TAARIFA KWA UMMA KUHUSU KUCHUKUA TAHADHARI DHIDI YA UGONJWA WA EBOLA
Mnamo
mwezi wa Machi 2014 Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ilipokea taarifa
kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu ugonjwa wa Ebola katika nchi
za Afrika Magharibi ambao ulianzia katika ya Guinea na kusambaa katika
nchi za Siera Leone, Liberia na Nigeria. Hadi tarehe 31 Julai, 2014
idadi ya wagonjwa ilikuwa 1323 na vifo 729.
Ugonjwa
wa Ebola husababishwa na virusi vya Ebola. Dalili zake ni homa kali ya
ghafla, kulegea mwili, maumivu ya misuli, kuuma kichwa, na vidonda
kooni. Mara nyingi dalili hizo hufuatiwa na kutapika, kuharisha, vipele
vya ngozi, figo na ini kushindwa kufanya kazi na kwa baadhi ya wagonjwa
kutokwa damu ndani na nje mwilini. Kipindi cha kuonekana kwa dalili za
ugonjwa ni kati ya siku 2 hadi 21 baada ya kupata maambukizi.
Ugonjwa wa Ebola unaambukiza kwa kasi na unaenea kati ya mtu na mtu kwa:
o kugusa damu na majimaji kutoka mwilini mwa mtu aliyeambukizwa ugonjwa huo
o kugusa maiti wakati ya mtu aliyekufa kwa ugonjwa huu.
o kugusa wanyama walioambukizwa Mizoga na wazima kama vile sokwe na swala wa msitu.
Aidha Ugonjwa wa Ebola hauna tiba wala chanjo.
Hadi sasa hapa nchini Tanzania hakuna mgonjwa yoyote aliyehisiwa au kuthibitishwa kuwa virusi vya Ebola.
Wizara
ya Afya na ustawi wa Jamii imeandaa mikakati ya kuzuia ugojnwa huu
usiingie hapa nchini na ikiwa utaiingia uweze kudhibitiwa kabla
haujasambaa. Mikakati hiyo ni pamoja na:
o
Kuunda kikosi kazi (Task Force) kinachohusisha wajumbe mbalimbali
wakiwemo wadau wa maendeleo ikiwa ni pamoja na WHO, UNICEF, USAID na CDC
kwa ajili ya kuweka mikakati ya kukabiliana na ugonjwa huu ikwa ni
pamoja na kusimamia utekelezaji wa mpango wa dharura wa kukabiliana na
Ebola ambao tayari umeandaliwa.
o
Kutoa taarifa ya tahadhari ya ugonjwa huu kupitia kwa Makatibu Tawala
na Waganga Wakuu wote wa Mikoa. Aidha taarifa hii pia imejumuisha namna
mgonjwa anavyoweza kutambuliwa (Ainisho la Ugonjwa), “Fact sheet” ya
ugonjwa, Mwongozo kwa watumishi wa afya wa namna ya kuchukua sampuli, na
na namna ya kuwahudumia wagonjwa.
o
Kuboresha ufuatiliaji na utambuzi wa ugonjwa katika maeneo ya viwanja
vya ndege na mipakani ili kuweza kubaini wasafiri watakaoonyesha dalili
za ugonjwa au wenye viashiria hatari. .
o
Miongozo ya utoaji elimu imeandaliwa ikiwemo Vipeperushi. Aidha
watalaamu wa Afya wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu dalili za
ugonjwa huu kupitia vyombo mbalimbali vya habari ili endapo ugonjwa huo
ukitokea uweze kutolewa taarifa mapema
o
Vifaa kinga (Personal Protective Gears) vipo vya kutosha na Wizara
imeanza kuvisambaza kutoka bohari za kanda za MSD na kuzipeleka kwenye
vituo vya kutoa huduma za afya ili watumishi wa afya waweze kutumia
iwapo mgonjwa atajitokeza. Aidha idadi itaongezwa kadiri ya mahitaji
yatakavyojitokeza.
o
Wizara imebainisha vituo vya kutolea huduma kwa mikoa yote iwapo endapo
ugonjwa huu utatokea hapa nchini. Aidha katika vituo hivi, vifaa kinga
pamoja na madawa vimeshaandaliwa.
o
Kuwasiliana na wadau mbalimbali ikiwemo wadau wa maendeleo ili kuweza
kupata msaada wa mahitaji mbalimbali kama yalivyoainishwa kwenye mpango
wa dharura wa kukabliana na Ebola ulioandaliwa.
Hitimisho
Wananchi
wanashauriwa kutokuwa na hofu ila kuendelea kuchukua tahadhari za
kujikinga na ugonjwa huu. Ugonjwa wa Ebola unaweza kuzuilika. Njia kuu
za kujikinga na ugonjwa huu ni:-
o
Kuepuka kugusa au kuingiwa na mate, damu, mkojo, jasho, kinyesi,
machozi na majimaji mengine yanayotoka mwilini mwa mwenye dalili za
ugonjwa wa Ebola
o
Wananchi wanatahadharishwa kuepuka kushughulikia maiti ya mtu aliyekufa
akiwa na dalili za Ebola; badala yake watoe taarifa kwa uongozi wa
kituo cha huduma za Afya kwa ushauri.
o Wananchi waepuke mila na desturi zinazoweza kuchelewesha kupata huduma muhimu na kuzidi kueneza ugonjwa wa Ebola.
o Zingatia usafi wa mwili tabia na kiroho.
o
&bbsp; Kutoa taarifa mapema kwa viongozi wa Serikali na wa huduma
za Afya katika ngazi zote pale anapotokea mtu mwenye dalili za Ebola.
o Kuwahi katika vituo vya huduma za Afya pale mtu anapoona dalili za ugonjwa huu.
Wizara itaendelea kushirikiana na sekta mbalimbali kuimarisha ufuatiliaji ili kudhibiti ugonjwa huu usiingie nchini.
Post a Comment