Mzee Petro Bulimi akiwa nyumbani kwake.
Mzee mwenye
miaka 72, Petro Bulimi mkazi wa Kijiji cha Itwimila A, Wilaya ya Magu
mkoani Mwanza anatembea kwa kutumia mikono na miguu kufuatia kusumbuliwa
na tatizo la uvimbe katikati ya uti wa mgongo. Ugonjwa
huo pia umesababisha kuibukwa kwa magonjwa mengine kibao yakiwemo ya
miguu kuchezacheza kama kuna golori ndani yake zinazozunguka.
Matatizo hayo yamesababisha mzee Petro kushindwa kutembea kama binadamu wengine! Ama kweli hujafa hujaumbika!
Akisimulia
kwa uchungu huku akiwa ameshika sikio moja ili apate uelekeo mzuri wa
mawimbi ya sauti, mzee huyo alisema alianza kuumwa mwaka 2007 kwa
kuvimba tumbo na kuwa kama mama mjamzito, baadaye alipelekwa Hospitali
ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure ambapo ugonjwa haukupatikana.
Mwaka
2008, alisema mzee huyo, alipata kizunguzungu kikali ambacho kilitibiwa
kwa dawa za kienyeji na kupona ila bado mwili haukurudi katika hali ya
kawaida kwa tumbo kuvimba.
Alisema
mwaka 2009 alipelekwa Hospitali ya DDH wilayani Bunda, Mara ambako
vipimo vilionesha kuwa, ana TB ya mifupa, alipatiwa dawa na kurudi
nyumbani.
Baada
ya miezi 6 alipona TB, lakini ndipo ukawa mwanzo wa miguu yake kupooza
na kukosa nguvu. Hakuweza kusimama tena kama zamani, muda mwingi
aliutumia kulala na kukaa kwenye kiti cha kuegamea na alipotaka kutoka
sehemu moja kwenda nyingine alitumia na mikono (angalia picha).
Mzee Petro aliendelea kusema kuwa, uliibuka uvimbe katikati ya uti wa mgongo uliomsababishea kupinda kwa mgongo.
Mzee Petro
alisema ameshahangaika sana kutafuta tiba lakini wapi! Amefikia hatua ya
kukata tamaa kwa sababu sehemu nyingi za tiba akienda anaambiwa atoe
shilingi 250,000 kwa ajili ya dawa.
Aliongeza kuwa, maisha yake
yamekuwa magumu sana kutokana na maradhi yaliyomkumba ambayo anaamini
kama atapata tiba ya uhakika atapona.
“Kwa sababu nashindwa
kutembea, nitashukuru sana kama nitapata baiskeli ya kukalia (wheel
chair) kwa sababu itanisaidia kutembelea kwa muda huu ninaosubiri kufa,”
alisema mzee huyo.
Kwa Watanzania walioguswa na
tatizo la mzee Petro wanaweza kumsaidia kwa kutuma fedha kupitia namba
0753 489614, Emmanuel Nhambi.
Post a Comment