Waziri
Mkuu Mizengo Pinda, ameiagiza Wizara ya Fedha kuhakikisha madeni ya
walimu yamelipwa hadi kufikia Juni 30 mwaka huu, ili Serikali isiingie
na madeni katika Bajeti ijayo.
Mbali na madeni ya walimu, Pinda alitaka pia madeni ya makandarasi,
pembejeo na mengineo, kulipwa ifikapo Juni 30 kutokana na madeni
kuchangia kutotekelezwa vizuri kwa Bajeti ya mwaka huu.
Pinda alisema hayo jana wakati wa kikao cha wabunge cha kupokea
taarifa ya mfumo wa Bajeti kwa mwaka 2014/2015 na kutaka Wizara hiyo,
kuhakikisha inalipa madeni haraka.
Alisema Bajeti iliyopita, ilikumbana na changamoto nyingi, lakini
katika Bajeti ya sasa, wamejipanga kuhakikisha changamoto hizo
hazijirudii na inatekelezeka, kama ilivyopangwa na kutaka wabunge
kupitia maelezo ya Waziri na kuyachambua kwa makini.
“Bado Bajeti inategemea misaada kutoka nje
na mikopo mpaka nchi itakapokuwa na uwezo wa kujitegemea kwani kila
mwaka inapungua taratibu hasa baada ya gesi toka Mtwara kufika jijini
Dar es Salaam na kuwa na umeme wa uhakika na viwanda vingi kuongeza
uzalishaji,” alisema Pinda.
Pinda alisema katika kukabiliana na tatizo la mapato yasiyokuwa na
kodi na katika Serikali za Mitaa kutofikiwa malengo wameunda timu maalum
ya kufanyia utafiti suala hilo kwa nini hayafikii malengo na kupitia
kila halmashauri kila baada ya miezi mitatu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu, Stephen Wasira
alisema thamani ya wazi ya utekelezaji wa miradi ya Matokeo Makubwa
Sasa, imeonesha mafanikio mazuri na kukubalika kwa utaratibu huo mpya.
Wasira alisema hayo wakati akiwasilisha Rasimu ya mpango wa maendeleo
wa taifa kwa mwaka 2014/2015 katika Bunge lililokaa kama kamati.
Alisema katika kilimo, wametoa mafunzo ya skimu za umwagiliaji kwa maofisa ugani 95 na wakulima 95.
Alisema katika nishati, wateja wapya 138,931 wameunganishiwa umeme
dhidi ya lengo la kuunganisha wateja 150,000 kwa mwaka 2013/2014 na
kupunguza upotevu wa umeme kutoka asilimia 21 hadi 19.
Post a Comment