Dar es Salaam. Aliyekuwa
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema
wanasiasa wanaomtuhumu kwa kumsaliti Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Nyerere kuhusu Muungano, ndiyo wasaliti kwa kuwa waliingiza kwenye
Katiba, mambo yanayokinzana na makubaliano ya Muungano huo.
Jaji
Warioba amesema usaliti huo ni pamoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
kuondoa mamlaka ya Bunge la Muungano katika utungaji wa sheria,
kuitambua Zanzibar kuwa nchi inayojitegemea na kuongeza mambo ya
Muungano bila kufuata Katiba.
Ametoa
kauli hiyo kujibu mwendelezo wa lugha za kejeli na matusi anazorushiwa
na baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wengi kutoka CCM na
baadhi ya viongozi wa Serikali baada ya Tume aliyoiongoza kupendekeza
muundo wa serikali tatu.
Akizungumza
juzi usiku katika kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na Kituo cha
Televisheni cha ITV, Jaji Warioba alisema viongozi wa pande mbili za
Muungano wanaomtuhumu, ndiyo waliouvuruga Muungano huo
“Mwalimu
aliacha Bunge likiwa na mamlaka kamili, aliacha nchi ni moja, aliacha
mambo ya Muungano 11 sasa yamekuwa ni 22, kwa bahati nzuri Rais Jakaya
Kikwete alieleza bungeni hilo kwamba mambo hayo yaliongezekaje,” alisema
na kuongeza:
“Katika
kubaini kuongezeka kwa mambo ya Muungano ndivyo ilikuwa inapunguza
mamlaka kwa Zanzibar, mambo 11 yaliyoachwa na mwalimu yaliingizwa
kikatiba lakini haya yaliyoongezeka yalipatikana kienyeji.”
Jaji
Warioba alisema enzi za uhai wake, Mwalimu Nyerere aliheshimu na
kuilinda Katiba hivyo, walioivunja ndiyo wasaliti wa Muungano.
“Sasa
kati ya mimi na wao ni nani msaliti kwa Mwalimu, angekuwapo (Mwalimu) ni
yupi angeonekana msaliti wa Serikali ya Muungano? Wao ndiyo
wameuvuruga, alichokiacha Mwalimu ni tofauti na kinachoonekana kwa
sasa,” alisema Jaji Warioba.
Kuhusu Bunge
Jaji Warioba alisema mipango mingi ya maendeleo inayopangwa ndani ya Bunge la Muungano inatekelezwa upande wa Bara pekee.
“Si hivyo
tu, Bunge hilo linajadili mambo ya Bara tu na halihusishi upande wa
Zanzibar. Zanzibar nayo inajadili mambo yake na kujiamulia lakini jina
la Bunge hilo ni Muungano,” alisema Jaji Warioba.
Kutokana
na mazingira hayo, Jaji Warioba alisema Zanzibar iliamua kuondoa mamlaka
ya Bunge hilo katika utungaji wa sheria kupitia Baraza la Wawakilishi
Zanzibar.
“Katiba
ya Jamhuri ya Muungano inasema sheria zinazotungwa katika Bunge hilo
zitatumika ndani ya pande zote za Muungano, lakini Zanzibar
wakabadilisha hilo kupitia Katiba yao wakasema sheria zote
zitakazotungwa ndani ya Bunge hilo, lazima zipitiwe tena na Baraza la
Wawakilishi,” na kuongeza: “(Zanzibar) Hawakuishia hapo, wakafanya
mabadiliko ya Katiba mwaka 2010 iliyovunja Katiba ikiitambua Zanzibar
kama nchi kamili, ikaondoa mamlaka ya Rais wa Jamhuri kugawa wilaya na
mikoa kwa Zanzibar tofauti na Katiba ya Muungano, kwa maana hiyo
Zanzibar ikavunja nguvu ya Bunge la Muungano.”
Aidha,
alisema hatua hiyo ilionekana kuuvunja Muungano kwa vitendo baada ya
kuvunja mamlaka ya Rais na kutambua marais kamili katika nchi mbili
tofauti.
“Kwa
kawaida nchi inakuwa na amri jeshi mkuu mmoja ambaye anapigiwa mizinga
21, Jeshi la Muungano linapiga mizinga kwa marais wawili kitu ambacho
hakiwezekani,” alisema.
Malalamiko ya Watanganyika
Jaji
Warioba alisema Kwa upande wa Tanzania Bara, walibaini malalamiko ya
Watanganyika kuwa ni pamoja na kukosa fursa mbalimbali ndani ya
Zanzibar. “Watu wa bara nao wanasema Zanzibar inashiriki Bunge la
Muungano, inakagua miradi ya bara na kuihoji lakini wao hawana nguvu ya
kushiriki mambo hayo kwa upande wa Zanzibar,” alisema.
Aliongeza:
“Mbaya zaidi wanasema Wazanzibari wanaweza kumiliki ardhi na kupata
uraia kwa upande wa bara lakini haki hizo haziwezi kupatikana kwa
Mtanganyika, njia pekee tukaona ni vyema Zanzibar nayo ilete mambo yake
ndani ya Muungano lakini ikashindikana.”
Hoja ya takwimu
Jaji
Warioba aliwataka wajumbe wa Bunge wasihangaike na takwimu badala yake
wajibu maswali yaliyojitokeza kutoka kwa washirika wa Muungano.
“Takwimu
siyo tatizo, sisi hatukufanya jambo jipya, ila ilikuwa ni kama marudio
tu ya Tume ya Nyalali, wanahoji takwimu hizo je, hawakuona dosari kwa
takwimu za maoni ya asilimia 20 kwa jaji Nyalali?
Alisema
Tume yake ilizunguka nchi nzima ikiwa na waandishi waliorekodi kwa tepu,
video na maandishi kwa ajili ya kuweka kumbukumbu katika mtandao wa
Tume. (CHANZO: MWANANCHI) (FS)
Post a Comment