Na Benedict Liwenga, MAELEZO-Dodoma.
MJUMBE wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. George Simba
Chawene amesikitishwa na kauli zilizotolewa na baadhi ya Wajumbe walioko nje ya
bunge hilo kuhusiana na uhalali wa bunge hilo lililoko Kisheria.
Kauli hiyo ameitoa leo wakati akichangia mada katika
mjadala ndani ya bunge hilo huku akisisitiza kuwa huo ni upotoshwaji mkubwa na
watu hao wanapaswa kuangaliwa kuhusu uzalendo wao.
Mhe. Chawene ameeleza kuwa inasikitisha zaidi hasa
pale shutuma zinapoelekezwa kwa Mwenyekiti wa bunge hilo, Mhe. Samuel Sitta,
kuwa bunge hilo sasa linaonekana ni mali ya Mwenyekiti wa bunge hilo wakati si
kweli.“Gazeti linachukua kurasa tatu hadi nne kuzungumzia
habari Sitta king’ang’anizi, hivi hili bunge lipo kama liliitishwa na Sitta ama
na Rais wa nchi?, hili bunge liko kisheria”, alisema Mhe. Chawene.
Aliongeza kuwa kwa niaba ya Watanzania wanafanya kazi ya
bunge hilo kwa mujibu wa sheria huku akisisitiza kuwa wajumbe waliotoka nje ya
bunge hilo wamevunja sheria na kwamba hawawezi kutafuta uhalali nje ya sheria.“Wanamlazimisha Rais avunje bunge hili, Rais wa
kufuata utawala bora anavunja kwa mamlaka yapi? Mamlaka ya Rais yako kwa mujibu
wa sheria”, alisema Mhe. Chawene.
Aidha, ameeleza kuwa Sheria inayoendesha mchakato wa
Katiba ni Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo imetungwa kutoka katika Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenye hatua tatu zikiwemo hatua ya kukusanya
maoni ambayo Tume ya Warioba ilifanya kazi hiyo na kumaliza, hatua ya Pili ni
bunge hilo kujadili kwa niaba ya wananchi wa Tanzania kwa uwakilishi uliopo
ndani ya bunge hilo na hatua ya tatu ni wananchi kwenda kutunga Katiba.
“Sisi hapa tunatoa Katiba inayopendekezwa, inayofuata
ni Watanzania kwenda kutunga Katiba kwa kutunga kwa kupiga kura ya kusema ndiyo
au hapana yale tuliyoyajadili na kuletwa na Tume”, alisisitiza Mhe. Chawene.
Aidha, amewataka watanzania kuwaona watu hao kuwa ni
watu wabaya na wasio na nia nzuri na nchi na kuepuka kuingia barabarani kufanya
maandamano ya kuipinga Katiba hiyo.
Post a Comment