Kijiko kikubomoa nyumba zinazodaiwa kumilikiwa
kinyume cha sheria na Mchungaji Getrude Rwakatare eneo la Kawe Beach
jijini Dar es Salaam jana. Kwa mujibu wa msimamiozi wa zoezi hilo,
Mhandisi Baraka Mkuye, kutoka Manispaa ya Kinondoni, zoezi hilo ni
utekelezaji wa amri ya Katibu Mkuu wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi, Aliphayo Kidata. PICHA: MPIGAPICHA WETU
*********
Imedaiwa kuwa Dk. Lwakatare alivamia kiwanja hicho kilichopo kitalu namba 314 Kawe Beach na kujenga nyumba hizo zinazokadiriwa kuwa na thamani ya Sh. milioni 200 kinyume na utartibu.
Amri ya kubomoa nyumba hizo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi na Maendeleo Makazi, Aliphayo Kidata na kusimamiwa na Mhandisi wa Manispaa ya Kinondoni, Baraka Mkuye.
Nyumba hizo zilivunjwa na katapila na kuzua taharuki baada ya magari ya Manispaa hiyo, Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi kuwasili yakiwa yameongozana na askari wa jeshi la polisi majira ya saa 5:30 asubuhi katika kiwanja hicho.
Baada ya kuwasili katika eneo hilo, askari wa polisi walitanda kuimarisha ulinzi hadi zilipovunjwa nyumba zote.
Kabla ya kuanza kwa uvunjwaji wa nyumba hizo, alijitokeza mtu aliyejitambulisha kuwa ni wakili wa Rwakatare kwa lengo la kutaka kuzuia zoezi hilo akidai wamefungua kesi mahakamani.
Juhudi zake hizo ziligongwa mwamba baada ya Mhandisi wa Manispaa huyo kukata kumsikiliza na kuamuru zoezi liendelee.
Mkuye alisema kuwa: “Natekeleza zoezi hili kwa amri ya Katibu Mkuu Wizara ambaye ndiye mtendaji mkuu, ”alisema Mkuye na kuongeza kuwa:
" Tulimwambia kabla ya kutekeleza amri akaona kwakuwa yeye ni mbunge na mtu mkubwa aendelee.... ajilaumu mwenyewe"
Alisema Mchungaji Lwakatare amekiuka zaidi ya makosa mawili, kwanza kujenga eneo ambalo si mali yake na kukosa vibali vya kujenga nyumba.
Kwa upande wake mmiliki wa kiwanda hicho, alisema alianza kukimiliki tangu miaka ya 80 na kupata hati ya ardhi mwaka 2010.
Alisema kabla ya Lwakatare kujenga nyumba hizo kwenye kiwanja chake hicho kulikuwa na nyumba ambayo ilikuwa bado inajengwa.
Alisema aliposafiri kwenda nje ya nchi alimuachia jirani yake awe mwangalizi wa kiwanja hicho ili kisivamiwe.
“Nikiwa nje nilipigiwa simu na jirani yangu kuwa kiwanja changu kimejengwa nyumba hivyo nilirudi Tanzania na kwenda polisi kufungua kesi ambayo mpaka sasa naambiwa iko kwa Mkurugenzi wa mashitaka.“
Alisema kutokana na polisi kumzungusha, aliamua kwenda wizarani na kugundua kulikuwa na mpango wa kubadilisha hati lakini walikwama kutokana na kuandikiwa jina lake.
Baadhi ya majirani walioshuhudia nyumba hizo zikibomolewa, waliipongeza Serikali kwa kutenda haki kwa wanyonge na kumrejeshea Janet kiwanja chake.
Wakili wa Janeth, Hawadi Msechu alidai kuwa kesi jalada la kesi hiyo halionyeshi kuwa mmiliki wa nyumba hizo ni mchungaji huyo bali ni mwanawe.
Alisema kwa upande wa wizara hiyo inatambua kuwa nyumba hizo ni mali ya Dk. Rwakatare kutokana nyaraka mbalimbali zikiwamo za kulipia huduma za maji taka na nyingine kuwa na jina lake.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment