Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Gharib Bilal,
anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru
2014, katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, mkoani Kagera Mei tarehe
2.
Hayo
yamesemwa leo na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt.
Fenella Mukangara wakati akiongea na Waandishi wa Habari Mjini Bukoba
kuhusu Mbio hizo.
Mwenge huo utakaobeba ujumbe usemao “Katiba ni Sheria Kuu ya Nchi” wenye kauli mbiu “Jitokeze kupiga kura ya maoni tupate Katiba Mpya”
utakimbizwa katika Halmashauri/Manispaa 165 za Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na kilele chake kitakuwa Mkoani Tabora tarehe14/10/2014.
Ujumbe
kuhusu mabadiliko ya Katiba kwa mwaka huu, umeandaliwa mahususi kwa
lengo la kuwahimiza wananchi kuendelea kushiriki kikamilifu katika
mchakato wa kutengeneza Katiba Mpya unaoendelea hivi sasa ambao mwisho
wake ni wananchi kupiga kura ya maoni ili tupate Katiba Mpya
iliyoboreshwa kwa maendeleo ya Taifa letu. Amesema Dkt. Mukangara.
Amesema
kuwa ujumbe huu utaambatana na kauli za uhamasishaji kuhusu mapambano
dhidi ya UKIMWI, Malaria, Rushwa na Matumizi ya Dawa za Kulevya.
Dkt.
Mukangara ameeleza kuwa nchi yetu bado inakabiliwa na changamoto ya
ugonjwa hatari wa UKIMWI, Malaria, matumizi ya dawa za kulevya na
rushwa, hivyo mwaka huu kupitia Mbio za Mwenge wa Uhuru Serikali
itaendelea kuwahimiza wananchi kupambana kwa dhati ili kumaliza
changamoto hii inayoathiri maisha ya Watanzania.
“Hata
hivyo, Mbio za Mwenge wa Uhuru pamoja na kuendelea kuhimiza umuhimu wa
amani, umoja na mshikamano wa Kitaifa; Serikali kupitia Mbio hizi
imekuwa ikiwahamasisha Wananchi, Mashirika, Taasisi na Wadau mbalimbali
kuchangia kwa hali na mali kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo”.
Amesema Dkt. Mukangara.
Amekumbusha
kuwa falsafa ya Mwenge wa Uhuru ni kumulika maovu ndani na nje ya
mipaka ya nchi yetu, kuleta matumaini ambapo hakuna matumaini, upendo
mahali palipo na chuki na heshima palipojaa dharau.
Post a Comment