MJUMBE
wa Bunge Maalumu la Katiba, Kabwe Zitto amesema muundo wowote wa
serikali uwe serikali moja, mbili au tatu unaweza kuvunja Muungano ikiwa
hakutakuwa na muafaka wa pande zote mbili za Muungano.
Zitto
alisema hayo jana bungeni wakati akichangia hoja za Kamati za Bunge
Maalumu namba moja hadi 12, juu ya Sura ya Kwanza na Sura ya Sita ya
Rasimu ya Katiba na kuwataka wajumbe wa Bunge hilo kujadili hoja badala
ya kutoa lugha za matusi.
“Mchakato
huu tuufanye kwa kujadiliana kwa hoja, tusitukanane, muundo wowote wa
serikali unaweza kuvunja Muungano, kikubwa ni kuafikiana maridhiano
kutoka pande zote mbili za Muungano”, alisema Zitto.
Zitto
ambaye hakusema anaunga mkono muundo upi wa Serikali, alisema jambo la
msingi linalopaswa kufanywa na wajumbe wa Bunge hilo ni kufikia
maridhiano ya pande mbili na sio kuendeleza ubaguzi na chuki ambavyo
vimeanza kutawala miongoni mwa michango ya wajumbe wa Bunge hilo.
Kuhusu
muundo wa Serikali, Zitto alisema ni vyema wajumbe wafikirie zaidi na
kujifunza kutoka kwa nchi kama vile Somali, ambayo ilikuwa na muundo wa
serikali moja lakini kwa kutoelewana ilivunjika na sasa hali sio nzuri
nchini humo.
Kadhalika
alitoa mfano mwingine wa Malaysia na kusema kama wajumbe wanataka
serikali ya shirikisho, nchi hiyo ilikuwa na muundo huo, lakini kwa
kutoelewana kwao ilivunjika na hadi sasa hakuna tafiti zilizothibitisha
ni muundo upi wa serikali unaweza kulinda serikali isivunjike.
Alifafanua
kuwa kinachoweza kulinda serikali ni kuwa na maridhiano ya pande
zinazohusika na kwamba kama suala ni gharama za kuendesha serikali,
ikiwa serikali itakusanya kodi ipasavyo, nchi itaendeshwa vizuri.
“Tuna
uwezo wa kuendesha serikali za idadi yoyote ile, kwa kukusanya kodi,
hiyo hofu ya kuendesha serikali ya Muungano kwa kutokuwa na fedha ni
jambo la ukweli, lakini tunaweza kuboresha hizo hoja, ndiyo maana
tumekuja, kama hatuwezi tumekuja kufanya nini hapa?” Alihoji Zitto.
Katika
hatua nyingine Zitto alisema ikiwa itaundwa serikali isiyo na
maridhiano ya pande zote mbili za Muungano, gharama ya kuulinda Muungano
huo ni kubwa kuliko uwepo wa kuwa na serikali tatu.
“Lazima
tuwe na Muungano unaoeleweka, tuepuke lugha za matusi, chuki, ubaguzi,
tunaelewa historia ya nchi yetu tubakie na Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania,” alisema Zitto.
Naye
mjumbe wa Bunge hilo kutoka Zanzibar, Issa Gafu alisema baadhi ya
wajumbe wanaotaka Muungano uvunjike ni wachache ambao walikana uhuru wao
wa mwaka 1964 na kamwe hawawezi kukubali Muungano.
“Hivi
kama wewe uliukana uhuru wako mwaka 1964, utawezaje kukubali Muungano?
Zanzibar inasumbuliwa na masuala ya uchumi na sio idadi ngapi za
serikali,” alisema Gafu.
Akisisitiza
hoja hiyo Gafu alisema, kama Zanzibar watatumia fursa zilizopo vizuri
kwenye muundo wa serikali mbili wataendelea, lakini kudai muundo wa
serikali tatu sio kwa manufaa bali ni kutaka kuvunja Muungano.
Akichangia
hoja hiyo, mjumbe mwingine kutoka Zanzibar, Waziri Rajab Salum alisema
mfumo wa serikali mbili ndio wenye manufaa kwa pande zote mbili na
kwamba mitafaruku iliyopo Zanzibar haijaanza leo, bali ni wapinzani wa
Muungano wa mwaka 1964.
Post a Comment