STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 2.10.2015
MGOMBEA nafasi ya Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM na Makamu
Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein amewahakikishia
wananchi wa Zanzibar kuwa atakapoingia madarakani katika awamu yake ya
pili ya uongozi sekta ya michezo atazidi kuiimarisha.
Dk.
Shein ambaye pia, ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi aliyasema hayo katika Mkutano wa CCM wa Kampeni za uchaguzi
huko Kiwani, Mkoa wa Kusini Pemba uliohudhuriwa na maelfu ya wanaCCM
pamoja na wananchi yakiwemo makundi ya vijana.
Katika
maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa atahakikisha sekta ya michezo
inaimarika zaidi katika kila nyanja ili Zanzibar irudi katika asili yake
ambapo Zanzibar ilitambulikana ndani na nje ya bara la Afrika katika
sekta hiyo.
Dk.
Shein alisema kuwa tayari kwa upande wa Serikali Idara maalum
imeshaundwa kwa ajili ya kushughulikia michezo ikiwa na lengo la
kuiimarisha sekta hiyo hapa nchini.
Aidha,
Dk. Shein alisema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha vuguvugu la
michezo linaimarika sambamba na kuwapa kipaumbele wanafunzi ili nao wawe
na muda wa kushiriki michezo.
Dk.
Shein alisisitiza kuwa michezo kwa vijana na watoto wa skuli ina
umuhimu mkubwa katika kuwajenga kiafya, kiakili pamoja na kuwajenga
watoto na vijana kujenga ushirikiano, upendo na umoja miongoni mwao.
Kutokana
na umuhimu huo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kwa kuwataka wazee
kutowazuia watoto wao kushiriki michezo kutokana na umuhimu wake mkubwa
katika maisha ya mwanaadamu.
Sambamba
na hayo, Dk. Shein alisema kuwa sekta ya michezo katika kipindi cha
miaka mitano ijayo itaimarishwa kwa mujibu wa Ilani ya uchaguzi ya CCM
ya mwaka (2015-2020) ambapo Serikali itatekeleza mambo kadhaa kwa lengo
la kuiimarisha sekta hiyo.
Katika
uongozi wa Dk. Shein Serikali imetekeleza mambo mbali mbali katika
kuimarisha sekta ya michezo ikiwa ni pamoja na kuandaliwa kwa Sera mpya
ya michezo ya Zanzibar itakayoimarisha na kuiendeleza michezo yote.
Aidha,
Serikali imeanzisha mashindano ya riadha ya Wilaya, kwa Wilaya zote
kumi za Zanzibar pamoja na kutoa vifaa mbali mbali vya michezo kwa
wanariadha wa Zanzibar ili kurejesha vuguvugu la michezo ya riadha
ambapo bado utaratibu wa kutoa vifaa hivyo unaendelea.
Pamoja
na hayo, Serikali imewahamasisha wananchi waendeleze michezo ili
wajenge afya zao kwa kufanya mazoezi ya viungo kila siku sambamba na
kushiriki kwenye tamasha la mazoezi ya viungo linalofanyika tarehe 1
Januari ya kila mwaka.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
Post a Comment