Rais
Jakaya Kikwete akiwa katika mahojiano maalumu na Mtangazaji Daniel
Kalinaki wa Kituo cha Televisheni cha Nation (NTV) kinachomilikiwa na
Nation Media Group, Ikulu jijini Dar es Salaam. Picha na Ikulu
Dar es
Salaam. Rais Jakaya Kikwete ameendelea kusisitiza kuwa Tume ya Jaji
Joseph Warioba haina ushahidi kwamba Watanzania wengi wanataka muundo wa
Muungano wa serikali tatu.
Kauli
hiyo aliitoa wiki hii jijini Dar es Salaam kwenye mahojiano maalumu na
Kituo cha Televisheni cha NTV kilichopo chini ya Nation Media Group
(NMG).
Baadhi ya
vyombo vingine vya habari vilivyo chini ya NMG ni gazeti hili la
Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti kwa upande wa Tanzania, Daily
Monitor kwa upande wa Uganda na Daily Nation kwa upande wa Kenya.
Rais Kikwete
ambaye moja ya mambo atakayokumbukwa kwenye uongozi wake ni kuasisi
mchakato wa Katiba, alizungumzia hoja ya serikali tatu akisema, hakuna
ushahidi kwamba Watanzania wengi wanataka muundo wa Muungano wa serikali
tatu.“Hakuna ushahidi kwamba watu wengi katika nchi hii wanataka
serikali tatu, hakuna ushahidi wa namna hiyo, hata tume yenyewe
haikubaini hicho. Kinachofanywa na vyombo vya habari ni kuandika habari
za wajumbe wa Bunge la Katiba wanaotaka serikali tatu, ndiyo kwenye
masilahi yao, wanapaza sauti za wale wanaotaka serikali tatu, hao ndiyo
sauti zao zinasikika. Lakini hawataki kupaza sauti za wale wanaotaka
serikali mbili,” alifafanua.
Hii ni
mara ya pili kwa Rais Kikwete kuikosoa ripoti ya Tume ya Mabadiliko ya
Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba. Mara ya kwanza aliikosoa
wakati akizindua Bunge la Katiba Machi 21 mjini Dodoma.
Rais
Kikwete ambaye amewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa kwa kipindi cha miaka 10, katika mahojiano hayo alisema katika
kuadhimisha miaka 50 ya Muungano, jambo muhimu na kubwa ni kuendelea
kuwapo kwa Muungano.
“Tunayo mifano ya nchi zilizojaribu kuungana, lakini zilishindwa, Senegal-Gambia, Ghana-Guinea, Misri na Libya.
“Muungano
umeendelea kuwepo kwa nusu ya karne ni mafanikio makubwa. Kumekuwepo na
wakati mgumu na changamoto mbalimbali, lakini tumeweza kukabiliana nazo
na umeendelea kuwa imara zaidi. Siyo kuendelea kuwepo tu pia umeendelea
kuimarika na mchakato wa mabadiliko ya Katiba utaimarisha zaidi
Muungano na tutakuwa na Muungano imara baada ya kupata Katiba Mpya,”
alifafanua Rais Kikwete.
Akizungumza
kwa kujiamini kutokana na uzoefu wake wa muda mrefu ndani ya CCM na
Serikali, Rais Kikwete alisema Muungano ulikotoka ulikuwa imara na
umeendelea kukua katika hali ya uimara wake.
“Kuna mambo ambayo tumefanya yamezidi kuimarisha Muungano na umeendelea kuwa na mafanikio makubwa.”
Rais
Kikwete: “Mimi ni mmoja wa wanaoamini kwamba muundo wa serikali mbili ni
bora zaidi kwetu. Siyo suala la kuendeleza hali iliyopo, ni muhimu
kubadilika kama kuna sauti zinazotaka kubadilika na pia kama kuna hoja
nzito ya kutaka mabadiliko, lakini sioni kama Muungano wa Serikali tatu
ni hoja nzito ya kufanya mabadiliko, itasababisha matatizo mengine na
mwisho kusababisha muungano kuvunjika.”
