
Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Bw.
Morrice Oyuke (katikati) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ukuaji
wa Pato la Taifa kwa bei ya Soko leo jijini Dar es salaam. Wengine ni Bw. Fred
Matola, Mtakwimu Mkuu Takwimu za Uchumi (kushoto), Bi. Adella Ndesangia (wa
pili kutoka kulia) ambaye ni Mtwakimu Mkuu wa Ofisi hiyo na Bi. Jovitha
Rugemalila.
Na. Mwandishi Wetu- Dar es salaam
Sekta
za Kilimo,Viwanda, Biashara za jumla na rejareja zimetajwa kuongoza katika
kuchangia kukua kwa pato la Taifa kwa asilimia 6.9 katika kipindi cha robo ya
pili ya mwaka 2014.
Akitoa
taarifa ya kukua kwa pato la Taifa leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa
Takwimu za Uchumi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Bw. Morrice Oyuke amesema kuwa
kuanzia mwezi Aprili hadi Juni 2014 sekta hizo zimetoa mchango mkubwa wa kukuza
pato la Taifa.
Amesema
ukusanyaji wa taarifa kutoka vyanzo mbalimbali vya uzalishaji uliofanywa na
wataalam wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kuzingatia kanuni za kimataifa za kukokotoa pato la
Taifa unaonyesha kuwa jumla ya thamani
ya pato hilo imefikia kiasi cha shilingi trilioni 5.4 ikilinganishwa na
trilioni 5.0 za mwaka 2013.
Bw.
Oyuke amesema katika kipindi hicho
shughuli za kilimo cha mazao zimekua na kufikia asilimia 6.5 ikilinganishwa na
5.4 za mwaka uliopita huku mifugo
ikifikia asilimia 0.9, misitu na
uwindaji zikifikia asilimia 0.8,
shughuli za uvuvi zikikua kwa asilimia 2.1.
Ameongeza
shughuli za uchimbaji wa madini ya Almasi, Tanzanite, mawe, na kokoto
zimechangia kukua kwa pato la taifa kwa
kasi ya asilimia 3.0 katika kipindi hicho ikilinganishwa na asilimia 2.6 za
kipindi kilichopita.
Aidha,
amesema sekta ya uzalishaji wa bidhaa za viwandani imekua kwa asilimia 7.0
ikilinganishwa na 6.6 za mwaka uliopita kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji
na uhifadhi wa bidhaa za nyama, samaki, matunda, mboga za majani na mafuta.
Shughuli
nyingine zinahusisha uzalishaji wa bidhaa za vyakula, nguo na simenti, utoaji
wa huduma na uchumi zikiwemo za ukarabati wa magari, pikipiki na vifaa vingine
vya majumbani zikikua kwa asilimia 7.1 ikilinganishwa na asilimia 6.6 ya
kipindi kama hicho kwa mwaka 2013.
Bw.
Oyuke ameeleza kuwa shughuli za uchukuzi na mawasiliano zimekua na kufikia asilimia 16.8 katika kipindi hicho huku
huduma za hoteli na migahawa zikifikia kasi ya ukuaji wa asilimia 4.0, shughuli
za uendeshaji wa Serikali zikiwa asilimia 4.8, Elimu asilimia 6.3, huduma za
afya na shughuli nyingine zikikua kwa
asilimia 4.8.
Amebainisha
kuwa sekta ya umeme katika robo ya pili mwaka 2014 imeendelea kukua kutokana na
kupatikana kwa vyanzo mbadala vya kuzalisha umeme hususan ugunduzi na matumizi
ya gesi nchini ambayo yameondoa tatizo la utegemezi wa umeme wa maji katika
kuzalisha umeme.
“Kwa
kipindi kirefu sekta ya umeme imekuwa na mawimbi kwa kiasi kikubwa , umeme wetu
umekuwa wa kutegemea maji ya mvua, baada ya juhudi za Serikali na kugundulika
kwa nishati ya Gesi nchini na kupatikana chanzo mbadala cha nishati tatizo hili
limeshghulikiwa sasa sekta hii imeimarika” Amesema.
Amesema
Tanzania sasa inafanya vizuri kiuchumi katika nchi za Afrika ya Mashariki kwa
kuendelea kushika nafasi ya pili ikifuatiwa na Uganda, Rwanda na Burundi na
kuongeza kuwa hali ya amani na utulivu iliyopo nchini inaiweka Tanzania katika
nafasi nzuri ya kukua zaidi kiuchumi.
Aidha amefafanua kuwa katika Afrika Mashariki,
Tanzania inaendelea kufanya vizuri
katika sekta ya utalii kwa kuwa na ongezeko la idadi ya watalii
wanaoingia nchini kutokana na hali ya usalama na amani iliyopo .


Post a Comment