Na Mwandishi Wetu, HANDENI
SHIRIKA
la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii NSSF Tanzania, limejitokeza tena kudhamini
Tamasha kubwa la Utamaduni linalojulikana kama ‘Handeni Kwetu’,
lililopangwa kufanyika Desemba 13 mwaka huu, katika Uwanja wa Azimio
(Kigoda Stadium), wilayani Handeni, mkoani Tanga.
Hii ni
mara ya pili kwa mfuko huo wa hifadhi kudhamini tamasha hili la
utamaduni lilioanza mwaka jana, ambapo lilifanyika kwa mafanikio makubwa
kwa kushirikisha vikundi vya ndani na nje ya Handeni, wakiwamo wa
jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
jana jijini Dar es Salaam, Mratibu Mkuu wa Tamasha hilo, Kambi Mbwana,
alisema kwamba kujitokeza kwa NSSF ni kitendo cha kiungwana
kinacholiweka tukio lao katika kiwango kizuri na mafanikio makubwa.
Alisema
kwa kuliangalia hilo, wameamua kutoa haki ya jina, ambapo sasa tamasha
lao litakuwa linajulikana kama NSSF Handeni Kwetu, wakiamini kuwa ni
ishara nzuri ya ushirikiano baina yao na wadau wote wa shirika hilo.
“Yapo
mashirika mengi Tanzania bila kusahau kampuni ambazo zingeweza kudhamini
matukio ya aina hii ambayo yana mchango mkubwa kwa taifa letu, lakini
baadhi yao yamekuwa magumu mno kudhamini au hata kuyasaidia kwa namna
moja ama nyingine.
“Shirika
kama NSSF linapoamua kuingia kudhamini ni kuonyesha jinsi
wanavyoithamini jamii yao, jambo ambalo kwetu sisi ni furaha kubwa na
kuona ipo haja ya kutafuta namna ya kurudisha fadhira kwa wadau hawa
muhimu nchini Tanzania,” alisema.
Kwa
mujibu wa Mbwana, siku ya tamasha, kutakuwa na shughuli ya kusajili
wanachama wapya wa kujiunga na NSSF, ili waweze kunufaika na huduma za
mafao kwenye Shirika hilo kubwa la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii hapa
nchini.


Post a Comment