Rais
Kikwete ambaye katika uzoefu wake wa kazi za kisiasa amewahi kufanya
kazi Zanzibar, alisema alipoingia madarakani mwaka 2005 hoja kuu ilikuwa
ni kutatua mzozo wa kisiasa uliokuwa ukiendelea kwa muda mrefu kati ya
vyama vya CUF na CCM visiwani humo.
Alisema:
“Tumeweza kuutatua na sasa tuna Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Kabla ya
hapo kulikuwa na matatizo mengi, wakati wa uchaguzi mambo yanatulia,
ukimalizika uchaguzi kunazuka matatizo ya kisiasa, tukaamua kuvileta
vyama hivi pamoja tukafanya mjadala wa kina na uamuzi uliofikiwa ni kuwa
na serikali ya umoja wa kitaifa, na sasa Zanzibar kuna utulivu wa
kisiasa.”
Rais
Kikwete akizungumzia suala la Muungano alisema wakati wa Rais wa Awamu
ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, aliunda tume, Tume ya Shelukindo (iliongozwa
na William Shelukindo) kuangalia kero za Muungano na walikuja na kero
31.
Alisema alipoanza kazi mwaka 2006 kero za Muungano zilikuwa zimebaki 13, akashughulikia kero tisa, zimebaki kero nne tu.
Rais
Kikwete alisema kimsingi uhuru wa vyombo vya habari kwa Tanzania ni
mpana na kwamba hata gazeti lililofungiwa ni moja na mengine yalifungiwa
kwa muda tu.
Alisisitiza
kwamba habari za kuchochea majeshi kufanya mapinduzi, habari za
kuchochea vijana kuleta vurugu hatazivumilia, na kwamba chombo cha
habari kitakachojielekeza kwenye habari za namna hiyo kitafungiwa.
“Wakiandika
Rais Kikwete nchi imemshinda hainipi tabu, kwa kuwa najua nchi
haijanishinda,” alisema Rais Kikwete huku akitoa mfano wa namna redio
Mille Collines ya Rwanda ilivyochangia mauaji ya halaiki nchini humo.
Rais
Kikwete alitoa mfano mwingine wa namna vyombo vya habari vilivyochangia
uvunjaji wa amani ni mwandishi wa habari wa Kenya ambaye amefunguliwa
mashtaka ya uhalifu wa kimataifa katika Mahakama ya Kimataifa ya Makosa
ya Jinai (ICC), iliyopo The Hague nchini Uholanzi.
Mwandishi
wa habari aliyefunguliwa mashtaka ICC ni mtangazaji wa Kituo cha Redio
ya Kass FM, Joshua arap Sang. Rais Kikwete huku akicheka alimuhoji
mtangazaji wa NTV “Unataka habari kama hizo tuzivumilie?”
Kuhusu
rushwa, Rais Kikwete aliitaja idara ya mahakama kuwa ni moja ya
changamoto na wiki iliyopita alizungumza na Jaji Mkuu kuona namna gani
wanaweza kuboresha, kuongeza mafunzo kwa wapelelezi au waendesha
mashtaka, kutokana na watuhumiwa wengi wa rushwa kuachiwa huru.
Kuhusu
uchumi, Rais Kikwete ambaye amewahi kuwa Waziri wa Fedha alisema
kinachofanyika ni kuimarisha uchumi mkubwa, na kwa mujibu wa wachumi,
uchumi wa nchi ukikua kwa asilimia saba katika kipindi cha miaka 10,
pato la taifa huongezeka mara mbili na uchumi wa Tanzania umekuwa ukikua
kwa asilimia saba kwa kipindi hicho.
Alisema
suala si kuendelea kwa muundo ulivyo sasa, suala la msingi ni kujadili
namna ya kutengeneza muundo wa Muungano, kwamba upi ni bora.
Source: mwananchi.co.tz



Post a Comment