MKUU wa Wilaya ya Kiteto, Martha Umbulla, amefanikiwa kumuondoa
katika ndoa mwanafunzi aliyekatishwa masomo na kulazimishwa kuolewa.
Mkuu huyo wa Wilaya (DC) amefikia hatua hiyo baada ya aliyekuwa
mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Uloki Moshi, Ngaya Baraka (17)
aliyeolewa mwezi mmoja uliopita kumpigia simu na kumuomba kumsaidia kwa
kuwa bado anahitaji kusoma.
Akielezea mkasa huo huo jana, Ngaya, alisema hakutaka kuolewa na
badala yake aendelee na masomo, lakini baba yake alimlazimisha.
Alisema kutokana na msimamo wa baba yake alilazimika kuwatafuta
viongozi mbalimbali kwa ajili ya kujiami, lakini hakufanikiwa na wakati
huo alikuwa akimtafuta mkuu wa wilaya bila mafanikio.
“Siku moja nilipokuwa natoka shule nilimkuta baba ameshamwandaa
kijana wa kiume ambaye alinipakia kwenye pikipiki na kunipeleka vijiji
vya porini. Nilikaa na mwanaume huyo kwa uchungu huku akipata mateso ya
kuchunga mifugo.
Alinipora simu ili nisiwasiliane na mtu yoyote,”
alisema.
Alieleza alifanikiwa kupata mawasiliano na kumpigia simu mkuu huyo wa
wilaya ambaye aliwatuma viongozi mbalimbali na kufanikiwa kumtoa kwa
mume huyo ambaye kwa sasa amekimbia.
Kutokana na hali hiyo, mkuu huyo wa wilaya ametangaza hali ya hatari
kwa jamii ya wafugaji wenye tabia ya kuwaozesha watoto wao wakiwa na
umri mdogo.
Alisema mapambano hayo yataenda sambamba na kuwachukulia hatua kali wazazi ambao wanakatisha masomo watoto wao.
Alisema kitendo kilichofanywa na familia ya binti huyo ni kitendo cha
udhalilishaji na unyanyasaji kutokana na kumkatisha masomo na
kumlazimisha kuolewa na mfugaji kwa lengo la kulipwa mahari ya ng’ombe
20.
Chanzo;Tanzania Daima
Post a Comment