JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
BUNGE MAALUM
BUNGE MAALUM LA KATIBA LIPEWE NAFASI YA KUFANYA KAZI ZAKE
Ofisi
ya Bunge Maalum, imeshangazwa na kusikitishwa na baadhi ya vyombo vya
habari na makundi ya jamii yanayoeneza upotoshwaji mkubwa ambao umedakwa
katika mitandao ya kijamii kuhusu kauli aliyoitoa Mwenyekiti wa Bunge
Maalum Mhe. Samuel Sitta (Mb) wakati wa mjadala wa kupitisha Kanuni
tarehe 5 Agosti, 2014 kuhusu midahalo ya Katiba inayoendelea katika
baadhi ya televisheni hapa Nchini.
Mwenyekiti
wa Bunge Maalum, Mhe. Sitta hapo tarehe 5 Agosti 2014 alitahadharisha
kuhusu baadhi ya midahalo hiyo inayoendeshwa ikiwa na mapungufu makubwa.
Wanapangwa washiriki wenye mawazo na malengo ya upande mmoja na kutumia
fursa hiyo kushambulia kwa lugha chafu makundi yenye mawazo tofauti
ambayo kimsingi yalitakiwa yashirikishwe kwenye midahalo hiyo.
Tumeshuhudia upotoshwaji mkubwa kuhusu kauli ya Mwenyekiti. Hali hii
inadhihirisha jinsi maadili ya upashanaji habari yanavyotumiwa vibaya na
baadhi ya vyombo vya habari na baadhi ya makundi katika jamii.
Ifahamike
wazi kuwa lengo la Mhe. Mwenyekiti lilikuwa ni kuwakumbusha wahusika na
waandaji wa midahalo hii pamoja na Serikali kuwa utaratibu huu wa
kualika kundi moja lenye mrengo mmoja na kuuita mkutano huo ni mdahalo
si sahihi. Mdahalo kwa tafsiri yake, hauna budi kuwa na pande mbili au
zaidi. Utaratibu wa uaandaji wa midahalo kote ulimwenguni msingi wake ni
kutoa fursa kwa wasikilizaji/watazamaji kusikiliza pande zote zenye
mawazo tofauti na kuwaachia wananchi kuchambua mawazo hayo na kuona yepi
wayakubali au kuyakataa.
Inasikitisha
pale ambapo baadhi ya watu wameamua kuitumia kauli ya Mwenyekiti, Mhe.
Sitta kwa kupotosha umma na kujikita katika kuzua malumbano yasiyo na
tija kwa Taifa hususan katika kipindi hiki ambacho wananchi wangependa
kufuatilia mijadala kuhusu Katiba.
Baadhi
ya vyombo vya habari, kwa makusudi vimeamua kubeba agenda tofauti na
kuangukia katika mtego wa kuchochea uhasama. Matoleo yao wamekuwa na
vichwa vya habari vilivyosomeka “Sitta Avaa Udikteta”, Bunge lataka kina Warioba wadhibitiwe”, Sitta avunja nchi nk na
hatimaye upotoshwaji wa aina hii kuenezwa katika mitandao ya kijamii
ili kuuchafua mchakato wa Bunge Maalum kutunga Katiba na kumchafua
Mwenyekiti.
Ofisi
ya Bunge Maalum inasisitiza na kuvikumbusha vyombo vya habari
kuzingatia maadili ya upashanaji habari kwa uadilifu, hususan katika
kipindi hiki ambacho Nchi ipo katika mchakato ambao wananchi
wangestahili kupata taarifa sahihi kuhusu utungaji wa Katiba. Bunge
Maalum linakaribisha maoni ya wananchi yenye dhamira safi bila kuingiza
chuki binafsi, uchochezi na upotoshaji habari wa makusudi.
Bunge Maalum linatoa rai kwa wote kwamba liachwe litimize wajibu wake.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA KATIBU WA BUNGE MAALUM
7 Agosti, 2014
Post a Comment