Waziri
wa Katiba na Sheria Dr. Asha-Rose Migiro akiwasilisha taarifa ya
makadirio ya bajeti ya Wizara yake kwa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria
na Utawala jana (Jumamosi, Mei 3, 2014). Kulia kwake ni Naibu wake
Angellah Kairuki na wa pili kulia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo Wiliam
Ngeleja.
Baadhi ya Maofisa wa Wizara ya Katiba na Sheria wakifuatilia mkutano huo. Picha na Wizara ya Katiba na Sheria.
Na Omega Ngole
Serikali
imesisitiza nia yake ya kuendesha shughuli zake kwa uwazi na kusema
maandalizi ya kutunga sheria ya haki ya kupata taarifa kutoka kwa
taasisi za umma yameanza kuongeza uwazi katika uendeshaji wa shughuli za
serikali.
Akiwasilisha
taarifa ya makadirio ya matumizi kwa mwaka ujao wa fedha kwenye Kamati
ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala jijini Dar es Salaam jana
(Jumamosi, Mei 3, 2014), Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Asha-Rose
Migiro alisema dhamira hiyo inatokana na matakwa ya Katiba kuhusu haki
ya kupata taarifa, Mpango wa Kimataifa wa Uendeshaji wa Serikali kwa
Uwazi (OGP) na ahadi ya Rais Kikwete.
“Azma
ya Serikali ni kuendesha shughuli zake kwa uwazi zaidi katika Nyanja
mbalimbali za huduma…hii ni kwa mujibu wa Ibara ya 18 ya Katiba sambamba
na Mpango wa Kimataifa wa Uendeshaji wa Serikali kwa Uwazi (OGP),”
alisema Waziri Migiro na kuongeza:
“Wizara
imeandaa Waraka wa Baraza la Mawaziri kuhusu kutunga sheria ya Haki ya
Kupata Taarifa kutoka taasisi za umma na ni matarajio ya Wizara kuwa
mchakato huu utakamilika kabla ya mwezi Disemba, 2014,” alisema katika
mkutano huo uliohudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria
Angellah Kairuki na viongozi wengine wa Wizara na taasisi zake.
Katika
mkutano huo, Waziri Migiro pia alizungumzia mpango wa Wizara yake wa
kupunguza mlundikano wa mashauri mahakamani ambapo Mahakama ya Tanzania
imeanzisha mpango wa ufanyaji kazi kwa kujipima.
Kwa
mujibu wa Dkt. Migiro, utaratibu huo unaweka wastani wa idadi ya
mashauri yatakayotolewa uamuzi na Majaji na Mahakimu katika kila ngazi
ya Mahakama kwa kila mwaka.
“Katika
Mahakama ya Rufani lengo ni kumaliza wastani wa mashauri 1,200 hadi
1,400 kwa mwaka, Mahakama Kuu mashauri 200 hadi 250 kwa kila Jaji kwa
mwaka , na Mahakama ya Hakimu Mkazi na Wilaya mashauri 250 hadi 300 kwa
kila Hakimu kwa mwaka,” alisema Waziri Migiro katika mkutano huo
ulioongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo na Mbunge wa Sengerema, William
Ngeleja.
Waziri
Migiro, ambaye aliteuliwa na Rais Kikwete kuongoza Wizara hiyo mapema
mwaka huu, alifafanua kuwa utaratibu huo umeshaanza kufanya kazi na
umeonyesha mafanikio makubwa.
Pamoja
na utaratibu huo, Waziri Migiro pia alizungumzia jitihada za Serikali
za kupunguza mlundikano wa wafungwa na mahabusu magerezani kupitia
mpango maalum wa kutenganisha shughuli za mashtaka na upelelezi.
Kwa
mujibu wa Waziri Migiro, kupitia mpango huu, Mkurugenzi wa Mashataka
huchuja majalada yanayowasilishwa kwake na taasisi za upelelezi kwa
kuzingatia ushahidi uliowasilishwa.
“Mkurugenzi
wa mashtaka ndiye mwenye mamlaka ya kutoa hati ya mashtaka baada ya
kujiridhisha na ushahidi unaowasilishwa na vyombo vya upelelezi, hivyo
kupunguza kwa mlundikano wa mashauri mahakamani kutokana na utaratibu
huu wa kuchuja majalada,” alisema na kuongeza:
“Idadi
ya Mahabusu mageezani imepungua kutoka 18,203 mwezi Juni, 2012 na
kufikia 17,284 mwezi Machi, 2014 na idadi ya wafungwa imepungua kutoka
17,548 mwezi Juni, 2013 na kufikia 16,547 mwezi Machi, 2014,” alisema.
Wakizungumza
baada ya Waziri Migiro kuwasilisha taarifa yake, Wajumbe wa Kamati hiyo
waliipongeza Serikali kwa mikakati iliyoanzisha ya kuondokana na
changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya sheria.
“Huu
mpango wa Mahakama wa kujipima wenyewe sisi tumefurahishwa nao sana,”
alisema Mwenyekiti wa Kamati hiyo, William Ngeleja ambaye aliungwa mkono
na mjumbe mwingine wa Kamati hiyo na Mbunge Wa Ngara, Deogratius
Ntukamazina.
Pamoja
na pongezi hizo, wajumbe wa kamati hiyo waliitaka serikali kuongeza
jitihada za kuondokana na changamoto zinazoikabili Wizara hiyo zikiwemo
uhaba wa watumishi na ufinyu wa bajeti.
“Bajeti
ya Wizara hii inayojumuisha mhimili wa Mahakama ni ndogo sana,” alisema
Nimrod Mkono, mjumbe wa Kamati hiyo na Mbunge wa Musoma Vijijini ambaye
aliungwa mkono na Nyambari Nyangwine, Mbunge wa Tarime.
Post a Comment