahimu Lipumba kufanya uchochezi
alioufanya hapa jana (juzi), kuanza kugombanisha Watanzania ni hatari
sana,” alisema Madabida.
Naye
Mjumbe Dk Christine Ishengoma aliungana na Madabida kuwataka wajumbe hao
kurejea bungeni ili kutengeneza Katiba. Hoja ya kuwataka warudi,
ilitolewa pia na Mjumbe mwingine Athuman Mfutakamba akiwataka warudi
bungeni na kuridhia ukweli kwamba wananchi wanataka muundo wa serikali
mbili na si vurugu.
CHANZO:HABARILEO
Post a Comment