![](http://www.mwananchi.co.tz/image/view/-/2369080/highRes/777606/-/maxw/600/-/14fcbp8z/-/lowassa.jpg)
Waziri Mkuu wa zamani na mbunge wa Monduli, Edward Lowassa akizungumza
wakati wa mahojiano na waandishi wa gazeti hili mjini Dodoma. Picha na
Edwin Mjwahuzi
**********
Yafuatayo ni mahojiano ya Mwananchi na Waziri Mkuu wa
zamani Edward Lowassa. Hata hivyo Lowassa hakuwa tayari kuzungumzia
masuala yanayohusu uchaguzi mkuu ujayo na mambo yanayohusiana na hilo
kwa sababu anatumikia adhabu ya kusimamishwa mwaka moja na Kamati Kuu ya
Chama cha Mapinduzi (CCM).
Swali: Umekuwa ukisema mara kwa
mara kuwa tatizo la ajira ni bomu linalosubiri kupasuka, je serikali
ifanye nini kukabiliana na tatizo hilo?
Lowassa: Duniani kote vyama vya
siasa vinapotaka kuingia madarakani huangalia masilahi ya watu,
huangalia ni jambo gani la msingi ambalo chama kikiingia madarakani
kitayafanya. Suala la ajira lipo karibu katika kila nchi, kila chama
kinachoingia madarakani hulizungumza hilo.
Labda niseme mfano mmoja, Mwalimu (Julius) Nyerere
alipokuwa anaanzisha elimu ya kujitegemea mwaka 1967 alikuwa anaangalia
ajira. Aliangalia akaona hatuna viwanda, kwa hiyo elimu ikawa lazima
iwe ya kujitegemea. Unamuandaa mwanafunzi kwa maisha ambayo yatamuajiri
vijijini. Mwaka 1967, Mwalimu Nyerere alikuja na elimu ya kujitegemea,
kwa hiyo ni lazima na sisi tuje na mawazo mapya ya ajira. Kwanza hakuna
ubishi kwamba watu wanaomaliza darasa la saba, kidato cha nne, kidato
cha sita, vyuo, vyuo vikuu na kadhalika ni wengi sana. Watu wote hawa
wanaangalia kwamba wanafanyiwa nini katika ajira.
Kwa hiyo mimi sisemi tu ni bomu, ila nasema ni
bomu linalotarajia kulipuka wakati wowote. Lakini ni bomu ambalo
tunahitaji kulishughulikia. Lengo langu la kupiga kelele ni kuitaka
jamii ishughulikie jambo hili. Nashukuru nilipopiga kelele kidogo,
wizara zilitoa takwimu na kila wizara ikatakiwa kuangalia kwenye eneo
lake inatengeneza ajira kiasi gani, mimi nasema huo ndiyo mchakato.
Lakini kwa maoni yangu, ajira ya Tanzania lazima
iangalie kwenye eneo kubwa la kilimo. Kilimo ndicho kinachochukua ajira
ya watu wengi nchini. Lakini sasa tukiwapeleka vijana kwenye kilimo
tutengeneze mazingira ya kumfanya mwanafunzi anayemaliza chuo kikuu awe
tayari kuishi mazingira ya kilimo.
Nilipokuwa Waziri wa Maji nilitembelea Misri, kule
mwanafunzi anapomaliza chuo kikuu anapelekwa Mto Nile anapewa ekari
tatu za kulima mizabibu, anapewa trekta na vyombo vingine na anapewa
mkopo ambao ataanza kuulipa baada ya miaka mitatu.
Pia tangu akiwa chuo, anajua ajira yake ni kilimo
na kwamba atapewa mazingira ya kufanya kilimo; si cha jembe la mkono ila
kilimo cha kisasa. Anakopeshwa na anawezeshwa. Kwa hiyo mimi nasema
jambo moja kubwa sana la kufanya ni kuhakikisha tunawapeleka vijana
kwenye kilimo, lakini kilimo chenye mabadiliko. Kilimo ambacho ni cha
kisasa zaidi ambacho atakifurahia na ambacho kitamletea maisha bora
katika maisha yake.
Eneo jingine mimi nadhani tungefanya uamuzi magumu ni kutenga maeneo tukapanda michikikichi (mawese), kama ilivyo Kigoma.
Tuchukue ekari kama milioni 10 tupande
michikikichi, michikichi hii tuigawe. Kwa mfano tungeweza kufanya kazi
ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), iwe ni kuhakikisha wanaanzisha mashamba
ya michikichi. Mkishaanzisha mashamba ya michikichi, mnawakabidhi
vijana ambao hawana ajira waendelee na michikichi na baada ya miaka
mitatu au minne watakuwa wamevuna, hali yao itakuwa nzuri na utakuwa na
mafuta ya chakula nchini, tutakuwa na mafuta ya ku-export (kuuza nje) na
utakuwa umetengeneza ajira kwa vijana wengi.
Vilevile la tatu ni eneo kubwa ambalo linategemewa
na watu; ni viwanda. Na mtakumbuka wakati (Rais wa Marekani, Barack)
Obama anagombea urais kwa mara ya pili wale wafanyakazi wa General
Motors (kiwanda kikubwa cha magari Marekani) waliandika bango ‘You saved
our jobs in September, this year we will save your job in November
(Uliokoa ajira yetu Septemba nasi tutaokoa ajira yako Novemba)
wakimkumbuka alivyofanya uamuzi ambao si wa kibepari; ulikuwa ni wa
kijamaa, kwamba serikali inawekeza kwenye viwanda.
Kwa siasa za kibepari jambo hilo halipo, lakini
serikali ililazimika kuwekeza kwenye viwanda ili ajira ziendelee na
viwanda viendelee. Sasa mimi nasema tunaweza na sisi tukajenga viwanda
makusudi vya nguo ambavyo vinachukua ajira ya watu wengi au viwanda
vingine tutakavyoona vinafaa vinavyochukua ajira ya watu wengi.
Post a Comment