WANANCHI wa Kata ya Kambasegela wilayani Rungwe mkoani hapa,
wamewafukuza viongozi wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM wa kata hiyo
walipotaka kufanya mkutano wa hadhara ili kuimarisha chama chao.
Akizungumza mwishoni mwa wiki katika ziara ya Mwenyekiti wa Jumuiya
ya Wazazi Mkoa wa Mbeya, Fatuma Kasenga, Katibu wa jumuiya hiyo Kata ya
Kambasegela, Frank Mwansasu, alisema wananchi walimtimua yeye na
msafara wake kwa madai kwamba waliahidiwa maji zaidi ya miaka kumi sasa
bila kupatiwa.
“Mwenyekiti, kero yangu kubwa ni kwamba, mimi na wenzangu tulifukuzwa
na wananchi tusifanye mkutano wa hadhara wakati wa ziara yetu ya kata,
wananchi wanasema waliahidiwa maji, lakini hawajapelekewa mpaka hivi
sasa,” alisema Mwansasu.
Akijibu kero hiyo, Mwenyekiti Kasenga, alisema hayo ni matokeo ya baadhi ya viongozi kutowajibika vema katika nafasi zao.
Alisema suala hilo limemsikitisha, na kwamba yeye na msafara wake
watalifikisha kwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Godfrey Zambi, ili
kulipatia ufumbuzi.
Akiwa katika ziara hiyo, mwenyekiti huyo alipokea kero nyingine kwa
baadhi ya wananchi wa Kata ya Nkunga, ambao walimwambia kuwa chama
hicho kinachukiwa kwa udhaifu wa baadhi ya viongozi wake.
Wananchi walisema kata hiyo ina uhitaji wa umeme, na kwamba katika
Kijiji cha Ibililo, kuna msigano wa viongozi, jambo ambalo
linasababisha kutopatikana kwa maendeleo ya kijiji.
“Jitokezeni kwenye marekebisho ya daftari la kudumu la mpiga kura na
ukifika wakati wa uchaguzi, wazee, vijana na wanawake wanaofaa wapeni
nafasi wagombee,” alisema Kasenga.
Post a Comment