Mkazi wa Singida Mjini, Jacqueline Kweka (30) jana alipandishwa
mahakamani mjini Hai akikabiliwa na tuhuma za kumfanyia ukatili
mfanyakazi wake wa ndani (15).
Inadaiwa kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa akimpiga
mfanyakazi wake huyo sehemu mbalimbali za mwili ikiwamo kumvuta nyama za
sehemu za siri kwa kutumia bisibisi.
Baada ya tuhuma hizo kuibuliwa na raia wema,
mtuhumiwa huyo alitoroka kutoka Singida na kukimbilia kijiji cha Narumu
wilayani Hai, Kilimanjaro alikokamatwa baada ya taarifa kuvuja.
Mtuhumiwa huyo alifikishwa mahakamani mbele ya
Hakimu Mkazi, Mfawidhi wa Wilaya, Denis Mpelembwa na kukanusha mashitaka
dhidi yake. Hati ya mashtaka hayo ya kujeruhi mfanyakazi wake huyo ni
ya awali ili kuruhusu polisi kutoka Singida kwenda kumchukua mtuhumiwa
huyo.
Akimsomea mashitaka, Mwendesha Mashitaka wa
Polisi, Inspekta Marwa Mwita alidai mtuhumiwa huyo alitenda makosa hayo
Julai mwaka huu siku tofauti.
Mtuhumiwa huyo alikanusha mashitaka hayo na
amerudishwa rumande hadi Agosti 21 wakati ukisubiriwa utaratibu wa
kumsafirisha kwenda Singida.
Msichana anayedaiwa kufanyiwa ukatili huo,
amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Hai kwa matibabu na taarifa
zinadai amepoteza uwezo wa kusikia na hapati tena siku zake za hedhi na
amelazwa hapo kwa wiki ya pili sasa.
Hivi karibuni matukio ya kunyanyasa wafanyakazi wa
ndani yamezidi kushika kasi likiwamo lile la msichana, Yusta Lucas (20)
anayedaiwa kuteswa kwa kung’atwa na kuchomwa kwa pasi mwili mzima na
mwajiri wake Amina Maige, mkazi wa Mwananyamala jijini Dar es Salaam.
Mwanamke huyo ameshtakiwa kwa kosa la kumjeruhi
mfanyakazi wake huyo kwa kumng’ata sehemu mbalimbali za mwili na
kumsababishia majeraha makubwa.
Kesi hiyo ambayo imeendelea kuvuta hisia za watu
wengi kila iitwapo, inaendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Wilaya ya
Kinondoni mkoani Dar es Salaam.
Baadhi ya watu wanaozungumzia unyanyasaji wa aina hiyo, wanataka upigwe vita na jamii.
Post a Comment