
Dar es Salaam.
Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) inatarajiwa kupata ushindani baada ya
Serikali kuamua kuruhusu wawekezaji wa sekta binafsi kutumia Reli ya
Kati.
Uamuzi
huo wa Serikali huenda ukaongeza ufanisi kwa shirika hilo ambalo kwa
miaka mingi limekuwa likikumbwa na matatizo ya kiufanisi.
Baada
ya kuanzishwa mwaka 2007, TRL ilikumbwa na misukosuko baada ya
mwekezaji Rites kutoka India kushindwa kulisimamia kikamilifu na
kusababisha hasara ya mabilioni. Kabla ya TRL reli ya kati ilikuwa chini
ya Shirika la Reli (TRC) ambalo nalo halikuwa na ufanisi.
Akizungumza
katika ufunguzi wa warsha ya kuijengea uwezo TRL iliyofanyika Dar es
Salaam jana, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk Shaaban Mwinjaka
alisema kampuni binafsi zitaruhusiwa kuingiza treni zitakazotumia reli
hiyo kwa kulipa ushuru kwa Serikali.
Kutokana
na mabadiliko hayo, Dk Mwinjaka alisema Serikali imeanza kuiandaa TRL
kupambana na ushindani utakaotolewa na kampuni hizo binafsi.
"Katika
hii warsha tunawaandaa kujua kwamba utafikia wakati wanahitaji
kujitegemea. Kwa misingi hiyo basi, tumepata wataalamu kutoka ndani na
nje kuweka mawazo yao pamoja kujua ni namna gani mabadiliko hayo
yatafanyika," alisema Dk Mwinjaka.
Alipoulizwa
kuwa uamuzi huo utaanza kutekelezwa lini, Mwinjaka alisema baada ya TRL
kujengewa uwezo wa kuwa na mabehewa, injini na watumishi wa kutosha ili
kuweka uwanja mzuri wa ushindani.
Hata
hivyo, Mwenyekiti wa Bodi ya TRL, Severin Kaombwe alisema mpango huo
huenda ukaanza baada ya mwaka 2015 kutoka na mkakati uliopo kwenye
Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
"Kwa
sasa tumeshaagiza vichwa (injini) 21 na takriban mabehewa 200 ambayo
yanatarajiwa kufika ndani ya Agosti mwaka huu," alisema Dk Mwinjaka huku
akisisitiza kwamba mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa BRN.
Alisema
injini na mabehewa hayo yana uwezo wa kurekebishwa kupita kwenye reli
zote; za kawaida (ya kati) na ile ya kisasa inayotarajiwa kujengwa.
"Serikali
imeamua kununua aina hiyo ya vifaa ili shughuli za usafirishaji wa
mizigo kupitia reli ya kati ziendelee bila kuathiriwa wakati wa kujenga
reli hiyo mpya na baada ya kukamilika tutarekebisha ili kupita njia
mpya."
Reli
mpya ya kisasa inatarajiwa kugharimu takriban Dola za Marekani 6
bilioni (Sh9.6 trilioni) zinazofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika
(AfDB).
CHANZO MWANANCHI
Post a Comment