Zanzibar. Viongozi
wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wameapa kuendelea kudai mfumo
wa Muungano wa serikali tatu nje ya Bunge la Katiba kwa nguvu zote,
ikiwamo kufanya maandamano ya amani nchi nzima.
Msimamo
huo ulielezwa na viongozi hao kwa nyakati tofauti katika mkutano wa
hadhara uliofurika mashabiki kwenye Viwanja vya Kibandamaiti, Unguja
jana.
Mwenyekiti
Ukawa, Freeman Mbowe alisema wameamua kuliacha Bunge la Katiba kutokana
na harufu za rushwa, vitisho na matusi huku baadhi ya wabunge
wakiahidiwa vyeo. Mbowe ambaye hata hivyo hakufafanua zaidi, alisema
Ukawa wameamua kwenda kwa wananchi kuwaeleza dhamira chafu walionayo
wabunge wa CCM katika mpango wao wa kukataa Rasimu ya Tume ya Mabadiliko
ya Katiba iliyowasilishwa na Jaji Joseph Warioba.
“Ni jambo
la hatari katika mchakato wa Katiba wananchi kuwa waoga au hofu...
Lazima tuwe tayari kuwaonyesha watawala kuwa tuna umoja imara,
tunayapigania mataifa huru ya Tanganyika na Zanzibar, Rais Kikwete
(Jakaya) asiwatishe wananchi kwa kivuli cha jeshi kuchukua madaraka,”
alisema Mbowe.
Lipumba anena
Mwenyekiti
Mwenza wa Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba alisema wajumbe wa Ukawa
wameamua kujitoa bungeni kutokana na kauli ya Rais Jakaya Kikwete ambayo
alidai kuwa iliibeza na kuidhalilisha Tume ya Warioba.
Alisema hawatarudi bungeni na kwamba hawawezi kujadili Katiba ambayo siyo maoni ya wananchi.
Alidai
kwamba kwa makusudi Rais Kikwete aliamua kutetea sera za chama chake na
kupingana na maoni yaliyotolewa na wananchi kupitia Tume ya Mabadiliko
ya Katiba.
“Rais
Kikwete ameharibu nia ya kupatikana Katiba Mpya, amekuwa akijulishwa
kila hatua na jinsi maoni ya wananchi walivyokuwa wakipendekeza serikali
tatu katika Rasimu ya Kwanza na ya Pili naye akawa anaafiki,
inashangaza amegeuka na kukataa maoni ya wengi,” alisema Profesa
Lipumba.
Mtikila akumbushia jela
Mwenyekiti
wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila alisema aliwahi kufungwa jela mara
tatu, kuwekwa mahabusu mara 43 kwa kudai lipatikane Taifa la Tanganyika
huku watawala wakikataa matakwa ya wengi kwa sababu na hoja dhaifu.
Mchungaji
Mtikila aliongeza kusema kwamba wanachokitaka CCM na Serikali zake ni
kuendelea kuwabana wananchi wa Tanganyika na Zanzibar wasiweze kuwa huru
na kujivunia mataifa yao.
Seif: Mimi Ukawa damu
Akihutubia
mkutano huo, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad alieleza
msimamo wake kuwa anaunga mkono harakati hizo na yeye ni Ukawa damudamu.
“Walikuwa hawajui msimamo wangu, waelewe kwamba mimi ni Ukawa damu,” alisema.
Seif
ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alisema wanaotetea
mfumo wa serikali mbili ni sawa na watu wanaopigania kuendelea kuwapo
kwa dhuluma Tanzania.
“Hatuwezi
kuendelea na mfumo huu, tumekuwa tukipiga kelele kwamba Muungano huu wa
serikali mbili umeteka mamlaka yetu,” alisema Maalim Seif. Alimtaka
Rais Kikwete asiwatishe wananchi kwa sababu wamependekeza mfumo mpya wa
serikali... “Unaposema kwamba jeshi litapindua nchi kama tukiwa na
Muungano wa serikali tatu, unamaanisha nini kama Amiri Jeshi Mkuu?”
alihoji Maalim.
Katika
mkutano huo, ulinzi uliimarishwa vya kutosha huku magari ya FFU na
vikosi vya SMZ yakiwa yameegeshwa pembeni na askari waliokuwa wamebeba
silaha na mabomu viunoni wakilinda. (CHANZO: MWANANCHI) (FS)
Post a Comment