JESHI la Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam limewakamata majambazi sugu sita waliohusika kumuua Afisa wa Polisi ASP Elibariki Pallangyo, aliyekuwa akifanya kazi katika kikosi maalum cha kupambana na majambazi.
Hayo yamesemwa jana jijini Dar es Salaam na Kamishna wa Polisi kanda
maalum ya Dar es Salaam,Suleiman Kova ambapo alisema kuwa majambazi hao
wanaongozwa na Omary Salehe maarufu kama Bonge Mzito walifanya tukio
hilo Agosti 4 mwaka huu nyumbani kwa Marehemu huko Yombo.
Kova aliwataja majambazi hao kuwa ni Omary Salehe (39), Saidi Saidi Mzee
(37), Rashid Waston(21), Ramadhan Salum (38), Bakari Salim Rashid (38),
na Hamisi Hamisi (24) ambao wote walikubali kuhusika katika mauwaji
hayo kwa makusudi.
Alisema kuwa majambazi hao walienda kwa ASP Pallangyo na kumvamia usiku
wa manane akiwa amelala na familia yake na kumuua mbele ya familia nzima
ikishuhudia.
Aliongeza kuwa mtuhumiwa namba moja Bw Salehe alikutwa na bastola aina
ya Revolver iliyofutwa namba na baada ya kuhojiwa alidai kuwa silaha
hiyo ndiyo iliyotumika katika tukio hilo.
Kamishna Kova alisema mtuhumiwa huyo alijaribu kuwa toroka Polisi kwa
kuwadanganya kuwa ameficha silaha nyingine mahali na kutaka kukimbia
lakini polisi walimuwahi na kumpiga risasi iliyopelekea akutwe na
umauti.
"Mtuhumiwa mwingine huyu Waston tumemkamata na silaha aina ya Shortgun
iliyokatwa mtutu ambayo waliitengeneza kihenyeji ikiwa na risasi nne na
betri nne zilizounganishwa kwaajili ya kulipua baruti,"alisema Kova
Katika tukio lingine Jeshi la Polisi limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa
wengine saba wa ujambazi wanaojihusisha na kuratibu matukio ya uvamizi
wa vituo vya polisi pamoja na ugaidi ambao watano kati yao ni familia
moja ya ukoo wa Ulatule.
Kamanda Kova alisema kuwa watuhumiwa hao wanahusika na matukio ya
kupanga na kuratibu uvamizi wa vituo vya polisi ambapo pia wamekuwa
wakiendesha kambi za mafunzo huko mkoani Morogoro kwa kutumia fedha
walizokuwa wakijipatia kwa njia ya udanganyifu.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Siad Mohamed Ulatule (67),Ramadhan Ally
Ngande(29),Hamis Mohamed Salum Simba Ulatule (51),Ally Mohamed Salum
Simba Ulatule (65),Nassor Suleiman Ulatule (40), Seleman Abdallah Salum
Ulatule (83) na Said Abdullah Chambeta (40).
"Jeshi la polisi limefanya operesheni hii kuhakikisha tunakomesha kabisa
vitendo vya uvamizi wa vituo vya polisi pia tuna lengo la kuwaondolea
wananchi hofu ya vitendo vya kigaidi nchini,"alisema Kova.
Post a Comment