Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

KISA CHA MTOTO WA YUSUPH MAKAMBA KUMKASILISHA KATIBU MKUU WA CCM ABDULRAHMAN KINANA NDIYO HIKI

 


 
KITENDO cha kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), January Makamba, kutangaza nia ya kugombea urais kimekera vigogo wengi wa chama hicho akiwamo Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana (pichani), imefahamika.

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vilivyo karibu na Kinana, kauli ya Makamba ambaye ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, ni sawa na kukiuka onyo alilopewa la kutofanya kampeni za urais kabla ya wakati.

Vyanzo vyetu vya taarifa vinasema kwamba kwa jinsi Makamba alivyotoa tamko hilo akiwa nje ya nchi, tena kwenye chombo kikubwa, katika mahojiano na Shirika la Habari la Uingereza (BBC), ni wazi alikuwa anajifanyia kampeni kabla ya wakati.

Kinana anasemekana kukasirishwa na kauli ya Makamba, huku baadhi ya makada wakisema kuwa amedharau mamlaka za chama zilizomzuia yeye na wenzake watano kufanya kampeni.

Taarifa hizo zinasema Kinana na wenzake wanadhamiria kumuita Makamba atakaporejea ili ajieleze kwanini anapuuza onyo la chama; maana wasipofanya hivyo atajitokeza kada mwingine ajitangaze, na hivyo kuibua upya suala lililozimwa, kwani wakati wa kutangaza waziwazi nia hiyo bado haujawadia.

Tangu Makamba alipotangaza nia yake hadharani wiki iliyopita, yametolewa matamko kadhaa kutoka kwa makada wa CCM, baadhi yao wakimpinga na wengine kumuunga mkono.

Mbali na wasomi na wanasiasa kadhaa kudai hoja ya Makamba ya kutaka wazee wasiingie kwenye kinyang’anyiro hicho akidai awamu ijayo ni ya vijana kuwa haina mashiko, CCM Mkoa wa Shinyanga imedai ni mbaguzi.

Kwa mujibu taarifa ya Katibu Mwenezi wa Wilaya ya Shinyanga Mjini, Charles Shigino, kauli ya Makamba inaleta ubaguzi ndani ya chama na kwamba ni ya kuwatusi wazee.

Katibu huyo alidai kuwa Makamba ana uzoefu mdogo wa uongozi ndani ya CCM, na kwamba kwa nafasi ya urais anapaswa kupata uzoefu na ushauri wa wazee ambao anawabagua na hivyo kuleta mpasuko.

Hata hivyo, baadhi ya washindani wa Makamba katika suala hili wanadai kwamba amewarahisishia kazi, maana asipochukuliwa hatua kali nao wanaweza kujitangaza rasmi au kufanya mambo yoyote yatakayowasaidia kusikika na kujadiliwa kama inavyotokea kwake sasa.

Mbali na Makamba, makada wengine waliofungiwa na Kamati ya Maadili ya CCM Februari mwaka huu, kwa madai ya kuanza kampeni za urais mapema, ni Edward Lowassa, Fredrick Sumaye, Stephen Wassira, Bernard Membe na William Ngeleja.

Dk. Khamis Kigwangala ambaye ni mmoja wa wanaotajwa kuitaka nafasi hiyo, aliliambia gazeti hili kuwa suala la urais bado hajaweka wazi, ingawa watu wengi wameshauri aingie kwenye kinyang’anyiro.

“Si kwamba najiona siwezi wala sioni kwamba ni jambo zito. Urais unahitaji kuwa na nguvu, uwezo, kuchukia rushwa, uvivu na uzembe, kuwa na nidhamu ya kazi, kuchukia matanuzi ya serikali.

“Nikijipima katika hayo nikaona nafaa, nadhani wakati wowote nitatangaza nia ila kwa sasa natafakari. Wakati muafaka kabla ya Septemba nitatangaza nia ya kugombea urais,” alisema.

Edward Lowassa, kupitia kwa msemaji wake, Aboubakary Liongo aliliambia Tanzania Daima kwa simu kuwa; “Mzee yupo kimya, no comment (hakuna maoni), anatumikia vema adhabu yake ukifika wakati atasema kitu”.

Samuel Sitta alisema suala la urais bado, kwamba anahangaika na suala la Bunge Maalumu la Katiba.

Alisema kuwa amewasikia wenzake wanaotangaza nia, na kwamba amewashangaa, lakini akadai acha waendelee kuhangaika.

CCM iliwaonya makada wake sita na kuwazuia kugombea uongozi wowote ndani ya chama kwa muda wa mwaka mmoja.

Katibu Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema baada ya kuhojiwa wote walithibitika kuanza kampeni za kutafuta kuteuliwa kugombea urais kabla ya wakati, jambo ambalo ni kinyume na kanuni za uongozi na maadili za CCM Toleo la Februari 2010, Ibara 6(7)(i).

Alisema kwa tafsiri ya adhabu ya onyo kali kwa mujibu wa Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM Toleo la Februari 2010, Ibara ya 8(ii) (b) ni; “Mwanachama aliyepewa adhabu hiyo atakuwa katika hali ya kuchunguzwa kwa muda usiopungua miezi 12, ili kumsaidia katika jitihada zake za kujirekebisha.”

Kujitangaza kwa Makamba kunaelezwa na wachambuzi wa kisiasa kwamba kutaibua mzozo tena, hasa wakati huu ambapo anaendelea kutumikia adhabu aliyopewa na chama.TANZANIA DAIMA.
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top