GARI la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, limekamatwa na kuendelea kushikiliwa mjini Mombasa nchini Kenya, kutokana na kuwa na namba mbili.
Taarifa
za jana kutoka Kenya zilieleza kuwa polisi nchini Kenya walipata
taarifa za kuwepo kwa gari hilo na watu ambao walionekana kutokuwa na
kazi maalumu.
Baada
ya kupata taarifa hizo, Polisi hao walio katika msako wa wageni na
magari yanayotiliwa shaka kuhusika katika uhalifu na ugaidi, walianza
kulifuatilia na kubaini wahusika wa gari hilo.
Ufuatiliaji
huo kwa mujibu wa taarifa hizo, ulibaini wahusika wa gari hilo
walipofika Mombasa kutokea Tanzania, hawakuonekana kupokewa na mwenyeji
yeyote, hali inayomaanisha wenyewe ni wenyeji wa mji huo.
Taarifa
za Polisi zilibainisha kuwa uchunguzi wao ulibaini kuwa gari hilo
liliwabeba Mbowe, Mbunge wa Mwanza Mjini, Ezekiah Wenje na dereva
Ibrahim Nguzo.
Polisi
hao inadaiwa walitilia shaka gari hilo kutokana na kuwa na namba za
usajili STK 8146, ambazo zilipandishiwa juu ya nambari halisi za gari
hilo ambazo ni KUB.
Uchunguzi
wa Polisi hao ulibaini kuwa Mbowe na Wenje waliwasili Mombasa, Kenya
kwa gari wakitokea Tanzania kupitia mpaka wa Horohoro/Lungalunga na
kwenda moja kwa moja hotelini.
Mashaka
kwa Polisi hao yaliongezeka baada ya Mbowe na Wenje Aprili 26 mwaka huu
kusafiri kwenda Nairobi kwa ndege, na kumwacha dereva pamoja na gari
hotelini.
Kutokana
na hali hiyo, Jumatatu wiki hii saa 5.00 asubuhi askari Polisi wa
Mombasa walimkamata Ibrahim pamoja na gari hilo, baada ya kuonekana
amekaa hotelini muda mrefu bila ya shughuli zozote.
“Hapo
ndipo alipotoa habari kwamba alikuwa akiwasubiri wakubwa zake ambao
walikwenda Nairobi tangu Aprili 26 na hawakuwa wamerejea,” ilieleza
taarifa hiyo.
Kwa
mujibu wa taarifa hiyo, Ibrahim alipoulizwa kwa nini gari lilikuwa na
nambari za kupandishiwa, alijibu huo ulikuwa ni uamuzi wa bosi wake
Mbowe.
Polisi
hao waliamua kukamata gari hilo na kulipeleka katika kituo cha Polisi
cha Kati kwa mahojiano zaidi na baada ya mahojiano, aliachiliwa Ibrahim
huru lakini gari limeendelea kuzuiliwa kituoni hadi Mbowe na Wenje
watakapofika kwa ajili ya kuhojiwa.
Gazeti
hili lilimtafuta msemaji wa Chadema, Tumaini Makene, ambaye aliomba
muda kupata taarifa halisi za tukio hilo na baadaye alituma ujumbe mfupi
wa maneno ambao hakukanusha wala kukubali kutokea kwa tukio hilo.
“Suala
hilo ni la kiutawala napendekeza utafute uongozi wa Bunge…mtafute
Katibu wa Bunge (Dk Thomas Kashililah), bila shaka ataweza kukueleza juu
ya safari ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na mengine yote ya
kiutawala unayotaka kupata majibu yake,” alieleza Makene.
>>Habari leo
Post a Comment