Mama Diamond akilia kwa furaha.
STAA wa
muziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’ amefanya tukio la
kihistoria kiasi cha kumliza mama yake mzazi, Sanura Kassim ambaye
alimwaga machozi kama mtoto mbele za watu.
Tukio la
mama Diamond kumwaga machozi lilishuhudiwa na kamera za Amani, juzi
Jumatatu, mishale ya saa mbili usiku nyumbani kwake, Sinza jijini Dar es
Salaam ambako kulikuwa na ‘bethidei’ ya mama huyo.
Waalikwa
na mama huyo, wote walijua kuwa shughuli ilikuwa ni futari lakini kumbe
nyuma ya pazia kulikuwa na tukio la kumbukumbu ya kuzaliwa kwa mama huyo
ambayo inadaiwa alikuwa hakumbuki.
Mmoja wa rafiki wa karibu na familia hiyo, kwa sharti la kutotajwa
jina lake gazetini, alisema kuwa hadi jioni, mama Diamond hakuwa
akifahamu kuwa aliandaliwa sherehe ya siku yake ya kuzaliwa.
“Mipango
yote ilifanywa kwa siri mama Diamond hakujua kilichoendelea. Diamond
akiwa Marekani alitoa maelekezo mama yake afanyiwe shughuli hiyo hata
kama hayupo kwa sababu siku ya kuzaliwa haijirudii,” alisema rafiki
huyo.
KILICHOMLIZA
Muda mfupi baada ya shughuli ya kufuturu kukamilika, mama Diamond
alishangaa kusikia kwamba kulikuwa na jambo jingine la ziada katika siku
hiyo. Alitolewa nje huku akiimbiwa ‘happy birthday’ ndipo alipogundua
kilichokuwa kikiendelea.
Mara
baada ya shampeni isiyo na kilevi kufunguliwa na waalikwa kupewa, meneja
wa Diamond, Babu Tale na wapambe wengine walimuongoza mama huyo hadi
kwenye gari aina ya Toyota Lexus Harrier na kuelezwa kuwa ni mali yake
kuanzia muda huo tamko lililomshtua na kuanza kulia akiwa haamini
alichosikia!Mama Diamond akilia huku kichwa kikiwa juu ya gari aliyopewa zawadi na mwanaye.
“Siamini
macho yangu, siamini... asante sana mwanangu (Diamond), nakuombea kila
kukicha mwanangu uwe na afya njema, unilee kwa upendo, asante Mungu,”
alisikika mama Diamond akitamka kwa sauti iliyoambatana na kilio cha
nguvu.
Muda huohuo akafunguliwa mlango na kuingia ndani ya gari hilo lililopambwa ndani kwa vitu kibao vya thamani.
WEMA, AUNT WAMBEMBELEZA
Machozi ya mama Diamond hayakukoma hata baada ya kushuka ndani ya
gari, alionekana kuchanganyikiwa kama siyo kutoamini sapraizi ya
mwanaye, ndipo Miss Tanzania 2006, aliye pia mchumba wa mwanaye, Wema
Sepetu na staa wa filamu za Bongo, Aunt Ezekiel walipovaa jukumu la
kumtuliza.
Mastaa hao
ambao ni mtu na shogaye, walimchukua mwanamke huyo na kwenda naye
pembeni ambako walimsihi atulie na akubaliane na alichokiona kwani ndiyo
ukweli wenyewe.
Juhudi zao zilizaa matunda, kwani muda mfupi baadaye mama Diamond
alifuta machozi na kurudi katika hali yake ya kawaida ingawa alishindwa
kuficha furaha yake.
DIAMOND, WEMA NDOA LAZIMA!
Katika kuonesha kuwa sasa amekubali kwa dhati Wema awe mkwewe, mama
Diamond aliapa lazima ahakikishe mwanaye anafunga ndoa na mlimbwende
huyo.
“Hilo nataka
mlijue kabisa. Nitafanya juu chini Diamond amuoe Wema maana ana roho
nzuri sana. Niseme ukweli kuwa huyu msichana ndiye chaguo langu na
wanaendana sana na mwanangu.
“Angalia wakiwa pamoja, mwanangu anapata mafanikio makubwa sana,
nadhani nyota zao zinaendana hivyo sina pingamizi lolote. Ninachotaka ni
kuhakikisha wanaoana,” alisema mama Diamond.
THAMANI YA GARI
Akizungumzia thamani ya gari hilo, Babu Tale alisema ni shilingi
34,000,000 (milioni 34) ikiwa ni pamoja na mazagazaga mengine baada ya
gari hilo kununuliwa.
“Hiyo milioni 34 ni pamoja na muziki unaouona ndani ya gari, hizi
skrini tatu na mazagazaga mengine kama mnavyoona,” alisema Babu Tale
huku akiwaonesha waandishi wetu.
DIAMOND BONGO
Hadi tunakwenda mitamboni, Jumanne usiku, ilielezwa kuwa, Diamond
alitarajiwa kutua jana Jumatano katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere (JNIA) akitokea Marekani alipokuwa kwenye kinyang’anyiro
cha Tuzo za BET.
Habari
kutoka ndani ya familia zilieleza kuwa, nyota huyo naye ameandaliwa
sapraizi ya nguvu kutoka kwa kampani yake wakishirikiana na familia.
“Wamejiandaa vya kutosha kumfanyia saprazi ya nguvu na yeye mara tu
atakapotua Bongo. Wanafanya siri sana, haijajulikana atafanyiwa nini,”
kilipasha chanzo chetu.
DIAMOND ANATISHA
Nyota ya Diamond imeonekana ikiwaka sana siku za hivi karibuni ambapo
amekuwa akipiga shoo za mara kwa mara katika nchi mbalimbali huku
akishirikishwa kwenye tuzo za ndani na za kimataifa.
Si jambo la ajabu kusema kuwa, Diamond kwa sasa ndiye Mwanabongo
Fleva anayefanya vizuri zaidi pengine kuliko wote katika muziki huo –
MHARIRI.
on Thursday, July 10, 2014
Post a Comment