
Bw. Salaah, Mkurugenzi
wa Home Shopping Centre
---
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
Hivi karibuni kumezuka taarifa za upotoshwaji zilizotolewa kwenye
mitandao ya kijamii kwamba Serikali ya Tanzania imemteua Bw. Salaah, Mkurugenzi
wa Home Shopping Centre, (pichani ) kuwa Konseli wa Heshima (Honorary Consul)
kwenye mji wa Guangzhou kwenye Jimbo la Guandong.
Watoa taarifa hizo, hawakutoa ushahidi wowote
kuthibitisha madai yao zaidi ya kutoa picha mbalimbali za Bw.Salaah kutoka
kwenye mitandao mingine ya kijamii.
Taarifa hizo sio za kweli.
Kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za mahusiano ya
kidiplomasia ya China, nafasi ya Konseli wa Heshima haitambuliki 'mainland'
China. Kwa maneno mengine hakuna nchi yoyote duniani inayoweza kuteua mtu
kuwa Konseli wa Heshima katika eneo lolote la China isipokuwa Hong Kong ambako
kuna mamlaka huru za utawala zinazofuata sheria zake.
Kwa faida ya umma, ni vema kufafanua kwamba
Nchi ya China inakubali nchi za Nje kufungua Ubalozi kamili (Embassy) ambao
makao yake yanatakiwa kuwepo katika mji Mkuu wa China- Beijing na Konseli Kuu
ama kwa lugha iliyozoeleka Ubalozi Mdogo (General Consulate) ambao unaweza
kufunguliwa kwenye makao Makuu ya mji wowote ule katika Majimbo ya China.
Watu wengi wamekuwa wakichanganya Ubalozi Mdogo
au Konseli Kuu (General Consulate) na Konseli (Ubalozi) wa Heshima
(Honorary Consulate). Konseli Kuu (General Consulate) ni sehemu ya
Ubalozi (ndio maana wengi huuita Ubalozi Mdogo) ambapo kiongozi wake na maafisa
wake wote ni watumishi wa Serikali kutokea Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa. Masharti ya kuwa Mkuu wa Konseli 'General
Consulate' lazima uwe Afisa Mwandamizi wa Mambo ya Nje mwenye uzoefu usiopungua
miaka 10 ya Utumishi katika Wizara ya Mambo ya Nje.
Kwa muktadha huo, taarifa kwamba Bw.Salaah
ameteuliwa kuwa Balozi wa Heshima wa Tanzania huko Guangzhou sio kweli
kwasababu Sheria za China haziruhusu uwepo wa nafasi hiyo. Aidha, Bw
Salaah hawezi kuwa Balozi Mdogo (Consul General) kwa kuwa yeye sio mwajiriwa wa
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Hivyo habari
zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii sio za kweli na zinalenga kuupotosha
umma.
IMETOLEWA NA
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
OCTOBER 30, 2014


Post a Comment