
Mwenyekiti
wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta anahaha kulinusuru Bunge hilo,
baada ya wajumbe ambao ni wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) kususia vikao vinavyoendelea mjini Dodoma.
Habari
ambazo zimelifikia gazeti hili zilisema Sitta anawasaka viongozi wa
Ukawa kwa lengo la kukaa nao katika meza ya mazungumzo, kutafuta
maridhiano yatakayowezesha kundi hilo kurejea bungeni.
Sitta jana
aliliambia Mwananchi kuwa wako njiapanda, kwa sababu hawafahamu kama
wajumbe hao wa Ukawa wametoka tu nje ya ukumbi na watarudi au
wamejiuzulu.
"Hapa
ninapozungumza na wewe nimesitisha kwenda mapumziko ya Pasaka...
Nimewapigia simu Lipumba (Ibrahim) na Mbowe (Freeman), lakini hawapokei
simu," alisema Sitta na kuongeza;
"Niliyempata
ni Mbatia (James) peke yake na ameniambia yeye yuko na wenzake na hana
uamuzi wa pamoja...Nataka nikutane nao ana kwa ana nasubiri kama
inawezekana tufanye mazungumzo."
Aliongeza:
"Nasubiri hata kama watatuma mwakilishi wao tukae tuzungumze hili
jambo, lakini mpaka sasa sijaona mwakilishi yoyote...huwezi kuamini
sijaenda Pasaka niko hapa Dodoma."
Sitta
alisema pamoja na viongozi hao wawili wakuu wa Ukawa hawapokei simu,
lakini amefanya jitihada ikiwamo kuwatumia ujumbe mfupi wa maneno (SMS),
lakini hadi jana mchana alikuwa hajajibiwa.
"Sitaki
kuongeza chochote kuhusu hili jambo kwa sababu kwa mazingira yenyewe
nikisema chochote ninaweza kuharibu japo nina maoni yangu binafsi kuhusu
hili, lakini sitaki kusema sasa," alisema Sitta.
Jana
gazeti hili lilimtafuta Mbatia ambaye alikiri kuzungumza na Sitta. "Ni
kweli amenipigia simu na nimemwambia kwamba nimemsikia, lakini siwezi
kufanya uamuzi peke yangu, lazima nishuriane na wenzangu."
Hata
hivyo, Mbatia alisema kwa mtizamo wake hadhani kama Sitta anaweza
kutatua mvutano uliopo na kwamba wanaopaswa kusimamia suala hilo ni
viongozi wa vyama vya siasa vinavyovutana.
"Mimi
naamini katika maridhiano, lakini vyama vya siasa ndivyo vinaweza
kutatua mzozo huu, kwa hiyo viongozi wa CCM ndiyo wanaweza kuonyesha nia
ya kuzungumza, Sitta ni kiongozi wa Bunge ambaye kazi yake ni kusimamia
uendeshaji wa vikao, hivyo suala la maridhiano kwake ni kumtwisha mzigo
mzito ambao hapaswi kuubeba," alisema Mbatia.
Kanuni za
uendeshaji wa Bunge hilo za 2014, zinasema kuwa ili ibara au Rasimu ya
Katiba iweze kupitishwa itahitaji kuungwa mkono na theluthi mbili ya
wajumbe kwa pande zote za Muungano.


Post a Comment