Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
(pichani) amesema kuwa Tanzania imeendelea kuwa nchi tulivu, yenye umoja
na yenye amani kwa sababu ya sera nzuri ambazo zilianzishwa na Baba wa
Taifa Mwalimu Nyerere na ambazo zimeendelezwa na viongozi wakuu ambao
walimfuatia Mwalimu.
Aidha, Rais
Kikwete amesema kuwa Tanzania imefanikiwa kudumisha umoja,mshikamano na
utulivu kwa sababu ya kuwa na sera zenye kujumuisha kila mmoja bila
kubagua Mtanzania yoyote kwa misingi ya kabila, dini, rangi,imani zake
na mahali atokapo.
Rais
Kikwete ametoa ufafanuzi huo, Ijumaa, Agosti 8, 2014, wakati
alipozungumza mjini Houston na taasisi ya ushauri na utafiti ya
Stratfor yenye makao makuu yake katika Jimbo la Texas, Marekani.
Akijibu swali kuhusu nini hasa siri ya utulivu, amani na ushikamano wa Watanzania, Rais Kikwete amesema:
“Tumekuwa na changamoto zetu nyingi kama taifa lakini tumekabiliana
nazo vizuri na nchi imebakia salama, tulivu na yenye umoja. Tumekuwa na
sera bora za kisiasa, kiuchumi na kijamii.Tumetunga sera za kumnufaisha
kila mtu bila kumbagua mtu yoyote kwa sababu zozote zile.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Sera
hizo zilianzishwa na Baba wa Taifa na sisi viongozi tuliofuatia
tumeziendeleza sera hizo. Hakuna ubaguzi wa rangi, ama kabila, ama dini,
ama sehemu atokapo mtu. Na ili kuhakikisha kuwa sera hizi zinaendelea
kuwa na maana tumefungua upeo na nafasi ya kisiasa.Tuna demokrasia
inayofanya kazi, Tuna uhuru wa kushirikiana na uhuru wa habari.”
Amesisitiza Rais Kikwete”
Kama wewe ni kiongozi ambaye amefungua milango ya demokrasia, huwaonei
watu wako wala kuwaua na kuwatesa, kama umefungua milango ya nchi kuwa
na utulivu kwa nini nchi isiwe na amani na utulivu.”
Rais
Kikwete pia ameishukuru Marekani kwa misaada yake mingi kwa Tanzania
ikiwemo misaada ya kupambana na ukimwi na malaria, ya ujenzi wa
miundombinu ya MCC, ya kilimo ya Feed the Future na Sacgot, uchapishaji wa vitabu vya kufundishia katika shule za sekondari.
“Sasa
tunaingia katika eneo jipya la biashara na uwekezaji kufuatia mkutano
wa Washington ambako viongozi wa Afrika walikutana na Rais Barack Obama
kuzungumzia aina mpya ya ushirikiano kati ya sehemu hizi mbili”.
Post a Comment