Chumba cha maabara
********
Wakati
sekta ya afya ikikabiliwa na upungufu wa wataalamu, Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii, imesitisha ajira za wataalamu 204 wa maabara
walioajiriwa mwishoni mwa mwaka jana kwa madai kuwa hawana vigezo vya
kufanya kazi katika maabara za binadamu.
Watalamu
hao waliohitimu kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) pamoja na
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wamefanya kazi kwa kipindi
kisichozidi miezi sita kabla ya ajira zao kusitishwa.
Habari
zilizopatikana zinaeleza kuwa kikao cha kusitisha ajira za vijana hao
kilifanyika Januari, kati ya wizara na wawakilishi kutoka Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma.(P.T)
Serikali
ilieleza wataalamu hao hawana sifa za kisheria za kuwawezesha kusajiliwa
au kupata leseni ya Baraza la Wataalamu wa Maabara wa Afya nchini, bali
wanatambulika kwa uwezo wao wa kufanya utafiti wa kisayansi katika
maeneo husika.
Baada ya
kikao hicho, Kaimu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Donan Mmbando alitoa
agizo kwa waajiri wote nchini ambao ni makatibu wakuu, makatibu tawala
wa mikoa na wakurugenzi wa halmashauri za jiji, manispaa na wilaya kote
Tanzania Bara kufuta ajira hizo za maofisa wa teknolojia Daraja la II.
"Kwa
mujibu wa waraka huu, wanaostahili kuajiriwa kama wateknolojia daraja la
II ni wenye shahada ya sayansi katika mojawapo ya fani za maabara,
radiolojia, macho, viungo bandia, meno na dawa kutoka chuo
kinachotambuliwa na Serikali na kusajiliwa na mabaraza ya taaluma,"
inaeleza sehemu ya waraka hiyo ya Dk Mmbando.
Msemaji
wa Wizara ya Afya, Nsachris Mwamaja, alisema kuwa hakuna mabadiliko
yoyote yanayoweza kufanywa baada ya maamuzi yaliyofikiwa na kikao cha
Januari.
Wataalamu
Profesa
Joshua Malago kutoka Sua anasema kuwa katika kikao hicho ilibainika kuwa
kuna kozi mbili ambazo hazifundishwi katika vyuo hivi viwili na kwamba
ndivyo vilivyowanyima wahitimu wao leseni kutoka bodi husika.
"Elimu ya
wahitimu wetu iko juu sana kuliko hata wanaozalishwa katika vyuo
vingine wanavyovitambua, changamoto pekee ni 'patient handling na
anatomy'. Lakini tumekubaliana tuziongeze. Ni kozi rahisi kuliko ambazo
tumewafundisha na zinaweza zikafundishwa ndani ya wiki mbili au tatu
kama utaratibu utaandaliwa wa kuwapa 'on job training," anasema Profesa
Malago.
Malago
anaongeza kuwa taarifa walizozipata kutoka kwa wahitimu wao waliokuja
kujiendeleza wakiwa wametoka kazini zinaeleza kuwa hawajakubaliwa na
bodi za taaluma zao kusajiri vyeti vyao vya shahada.
"Wanatambulika kuwa na stashahada hata baada ya kupata shahada yetu ambayo inatambulika kimataifa," anaeleza Profesa Malago.
Chanzo:Mwananchi
Post a Comment