Dar es Salaam. Bajeti
inayotarajiwa kuwasilishwa hivi karibuni bungeni Dodoma haitakuwa na
manufaa yoyote kwa Watazania, iwapo Serikali haitakuwa tayari kupunguza
nakisi inayotokana na matumizi makubwa yasiyokuwa ya lazima.
Akizungumza
baada ya uzinduzi wa Ripoti ya Ukuaji wa Kiuchumi kwa nchi za Afrika
Kusini mwa Jangwa la Sahara iliyotolewa na Repoa, Mtaalamu wa Uchumi,
Profesa Ibrahim Lipumba alisema tatizo lililopo kwa sasa ni matumizi
makubwa ya Serikali kwa mambo yasiyo ya lazima, huku ikiwa na mapato
madogo.
Profesa
Lipumba ametoa maoni hayo siku moja baada ya Waziri wa Fedha, Saada
Nkuya kuliambia gazeti hili kuwa masharti ya wahisani na utegemezi wa
fedha ni mambo ambayo kwa kiasi kikubwa yanakwamisha utekelezaji wa
miradi mingi ya maendeleo nchini.BBBB
Pamoja na
kukiri imekuwa vigumu kwa Tanzania kuridhia masharti mapya ya wahisani,
pia alikiri kwamba matumizi ya Serikali yamekuwa makubwa kuliko mapato,
hivyo kusababisha nakisi kubwa katika bajeti ya mwaka 2013/14.
Hata
hivyo, Profesa Lipumba alifafanua chanzo cha tatizo hilo wakati wa
uwasilishaji ripoti iliyoandaliwa na Taasisi ya Utafiti na Kupunguza
Umaskini (Repoa) kwa kushirikiana na Shirika la Fedha Duniani (IMF)
ikilenga kuangalia ukuaji wa kiuchumi kwa nchi za Afrika Kusini mwa
Jangwa la Sahara, Tanzania ikiwa miongoni.
Alieleza
kwamba matumizi hayo ni pamoja na ya zaidi ya Sh60 bilioni zilizotumika
kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo hata baada ya kukamilisha
kazi yake, Serikali imesimamia kutotumia mapendekezo ya Rasimu ya Katiba
iliyoandaliwa, hivyo kupoteza mabilioni ya shilingi za walipa kodi bila
sababu.
“Pamoja
na matumizi makubwa ya Tume, matumizi ya Bunge la Katiba bado thamani
halisi ya fedha za walipa kodi haiwezi kulipwa kwa utaratibu ambao
Serikali imeamua kuutumia. Hapa tunaona namna Serikali inavyokuwa na
matumizi makubwa ambayo hayana tija kwa wananchi,” alisema.
Alisema
ili kuondoa kasi ya ukuaji wa nakisi, Serikali pia inatakiwa kufuta
kabisa misamaha holela ya kodi inayofikia Sh1 trilioni na bilioni 800
ambayo ni sawa na asilimia tano ya pato la taifa.
Alisema
miongoni mwa maeneo mengine yanayosababisha tatizo hilo ni katika miradi
inayosimamiwa na Serikali ambayo mingi imekuwa ya gharama kubwa kuliko
uhalisia na gharama huongezwa kwa kati ya asilimia 30 hadi 50 zaidi ya
gharama halisi.
Hata
hivyo, akizungumzia ripoti hiyo ya Repoa iliyoangazia zaidi ukuaji wa
kiuchumi kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, alisema japokuwa
uchumi huo unakua, haujaweza kuwasaidia wananchi wa kawaida katika nchi
za Afrika.
Awali,
mwakilishi wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) nchini, Thomas Baunsgaard
alisema japokuwa ukuaji wa uchumi umekuwa ukitia moyo na Tanzania
inafikia asilimia 7.2, bado upunguzaji wa umaskini unakwenda kwa kasi
sana.
Alisema
kupungua uzalishaji kwenye sekta ya kilimo kumechangia ukuaji wa sekta
ya utoaji huduma na Dar es Salaam idadi ya maskini imepungua. (CHANZO: MWANANCHI) (FS)
Post a Comment