Zaidi ya kaya 300 zenye wakazi zaidi ya 100 za Kawe Tanganyika Pecus jijini Dar es salaam hazina makazi baada ya kuvamiwa na kundi la watu waliotumwa na shirika la nyumba la taifa kuvunja nyumba zao bila taarifa zozote za kuwataka kuhama makazi hayo.
Wakazi hao wamelaani kitendo hicho na kuiomba serikali kuingilia kati zoezi linaloendelea la kuvunjwa kwa nyumba hizo ili kuwapa muda wa kufahamu hatma ya maisha yao.
Mwandishi alifika katika eneo hili na kushuhudia askari wa jeshi la polisi wakiimarisha ulinzi huku baadhi ya nyumba zikiwa zimevunjwa na baadhi ya wakazi wakiendelea kuhamisha vitu huku wengine wakipigwa na butwaa bila kujua nini cha kufanya ambapo wamesema wameshangazwa na kitendo hicho walichokiita cha kinyama baada ya mali zao kuharibiwa licha ya kukaa katika makazi hayo kwa zaidi ya miaka 50 na kuiomba serikali kuingilia kati.
Kufuatia tukio hilo Diwani wa kata hiyo amelazimika kufanya mkutano wa hadhara ambapo licha ya kukiri ubomoaji huo umekiuka taratibu, ameagiza wakazi hao kutulia na wale wote ambao hawajavunjiwa kutohamisha vitu hadi hapo utaratibu mwingine utakapotangazwa.
Mwakilishi wa shirika la nyumba la taifa Bw. Joshua Elius amekiri kundi lililovunja nyumba hizo liliagizwa na shirika hilo na kuwa utaratibu uliofanywa ni kuwalipa laki moja moja kama nauli wapangaji katika nyumba hizo na shilingi laki tano kwa waliokuwa wafanyakazi wa Tanganyika Pecuz na kuwa eneo hilo limekabidhiwa kwa shirika hilo ili kujengwa mji mpya utakaojulikana kama Kawe City.
Post a Comment