Wananchi wenye hasira, wameteketeza kwa moto nyumba ya mkazi wa
Kijiji cha Mwika Uuwo, Wilaya ya Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro,
wakimtuhumu kulawiti wanaume wenzake.
Hasira za wananchi hao zilifikia kiwango
kisichohimilika baada ya mtuhumiwa huyo mwenye umri wa miaka 42, kudaiwa
kumlawiti mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 12 kijijini hapo juzi.
Wananchi wa kijiji hicho wanamtuhumu mwanamume
huyo ambaye jina lake tunalihifadhi kwa sasa kwa sababu za kitaaluma,
kuwa ana tabia ya kuwalawiti vijana kijijini hapo.
Habari kutoka kijijini hapo zilizothibitishwa na
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, zilisema kuwa mbali
na kuchoma moto nyumba hiyo, pia walifyeka ekari moja ya shamba la
migomba la mtuhumiwa huyo.
Kamanda Boaz alisema jana kuwa
tukio la kuchomwa moto kwa nyumba hiyo lilitokea saa 3:30 usiku na
ilipofika saa 6:00 usiku wa kuamkia jana, nyumba hiyo ilikuwa
imeteketea yote.
Kwa mujibu wa Kamanda Boaz, wakati wananchi
wakiiteketeza nyumba hiyo na kufyeka shamba lake la migomba, mtuhumiwa
huyo anayetafutwa na polisi hakuwepo ndani ya nyumba hiyo.
“Siyo jambo jema kuchukua sheria mkononi kwa
sababu huyu ametenda kosa halafu mnaokwenda kuchoma nyumba yake, nanyi
pia mnatenda kosa la jinai,”alisema Boaz.
“Kama walijua (wananchi) kuwa huyo mtuhumiwa amerudi na yuko ndani, wangemkamata na kumfikisha polisi siyo kuchoma nyumba. Nchi lazima iendeshwe kwa misingi ya kisheria,”alisisitiza.
Kamanda Boaz alisema kuwa juzi polisi walifika
kumtafuta mtuhumiwa huyo kwa lengo la kumkamata, lakini hawakuweza
kumpata na inadaiwa alikuwa amekimbilia mahali kusikojulikana.
Mwinjilisti mmoja wa Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT), aliyeshuhudia tukio la kuchomwa moto nyumba
hiyo, alisema familia ya mtuhumiwa imehifadhiwa kwa ndugu yake.
“Huyo bwana (mtuhumiwa) ni baba mwenye mke na
watoto sita na kabla ya kuichoma moto nyumba wananchi waliitaka familia
yake kuondoka kwenye nyumba,”alisema Mwinjilisti huyo.
Mwinjilisti huyo ambaye hakupenda jina lake liandikwe kwa kuwa siyo msemaji, alisema awali saa 1:00 usiku wananchi waliiwasha moto nyumba hiyo lakini wakatokea wasamaria wema wakauzima
Mwinjilisti huyo ambaye hakupenda jina lake liandikwe kwa kuwa siyo msemaji, alisema awali saa 1:00 usiku wananchi waliiwasha moto nyumba hiyo lakini wakatokea wasamaria wema wakauzima
Post a Comment